Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hii hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Nakushuru sana Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Naibu Mawaziri mnafanya kazi nzuri ni imani yangu kwamba tukiendelea hivi basi tutaweza walau kutatua changamoto nyingi zinazowahusu wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naendelea kuishukuru sana Serikali kwa maana ya Mheshimiwa Rais Samia tumeweza kupata fedha za kutosha kujenga vyumba vya madarasa, kujenga zahanati, vituo vya afya pamoja na barabara. Kwa hiyo, nawapongezeni sana, lakini bahati nzuri ni kwamba fedha zimekuja na tumezisimamia vizuri, lakini huu usimamizi mzuri huu kwa namna yoyote ile tusingeweza kusimamia pasipokuwa na madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, hiyo kazi nzuri ambayo inafanyika na hata kwa sasa safari hii inaonekana tena fedha nyingi zaidi zitakuja, sasa mimi ombi langu ni vizuri na wale Waheshimiwa Madiwani tukaendelea kuwajali, lakini hali kadhalika na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa sababu hao ndiyo wanaofanya kazi kubwa huko hasa tunapokuwa hatupo majimboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo katika kuteleleza hayo, maana mimi bahati nzuri nimekuwa Diwani mwaka 2000 kabla sijawa Mbunge mwaka 2005 mojawapo ya mambo yaliyokuwa yanafanyika ilikuwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya Madiwani lakini na kuwajengea uwezo ili waweze kuzisimamia. Sasa umezungumza vizuri katika hotuba yako, lakini bado hujazungumza namna ya kuendelea kuwajengea uwezo pamoja na maslahi yao kwa sababu wale watu wanasimamia fedha nyingi sasa, lakini ni kwamba uwezo wao kiuchumi ni mdogo sana. Kwa hiyo, nadhani hilo utakapokuwa unajibu ni imani yangu kwamba utalijibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine pamoja na miradi mingi na fedha nyingi tulizozipata kwangu pale Mheshimiwa Waziri, aidha, mambo yalifanyika kimakosa, aidha, kwa makusudi mfano, kwenye zile fedha zilizokuja fedha za tozo na fedha za UVIKO kwenye barabara mimi nipata shilingi milioni 500 peke yake nilipokuja kuuliza kulikoni nikaambiwa kuna fedha za TACTICS pamoja na miradi ya kimkakati. Sasa at least katika majimbo mengine zilipatika shilingi bilioni 1.5 mimi nimeambulia shilingi milioni 500 lakini mpaka leo hivi ninavyozungumza hakuna dalili ya fedha za kimkakati wala za TACTIC. Kwa hiyo, nitaomba wakati unasimama unieleze hilo, vinginevyo mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kuanza na shilingi yako Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ipo ile miradi mfano; fedha zimekuja, lakini vile vituo vya afya vya zamani vilivyochoka, ninacho Kituo cha Afya cha Bwiru pale, leo ukikiona ni afadhali hata zahanati, lakini zipo shule za msingi kama Mtakuja yaani imechoka yaani ile inahitaji tui-condemn. Kwa hiyo, pamoja na mengine yote ningekuomba utakapopata nafasi baada ya Bunge hili twende Musoma nikutembeze na hivi wewe ni mjukuu wangu nitakutembeza mradi kwa mradi uweze kuiona ili uweze kuona kwamba ni kwa kiasi mtaweza kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilidhani kwamba kwenye upande huo Mheshimiwa Waziri hebu basi angalia namna ambavyo tutakavyopata fedha kwa ajili ya kufidia yale mapengo ya barabara ambazo hazikujengwa. Lakini cha ajabu zaidi sasa kwa miaka mitano mfululizo Musoma hatujawahi kupata fedha za maendeleo kwa ajili ya barabara hatujawahi yaani tofauti na fedha tulizo bahatisha za World Bank ambazo tumezipigania kwa muda mrefu hakuna fedha yoyote ambayo imeshakuja na ukiangalia kwa muda wa miaka mitano kwa namna ambavyo Madiwani wangu wanafanyakazi nzuri hatujawahi kupata hata hati chafu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ni imani yangu kwamba katika yale yote ambayo ni ya kimsingi katika kutusaidia mji wetu wa Musoma ili nao uweze kuendelea basi katika bajeti hii utaweza kusema namna ya kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme jambo moja ambalo ninadhani aidha tunaliona, lakini tunajifanya kama hatulioni. Mheshimiwa Waziri umetoa takwimu nzuri kwamba darasa la saba wanamaliza wanafunzi zaidi ya 1,130,000; kidato cha nne wanamaliza wanafunzi zaidi ya 880,000; kidato cha sita wanamaliza wanafunzi 80,000; tafsiri yake ni nini? Kwamba kumbe basi kila mwaka wanafunzi au vijana zaidi ya milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira, yaani wanapaswa waanze maisha lakini ukiangalia sasa kama wanapaswa waanze maisha na jukumu mojawapo kubwa la Serikali ni pamoja na kuwapatia wananchi wake ajira, sasa leo ni tatizo ambalo linatutesa, kwangu mimi pale Musoma vijana wangu wengi hawana ajira, lakini hawana ajira sijasikia kwenye bajeti yako ni namna gani mmewatengenezea mazingira kwamba sasa kila wanapomaliza hawa zaidi ya milioni moja wakimaliza shule mmewaandalia mazingira gani ya ujasiriamali aidha, mazingira gani ya kuweza kupata ajira.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilipomuuliza Mheshimiwa Bashe hapa swali la nyongeza alisema kwenye bajeti hii ameandaa fedha kwa ajili ya miradi ya kilimo kwa ajili ya vijana ili waweze kujiajiri, lakini wanatatizo moja kubwa la maeneo sasa nilitegemea kabisa kwamba na wewe hapo ungeweza ku-chip in kwa maana ya kutenga fedha kwenye kila halmashauri ili tuweze kuandaa maeneo ili atakapokuwa na fedha kwa ajili ya vijana basi tayari tuna maeneo ya kuweza kuwa-accomodate.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine sambamba na hilo wapo vijana wetu wa kimachinga, wapo vijana wetu wa bodaboda, nashukuru kwamba hilo nililipigia kelele mwisho tukawa- official rise wanaendelea na shughuli zao pamoja na kwamba bado yapo mambo ya kurekebisha, lakini wale wamachinga wale ni watu ambao wao ili waweze kufanyabiashara wanatafuta watu walipo, sasa cha ajabu kila mnaposema mnawapanga tunawapanga kwenye maeneo ambayo hakuna watu na wao kwa sababu biashara yao ni ndogo ndogo maana yake ni kwamba lazima tuwaandalie maeneo ambayo tayari wapo watu. (Makofi)
Sasa kila mara hilo nalo hatujalitekeleza vizuri sana na hata katika bajeti yako sijasikia namna gani umeweza kuwagusa. Kwa hiyo, mimi niombe hapa sasa kwamba pamoja na Wizara yako na wizara zingine ni vizuri kipaumbele chetu kuliko yote ni pamoja na ajira kwa watu wetu ni imani yangu kwamba kila Wizara, juzi nilisikia hapa mfano; TRA wametangaza ajira 1000 napo wanajigamba kwamba ajira nyingi zimetoka ajira 1,000 hivi ninyi ajira 1,000 katika watoto zaidi milioni moja ambao kila mwaka wanakuwa tayari kwa ajili ya kuanza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba kila Wizara iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba inatoa ajira kwa kila mwaka na kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia vijana wetu.
NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nawashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)