Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na kabla ya yote kabisa nimpongeze sana Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyofanya kwa mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia Makamu wa Rais, Dkt. Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuendelea kumsaidia Rais wetu kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru sana Waziri wa TAMISEMI na timu yake yote kwa hotuba nzuri sana. Nimshukuru vilevile jirani yangu hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Makamu wake na timu yote na Kamati yote ile kwa kuendelea kuwakilisha Bunge vizuri kusimamia TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiteto peke yake kwa mwaka huu uliopita, tumepata miradi ya zaidi ya shilingi bilioni saba hongereni sana. Wananchi wa Kiteto wamepanga na wameniomba nije niwashukuru sana kwa miradi na heshima kubwa mliyoijengea Kiteto. Madarasa ya shule shikizi peke yake ni shilingi 1,140,000,000 tumejenga madarasa 57; madarasa ya sekondari madarasa 44, shilingi milioni 880; vituo vya afya bilioni moja, vituo viwili vya afya vya tarafa zile na sisi tumepanga, nimeongea Mkurugenzi wangu asubuhi hii. Sisi tutamaliza hiyo kazi tarehe 20 Mei, mwezi mmoja kabla ambao mmetuwekea na nakukaribisha sana Mheshimiwa Waziri ututembelee ili vituo vile vingine vitatu vya tarafa tulivyokubaliana, hapa tulishakubaliana tujenge kwenye tarafa zote, Tarafa ya Makame, Dosidosi na Kibaya. Kwa hiyo, sisi sasa tunawadai tatu tu na kwa kweli kwa speed tunayokwenda nayo na nakualika Mheshimiwa Waziri uje uone ili mtupatie hizo fedha zingine tumalize biashara ya Tarafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata fedha shilingi 1,500,000,000 kwa TARURA tunawashukuru sana. Na namshukuru sana kumuona Engineer Seif hapa, nimualike atembelee Kiteto. Kiteto ni jimbo kubwa sana ni kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro na tuna Meneja pale mzuri sana, shida yetu ni gari. Terrain ya Kiteto, jiografia na umbali wake, kwa kweli mtuletee Landcruiser moja nzuri sana ili kazi hii iendelee kufanyika vizuri zaidi. Namualika vilevile Mkurugenzi Mkuu wa TARURA atembelee Kiteto, karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumepata shule za sekondari mbili mpya shilingi 1,200,000,000 na kazi zinaendelea. Bado sasa na kama kata nne hivi hazina sekondari na kwa kuwa tulishapanga tujenge sekondari kwa kata zote; tukiendelea na kasi hii Kata za Makame, Leseri, Lolela na Ndiligish na uzuri Mwenyekiti wangu wa Halmashauri yupo hapa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaushauri sana ambao nilishakuutoa siku nyingi kidogo; ipo miradi, miradi ya wananchi ambayo imejengwa na nguvu za wananchi na niitumie nafasi hii kuwapongeza sana wananchi Kiteto. Mheshimiwa Waziri nipo na karatasi hapa miradi zaidi ya 119 ipo kwenye stage mbalimbali ambazo zimejengwa na nguvu za wananchi. Wakati tunapata fedha za UVIKO-19 tulitamani zile fedha zingemalizia miradi ile iliyojengwa na wananchi, lakini kutokana na masharti ya fedha za UVIKO tulimuelewa sana aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI kwamba kwa sababu ya masharti tusingeweza kumalizia majengo yale. Lakini kwa kweli kwa juhudi hii iliyooneshwa na wananchi madarasa tu peke yake kwa mfano tu Kiteto tuna miradi 80 inaendelea kwenye vijiji 50 kati ya vijiji 63 vya Wilaya ya Kiteto. Lakini kwenye miradi ya shule shikizi bado tuna uhitaji wa madarasa 26. Lakini kwa zahanati 13 hizi nguvu za wananchi wa Kiteto kwa kweli zina-deserve Serikali iwaunge mkono, kwani tulishatoa ushauri Mheshimiwa Waziri I am sure kwa kweli m-consider hizi nguvu za wananchi ili wananchi waendelee kupata ari ya kuchangia miradi kwa kweli tutafarijika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni la watumishi; ripoti ya CAG inaniambia Kiteto tuna upungufu wa watumishi 651. Sasa watumishi wakipungua kwa kweli ufanisi wa kazi utapungua nao zaidi. Kwa hiyo, naomba na ninafurahi sana kuona kwamba Waziri wa Utumishi ametoa ajira zile na ametoa breakdown kwamba walimu nafasi 12,000, afya 10,000, kilimo 814, mifugo 700, uvuvi 204, maji 261, sheria 53; tunachowaomba ajira hizi zinavyotoka mtumia formula mliyotumia wakati mnagawa fedha za Uviko, wote tupate. Heshima mliyowajengea Wabunge kwa fedha kwa hizi za UVIKO-19 mkifuata formula hii wallah nawaambia wale wanaotaka majimbo haya watapata taabu sana huko mbele kwa sababu mtakuwa mmewajengea heshima Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile maslahi ya watumishi, yakiangaliwa yanaongeza ufanisi zaidi. Na wameyazungumza Waheshimiwa Mabunge hapa kuhusu maslahi ya Madiwani kwa kweli Madiwani wetu wanafanya kazi nzuri zaidi. Tuwaangalie namna ya kuboresha maslahi yao. Lakini vilevile Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa wanafanya kazi kubwa sana tuwaangalie namna ya kuwasaidia ili kujenga ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini walikwisha kusema wengine hapa, tukiwapa uwezo, tukitengeneza zile semina za kuwajengea uwezo Madiwani na Wenyeviti, itaongeza ufanisi zaidi katika kusimamia miradi. Kwa hiyo, zile semina za kuongeza uwezo zitasaidia sana msiziache. Kwa kweli Madiwani wetu wangekuwa wanapata from time-to-time wapate semina kama hizo itaongeza ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la TARURA; nawashukuru sana kwa kuongeza fedha kwa TARURA, lakini ni kweli Ilani ya Chama cha Mapinduzi tulishasema hivyo, tunataka tuongeze fedha nyingi zaidi najua mmeongeza fedha karibu bilioni 100 tena nawapongeza sana. Tunataka fedha za TARURA ziendelee kuwa nyingi zaidi ili barabara za vijijini na mijini zikapate kufunguka; barabara zitaongeza kasi ya uzalishaji. Kwa hiyo, kwa kweli endeleeni kuangalia TARURA kila wakati ikipatikana fedha muongeze fedha kwa ajili ya TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna majengo haya ya Halmashauri; Kiteto tuna jengo la Halmashauri ambalo sasa linaendelea kwa muda mrefu kidogo na kuna fedha karibu milioni kama 400 hivi bado; na mkandarasi anasema kwa kuwa malipo yamechukua muda mrefu kidogo tangu mwaka 2016 anaanza kufikiri kwamba zile fedha ni kidogo. Kwa hiyo, nawaombeni sana, hii miradi mkitoa fedha kwa utaratibu ili zisichelewe mtatuepusha sisi na matatizo ya huko ya kuanza kugombana na wakandarasi. Kwa hiyo, mkitugawia milioni 400 hiyo lile jengo tulimalizie kwa sababu mmeshatumia fedha nyingi sana na tunawashukuru sana. Kwa hiyo, nakukumbusha Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyingine, kwenye ajira hizi hasa za walimu muangalie sana namna ya kuwajali walimu ambao wamekuwa wakijitolea kwa miaka mingi kidogo; hiyo iwe criteria kabisa namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wetu ambao wamemaliza elimu zao na wakaona wasikae bure nyumbani waendelee kutusaidia wanafanya kazi kubwa sana. Mkiweka hiyo kama criteria wale wote ambao wana-volunteer na wanaendelea kutufundishia watoto wetu hiyo iwe criteria namba moja. Mheshimiwa Waziri usikubali kabisa kumuacha mwalimu ambaye ana record ya kuendelea ku-volunteer, mkifanya hivyo mtakuwa mmetenda kazi nzuri sana; na tuangalie wafanyakazi wetu wote wanao-volunteer kwenye sekta fulani fulani kila mtu anaye- volunteer nia yake ikitokea kanafasi basi apewe priority. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli baada ya kusema haya, mimi nakushukuru sana naunga mkono TAMISEMI mtakijengea heshima Chama cha Mapinduzi kwa sababu ukisoma ilani...

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nakushukuru sana naunga mkono hoja ahsanteni sana. (Makofi)