Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mungu wa Rehema kutujaalia uzima na afya na wale wanaotekeleza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya kuwaletea Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake tumeona maono yake, tumeona dhamira yake na kwa hakika tumeona huruma yake kwa ajili ya Watanzania na sisi tunao wajibu wa kuendelea kumuombea na kumuunga mkono sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri kwa kutuwasilishia hotuba nzuri leo asubuhi. Hotuba ambayo imetuonesha dhamira ya dhati ya ofisi hii katika kuwaletea maendeleo wananchi. TAMISEMI ndiko ambapo wananchi walipo wengi. TAMISEMI ndiyo inatoa huduma nyingi kule vijijini. Ukiongelea Halmashauri au Mamlaka za Serikali za Mitaa unaongelea wananchi wa kwenye vitongoji. Maana yake ni kwamba kule tuliko sisi wananchi. Kwa hiyo, leo tumeona dhamira ya Serikali kupitia Wizara hii na kwa hakika nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa namna ambavyo amekuwa akitupa ushirikiano kwa muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mara tumekuwa tukimpa ushirikiano na kero ambazo zipo kwenye maeneo yetu amekuwa akizitatua kwa wakati, kwa hakika tunasema wewe ni hazina ya Taifa na tunaendelea kukuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwa wenzetu Naibu Mawaziri wake Davis Silinde ndugu yangu pamoja na Ndugu Dkt. Ndugange mnafanya kazi nzuri sana. Kipekee kabisa Profesa Shemdoe pamoja na wenzake wote katika Wizara watendaji mnafanya kazi nzuri ya vijijini na niendelee kukumbusha tu kwamba kule Kipompo ambapo Profesa Shemdoe uliahidi shule ya msingi itapauliwa wananchi washajenga madarasa manne pamoja na nyumba ya mwalimu, tunasubiri mkapaue ili shule ile iweze kusaidia wananchi ambao watoto wanatembea kilometa tisa kutoka pale wanakoishi kitongoji cha Kipompo katika Kata ile ya Mang’onyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa maana ya mwaka mmoja huu ambao tunauona, Halmashauri ya Ikungi tumepokea zaidi ya shilingi bilioni saba ambazo kwa hakika ni fedha nyingi sana za maendeleo ambazo leo tunaona ziko kwenye maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu na zaidi tumeona jambo kubwa lililofanyika la kujenga madarasa 67. Tulipata jumla ya shilingi bilioni 2.6; ni fedha nyingi kwa wakati mmoja. Sisi tunashukuru sana na tunaipongeza Serikali kwa hatua kubwa ya mapinduzi makubwa ya kielimu katika Halmashauri yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema hayo pia tumepata eneo la vituo vya afya. Lakini nishukuru sana tumepata Hospitali yetu ya Wilaya imepata shilingi milioni 800 inakwenda kukamilika sasa ambayo tulikuwa hatuna huko nyuma. Lakini kwenye eneo hili niseme tu kwamba katika Kata zangu 13 za Jimbo la Singida Mashariki, Mheshimiwa Waziri mimi nilipata kituo kimoja tu. Kata 13 za Jimbo la Singida Mashariki tumepata Kituo cha Ntuntu. Nashukuru kwamba tumepata shilingi milioni 500 na tunaenda kumaliza kabisa tatizo la afya katika eneo lile la Kata ya Ntuntu ambayo iko mbali na Wilaya. Lakini kwa maana ya Kata 12 zilizobaki, niombe sana kwenye bajeti hii angalau tukipata vituo vingine vitatu tutakuwa tumegusa maisha ya wananchi. Tukiweza kupata Misuwakha, tukiweza kupata katika Kata ile ya Mang’onyi, tukapata na Kata ya Isuna, tutakuwa tumesambaza vizuri huduma na tutawasaidia wananchi wetu kutembea kwenda kupata huduma mbali. Nikisema hivyo, kwa sababu naenda sambamba pamoja na watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika Halmashauri yetu ya Ikungi tuna upungufu wa walimu wengi sana. Walimu ukiangalia hesabu yetu tunahitaji walimu 2,685 lakini tunao walimu 1,305 tu maana yake tuna upungufu wa walimu 1,380. Walimu hawa ni wengi sana katika kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu yetu. Leo tunataka ufaulu upande, lakini hatuwezi kupandisha ufaulu bila kuwa na walimu wa kutosha, hatuwezi kusema leo tunaenda kuongeza uwezo wa kufundisha watoto wetu kwenye shule za msingi, unakuta walimu wako watano kwenye shule ya msingi yenye watoto zaidi ya 700 usitegemee mapinduzi ya elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana tumeweza kupata fedha katika shule shikizi, shule za Simbikwa, shule za kule Talu Mlimani, shule ya kule Mau, shule ya Mboghantigha tumepata kule ambapo sasa tumepata madarasa na shule zile zinakwenda kusajiliwa. Lakini leo hii tumepanga tusajili zile shule zianze, lakini ina mwalimu mmoja, wawili katika shule, usitegemee mabadiliko makubwa ya kitaaluma katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana tuisaidie Idara ya Elimu ipate walimu wa kutosha ili hata Afisa Elimu anaposimamia awe na uwezo mzuri wa kuelekeza namna ambavyo Serikali inataka kuboresha elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongelea eneo hilo nikikazia zaidi kwenye eneo la afya pia tunao upungufu mkubwa sana. Kuna zanahati unakuta ina mganga au nurse mmoja ni kilometa zaidi ya 60 kutoka Makao Makuu ya Wilaya na kila mwezi anatakiwa apeleke report. Siku anapeleka report au anakwenda benki kutafuta mshahara, ile zahanati inafungwa, huduma haitolewi, ugonjwa hauna taarifa, hauwezi kujua leo umepeleka report. Kwa hiyo, wananchi hawawezi kupata huduma kwa sababu hatuna waganga au wahudumu wa afya wa kutosha. Niombe sana Serikali mnapokuja mje mtuambie mkakati ambao mmeupanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili la elimu, lakini pia na kuwasaidia vijana wetu ajira. Mimi niseme tu kwamba naishukuru Serikali tulipata fedha au tulitengewa shilingi bilioni mbili kujenga Chuo cha VETA pale Ikungi. Leo tunavyoongea mimi na wewe kile chuo sasa hivi kimesimama ujenzi. Watu wa VETA walipewa kandarasi ya kujenga kile chuo, namshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa Kipanga ulikuja, ulivyokuja ukasema sasa tutabadilisha iende Halmashauri. Hivi ninavyongea wamerudisha tena imekwenda VETA, hivi ninavyoongea sasa hivi wale wakandarasi hawajalipwa, mradi umesimama, vifaa hakuna, zaidi ya mifuko ya cement 1,800 ilikuwa inaletwa Ikungi imepotea njiani. haijafika. Leo hii imesimama ujenzi, hakuna kinachoendelea na kuna watu wanadai. Usitegemee hawa vijana ambao tunategemea wakasaidiwe elimu pale hawana mahali pa kufundishiwa. Kwa hiyo, usitegemee kwamba tutapata mabadiliko ya kielimu au kusababisha ajira za wananchi wetu. Kwa hiyo, nilitaka nilieleze hili eneo katika kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu katika eneo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la barabara; barabara kweli tumepata fedha shilingi bilioni 1.5 kwenye maeneo yetu imeleta mabadiliko makubwa tunaipongeza Serikali. Lakini kwa barabara za vijijini ambazo tunahitaji vivuko na madaraja, fedha ambazo tunasubiri hizi za pamoja na bajeti hatutengi tutakuwa tunategemea kitu ambacho hatujakipanga.

Kwa hiyo nimeona hapa kuna fedha mmeongeza kweli lakini fedha zile hazitoshi, mngekuwa kwenye fedha za maendeleo zinatoka moja kwa moja TARURA tunatenga kwa ajili ya vivuko na madaraja ili Mameneja wa Wilaya wabaki kwenye eneo la kutengeneza barabara tu na matuta. Lakini ukisema leo wafanye kazi ile ile shilingi milioni 800 haifiki hata shilingi bilioni moja kwa mwaka usitegemee mabadiliko ya barabara katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Kwa hiyo niombe sana tuwe na mpango maalum wa fedha maalum ambazo zinakwenda kwa ajili ya kujenga madaraja na vivuko ili isaidie barabara zetu za vijijini. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE: MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo maneno naomba nirudie tena kushukuru, lakini naomba niseme naunga mkono hoja, kuna mambo ya kimkakati ambayo nitamuandikia Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya maboresho. Ahsante sana. (Makofi)