Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na mimi naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kuweza kusimama hapa leo, lakini kipekee naomba nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayofanya ya kutuletea maendeleo Watanzania, lakini pia ya kuongoza Serikali vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba nikiri kwamba, Waziri anatupa nafasi ya kutosha kutusikiliza, anatoa ushirikiano mkubwa, lakini ni mtu ambaye yuko accessible, unaweza kumpata muda wowote unapomuhitaji. Kwa hiyo, yeye pamoja na timu yake nzima, Katibu Mkuu na wasaidizi wake tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasahau mdogo wangu Mheshimiwa Sanga amezungumzia mitambo ya kutengeneza barabara na akatamani Halmashauri ziruhusiwe kununua. Natamani sana aje ajifunze Geita, tulitenga shilingi bilioni 1.4 kila halmashauri kununua mitambo na ile mitambo haijawahi kuonesha value for money. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasikitika sana hiyo mikoa yote naweza nikakutajia Mwanza wanayo, Sengerema wanayo, yote yako grounded, kwa nini, na ni mapya? Yote ni kutoka CAT - Caterpillar, lakini huwezi ku-manage matumizi yake, wakienda site wale wanaoendesha wanabadilisha pump, anabadilisha roller, anabadilisha hiki, matokeo yake yale madude yanakuwa grounded siku mbili hayana kazi. Sasa ni vizuri kuja kujifunza kabla ya jambo hilo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa mzungumzaji, hatuwezi kuacha kufanya maendeleo kwa kuogopa uzembe wa baadhi ya watu ambao hawasimamii wajibu wao waliopewa na Serikali. Kwa sababu watu wa Geita kama hawasimamii hayo ma-caterpillar wanaachia watu wanaenda kuiba na kuchukua vitu haizuwii Halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Mheshimiwa Sanga kununua ma-caterpillar kwa halmashauri nyingine zinazofuata. Ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, hiyo taarifa, umeipokea?
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia na Watanzania wamemsikia, lakini nimesema akajifunze Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Ntaka kuipongeza sana Serikali, ilisema katika Bunge hili kwamba, itatangaza ajira 30,000 na zimetangazwa…
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba Makete tulinunua excavator toka mwaka 1998 na tunalo hadi leo. Anavyosema kwamba tukajifunze kwa watu ambao wame-fail, hakuna utamaduni wa kujifunza kwa watu walio-fail, tunajifunza kwa watu waliofanikiwa, kwa hiyo, hatuwezi kwenda kujifunza Geita kwa watu walio-fail. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Na mnaweza mkajifunza kwa Mheshimiwa Jerry Silaa mpaka leo analo bado. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa yake siipokei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema naipongeza Serikali ilipotimiza ahadi yake ya kuajiri watumishi zaidi ya 32,000 na ninaipongeza kwa sababu tumekuwa na uboreshaji na uongezaji wa miundombinu katika maeneo mbalimbali kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, tulipata fedha za UVIKO, tumejenga madarasa katika Halmashauri ya Mji wa Geita, madarasa zaidi ya 63, lakini kutokana na mapato ya ndani tumejenga shule karibu sita mpya, shule tatu za sekondari na shule mbili za primary. Tunahitaji walimu wa kutosha, lakini kwa bahati mbaya shule zile nyingi zina walimu wachache kwa sababu hapakuwa na staff, hatukuwa na walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaipongeza Serikali, lakini namuomba Mheshimiwa Waziri aje sasa na taarifa inayoonesha uwiano wa mahitaji pamoja na ajira iliyotolewa ili tuweze kujua tume-cover kwa asilimia ngapi. Kwa sababu tunaweza kuajiri 32,000; lakini mahitaji ya mpaka tunaahirisha Bunge mwezi wa pili ilikuwa ni walimu 120,000 lakini pia aje na mkakati tunaziba vipi hilo gape ambalo sasa litakuwepo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri na tunashukuru kwa hizo ajira ambazo zimetangazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nataka kuzungumza, Geita Mji imekuwa na ahadi ya kuwa Manispaa tangu mwaka 2018. Tumezungumza na Waheshimiwa Mawaziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wote waliokuwepo na ahadi mbalimbali zimetolewa. Nataka nitoe vigezo ambavyo vinasababisha Halmashauri kuwa Manispaa; la kwanza ni kuwa na watu wasiopungua laki moja sisi tuna watu takribani laki tatu, lakini la pili asilimia 30 ya wakazi wake wawe na ajira isiyohusiana na kilimo. Sisi pale asilimia 80 ni wafanyabiashara ya madini na biashara nyingine ambazo hazina uhusiano na kilimo, tuko mjini, lakini la tatu inasema kuwe na walau kiwanda kikubwa kimoja, tuna mgodi mkubwa pale ulioajiri zaidi ya watu 12,000; lakini la nne inasema tuwe na uwezo wa asilimia 70 ya uwezo wa kujitegemea Halmashauri, Halmashauri ya Geita Mjini ina uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 83, maana yake tumeshavuka hiyo habari, lakini lingine inasema kuwepo na huduma mbalimbali ya kwanza elimu ya watu wazima tunayo, hospitali ya rufaa tunayo, chuo kikuu tunacho, ukumbi wa mikutano tunao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kumwambia Mheshimiwa Waziri tunataka Geita ipewe hadhi yake ya kuwa Manispaa. Mlituongezea sharti moja tu la kupata master plan, tumekamilisha master plan na tayari Geita tunayo master plan. Sasa tunakuomba tupewe hadhi ya kuwa manispaa kwa sababu, mnatuchelewesha kuendelea, tunakusanya zaidi ya bilioni 15 kwa mwaka kwa hiyo, tunataka sisi tukimbie ninyi mnatusimamisha, tunaomba tupewe tuweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongea ni jambo la TARURA. Kwanza naipongeza sana Wizara imefanya kazi vizuri, naipongeza sana Serikali, kwa mujibu wa takwimu kwa miaka minne yote mfululizo TARURA walikuwa wanapewa kwa wastani wa fedha wanazoomba; walianza kuomba mwaka 2019 shilingi bilioni 639 walipata fedha kwa asilimia 25 takribani, mwaka 2020 waliomba shilingi bilioni 699 wakapata asilimia 24 na asilimia 38 asilimia 35, lakini mwaka huu wa fedha unaoisha waliomba shilingi bilioni 717 wakapata kwa zaidi ya asilimia 96, naipongeza sana Serikali kwa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo nataka kusema hapa TARURA inasimamia mtandao wa barabara zaidi ya asilimia 90 Tanzania kwa hiyo, ni chombo ambacho lazima kitazamwe upya kiongezewe uwezo ili kiweze kusaidia miundombinu, lakini jambo moja Mheshimiwa Waziri Halmashauri zote uliziongezea pesa, ulitoa mwanzo milioni mia tano-mia tano fedha za jimbo za barabara ukapandisha bilioni moja, lakini Geita Mjini ukaiacha na milioni 500.
Mheshimiwa ninaomba hiyo pesa iongezeke ili tuweze kutengeneza barabara, barabara ni mbaya na Geita imekaa kwenye muinuko kila mvua inayonyesha maji yanaenda kwenye miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niipongeze pia Serikali kwa mradi wa TACTIC, tumeusubiri kwa miaka mingi sana, tumekaa tukiusubiri, lakini sasa unakuja. Hoja yangu hapa Mheshimiwa Waziri wakati ule tunatekeleza mradi wa LGSP tulijikuta mradi una- phase out fedha ziko kwenye account. Sasa tunataka tuiombe Serikali this time kwa sababu tunakwenda kwa pamoja tutakaposema tunaanza paa, miradi yote iliyotajwa kwenye mradi itangazwe ili tusiache fedha kwenye account, lakini barabara zitengezwe. Tumeipongeza sana Serikali kwa mradi huo na tunaomba jambo hilo liweze kufanyiwa mchakato mapema ili tuweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia ni kuhusu Machinga Complex. Nampongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa kwetu wa Kamati amezungumzia kuhusu Dodoma, tulikwenda kutembelea machinga inayojengwa hapa Dodoma, mimi nikataka kukuuliza Mheshimiwa Waziri, hawa viongozi wetu wa mikoa wanakwenda kwenye semina tofauti?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia modal waliyoitumia Dodoma, namna walivyo-handle machinga ni tofauti na machinga nchi nzima. Ukienda mikoa yote machinga wamekuwa displaced, wamepelekwa kwenye maeneo ambayo wamefilisika, Dodoma wameachwa wanafanya kazi zao, mpaka leo tunavyozungumza wako barabarani, lakini wanajengewa miundombinu na miundombinu ile inaonesha wazi kwamba kuna mtu amekaa ame-plan. Sasa Dodoma walikuwa na formula tofauti na mikoa mingine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu kingine cha mwisho Mheshimiwa Waziri, nimeona Dodoma Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kujenga machinga. Naamini tu sababu ni makao makuu, unakuja na package gani ya mikoa mingine ya Halmashauri nyingine ili kama hazina uwezo wa kutenga fedha hizo kwa sababu kundi hili ni muhimu ziweze kutengewa fedha kujenga kwa sababu, sasa hivi ninavyozungumza na wewe machinga almost wamefilisika na watu wengi sasa usije ukashangaa ujambazi ukaongezeka kwa sababu hawana kazi ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo nataka kuzungumza hapa ni hoja ya mifumo. Ilikuja moja ya idara zinazoshughulikiwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni eneo la uboreshaji wa mapato. Halmashauri yangu na Halmashauri nyingine wamebinafsisha ukusanyaji wa mapato, sasa nataka kutoa mfano; mmempa uzabuni wa kukusanya takataka mwananchi kwenye mitaa miwili ukamwambia kwa mwezi akusanye milioni tano, lakini asilimia 80 ya fedha ni za kwake, anakusanya anapata kwenye mashine yake inasoma alikusanya milioni 3.8, zile fedha unazikataa unasema hapana kalete milioni tano, akizikosa anawekwa ndani mpaka ifike milioni tano, lakini akishaweka milioni tano unamrudishia milioni nne na laki mbili. Kwa nini watu wa mifumo wasi-develop system ambayo computer iwe ina-tally ambazo zinatakiwa zipokelewe na Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama ninatakiwa kwenye shilingi mia hela ya Serikali ni shilingi ishirini, computer imuoneshe mzabuni kupeleka shilingi ishirini kuliko kumng’ang’aniza apeleke milioni kumi anawekwa ndani, anakopa halafu baada ya siku mbili unamrudishia milioni tisa, kazi zimesimama mwezi mzima. Sasa hivi mji wangu wa Geita ni mchafu kwa sababu wazabuni wote wamekimbia, kwa nini, kwa sababu mwingine anadaiwa laki tano, anadaiwa laki nne, lakini katika milioni kumi hela ya kwetu ya Serikali ni shilingi milioni 1.2. Mfumo unaweza kutengenezwa ili kuweza kudhibiti suala hilo. Pesa inayopokelewa pale iwe ni ile ambayo kisheria inayotakiwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)