Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kupata nafasi niweze kuchangia kwenye hotuba nzuri sana ya Ofisi ya TAMISEMI.
Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake, vijana mahiri, wachapakazi, wanaokimbia huku na huku na mimi nawashukuru sana Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wote wameshafika Chunya, tunawashukuru sana kwa kazi nzuri ambayo wamendelea kufanya, lakini pia tuipongeze Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo imeweza kushusha miradi mingi kupitia TAMISEMI, imeweza kushusha fedha nyingi sana kupitia TAMISEMI, tumpongeze sana Mama yetu Samia Suluhu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kufanya na ninyi kama wasaidizi wake mmekuwa mnaweza kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tumekuwa mashahidi namna ambavyo fedha hizi zimekuwa zinakwenda kwenye majimbo yetu na kwenye Wilaya zetu. Nianze tu kuzungumza kwenye upande wa TARURA. Tumeona namna ambavyo kila mmoja hapa ameweza kuguswa na pesa nyingi sana ambazo zimekwenda kwenye upande wa kujenga barabara hasa barabara ya TARURA. Pesa hizi zimeshuka nyingi ambazo zimeweza kwenda kule kwenye vijiji vyetu, kwenye kata zetu, kwenye Wilaya zetu na ameweza kuchechemua uchumi wa kwenye maeneo yetu yale na kwa mara ya kwanza sisi tumeweza kupata fedha nyingi, kwa Wilaya ya Chunya peke yake tumepata zaidi ya shilingi bilioni 2.3. Ni fedha nyingi ambazo tumezipata kipindi chochote ambacho Wilaya hii imeumbwa, tuipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeendelea kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pesa hizi pamoja na kufika huko tumeona namna ambavyo zimeweza kuchechemua uchumi wa nchi, namna ambavyo wakandarasi wameweza kuzidiwa kwa miradi mingi waliyokuwanayo. Leo hii wakandarasi tunawadai kazi siyo pesa, pesa zimekwenda huko nyingi za kutosha, lakini wao ndiyo wamekwama kutekeleza kwa wakati. Aidha, hawana vitendea kazi, hawana wataalam wa kutosha ambao imepelekea mpaka hii miradi kwenda kwa kusuasua. Lakini kwa upande wa Serikali tumeona kwamba fedha zimeweza kwenda kwa wakati. Zimeweza kwenda kwa wakati, tunaweza kuipongeza sana Serikali hii imeweza kufanya mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja nakufanya mambo makubwa haya tuwapongeze tumeona kwenye hotuba yako hapa ya bajeti yale mawazo tuliyokuwa tukiishauri Serikali mara kwa mara mmeweza kuyachukua. Tulikuwa tunawaambia kwamba mwaka wa fedha unaanza Julai, ninyi mlikuwa mnakaa mnasubiri Julai mwaka wa fedha unapoanza ndiyo mlikuwa mnaanza kutangaza tender kwa ajili ya kufanya hizi kazi za ujenzi wa barabara. Lakini tumewashauri mara kadhaa, nimeona kwenye bajeti yako umesema. Sasa haya mmeyapokea na mmeweza kuyafanyia kazi. Sasa hivi mnaanza kutangaza hizi tender ili kuanzia mwezi Julai mwaka wa fedha unapoanza maana yake watu wanapewa sasa mikataba hii na kazi zinaanza kwenda kwa wakati. Hii tunawapongeza sana na kwa kweli ule utaratibu wa nyuma ule ulikuwa unatukwamisha sana. Leo hii sisi kwa Chunya unakuta fedha zilitoka toka mwaka jana mwezi wa nane wa tisa leo ndiyo miradi ya barabara inatekelezwa. Watu wamepata shida kipindi chote cha masika wakati fedha zipo. Lakini kwa utaratibu huu ambao mmeanza nao mmetuambia leo kwa kweli tunawapongeza sana mmechukua ushauri wetu uliokuwa mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tumeona kwamba sasa TARURA pamoja na kazi nzuri ambayo wanafanya lakini na wao pia kuna changamoto wanazo, wana changamoto za wafanyakazi, za ma-engineer, sisi Wilaya yetu ya Chunya tuna ma-engineer watatu almost kama wanne, Wilaya ni kubwa sana kwa Mkoa wa Mbeya tunakaribu ya eneo la ukubwa zaidi ya asilimia 40 ya Mkoa mzima wa Mbeya, sasa unapotupa wahandisi watatu, na bosi wao mmoja pale Mkuu wa Idara maana yake unatulinganisha sisi na Wilaya nyingine, sisi tunakuwa kwenye wakati mgumu kwenda kusimamia hii miradi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake kule barabara za vijijini zinakosa usimamizi mzuri wa ma-engineer hawa waweko kule kwa wakati barabara zinajengwa wakati mwingine wakati mwingine zinajengwa mkandarasi anajenga chini ya kiwango, lakini mainjinia wetu hawa wanashindwa kufika maeneo husika kwa wakati kuweza kusimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nishauri kwenye ajira ambazo zinakuwa zinatolewa hizi pamoja na kuajiri ma- engineer hawa tuajiri pia na wale ma-engineer wa kati wale ma- technician wawepo, wawe ndio wanashinda kulekule site muda wote, wataweza kutusaidia sana kuhakikisha kwamba thamani ya fedha inayotolewa inakwenda sambamba na kazi ambayo inakwenda kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine kwenye upande wa TARURA ni vitendea kazi hasa magari. Wilaya zetu hizi zinatofautiana Wilaya za mjini na wilaya za vijijini, Wilaya ya mjini ukiwapata magari ya kawaida, ukiwapa pickup za kawaida, wao zinaweza zikawasaidia sana, lakini kwa Wilaya zetu sisi zenye miundombinu mibovu ya barabara kama Wilaya yetu ya Chunya kuweza kuwapa pickup ya kawaida ni ngumu sana utekelezaji wake kwenda kusimamia hii miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana wakati ugawanyaji huu wa rasilimali hizi za magari unafanyika Wilaya sisi hizi zenye miundombinu dume tuweze kupata yale magari ambayo yanaweza yakahimili, tuweze kupata landcruiser pickup ziweze kufanya kazi kule. Leo tunapozungumza hapa sisi pale Wilaya ya Chunya tuna pickup moja ambayo pickup yenyewe bado ni mbovu, leo ni spana mkononi matokeo yake ma- engineer wanashindwa kwenda kufanya kazi kufikia miradi kwa wakati, kila siku wanabisha hodi kwa Mkurugenzi kwenda kuomba magari pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana kwenye bajeti zenu hizi mnapotenga vitendea kazi muone miundombinu ya Wilaya za vijijini hizi tuweze kupata magari ambayo yataweza kutusaidia kuweza kufikia na kuweza kusimamia hii miradi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lakuweza kuchangia ni kwenye upande wa elimu, niipongeze Serikali imefanya kazi kubwa, imeweza kujenga miundombinu ya majengo vizuri sana, sisi sote tumekuwa mashahidi tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia, tunashukuru sana viongozi wa Wizara, pamoja na kazi kubwa hii iliyofanyika leo hii majengo yetu kule yanakuwa hayajaweza kutumika ipasavyo, majengo yamekamilika watoto wapo lakini hatuna walimu wakuweza kwenda kuwafundisha watoto wetu. Lakini pamoja kwamba shule shikizi zimejengwa kule na leo hapa naona umezungumza kwamba zitaendelea kwenda kujengwa, tuone namna ambavyo hizi shule shikizi tuwapeleke walimu ambao wanaweza wakakaa kwenye mazingira yale, na walimu wanaweza kukaa kwenye mazingira yale tunao sasa hivi walimu wapo wanaojitolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ajira zinapotoka hizi wao ndio tuwape kipaumbele kwa sababu tayari wameweza kumudu yale mazingira, ajira zilizopita awamu iliyopita tumeona walimu wanaojitolea wameachwa, sasa tunaomba sana awamu hii walimu wanaojitolea wale waweze kupewa kipaumbele cha kwanza hii itaweza kutusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwapongeze mnasema mnakarabati shule kongwe sisi pale Chunya tuna shule zetu kongwe za miaka mingi toka enzi hatujapata uhuru, shule ya msingi ya Chunya kati, shule ya msingi ya Mjini pale tumerithi kutoka kwa Wamisionari, zimechakaa zimeharibika zimekuwa za muda mrefu sana sasa shule shikizi zinakuwa ni nzuri kuliko zile shule ambazo zilikuwa muda mrefu na ziko katikati ya mji. Tuombe sana mnapotenga kwenye bajeti yetu zile shule kongwe muweze kuzikumbuka na hizi shule tutaweza sana kuendana sambamba ya utoaji wa elimu bora tunayoendelea nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na haya walimu tutawapeleka kule tuone namna ya kuweza kuwasadia kuwajengea nyumba kule kwenye shule shikizi kule kuna maeneo mengine sisi wanakokaa wafugaji kule hata nyumba ya kupanga mwalimu hakuna, sasa tuone namna ambavyo kupitia Wizara yenu, mkishirikiana pamoja na Wizara ya Elimu kuona namna ambavyo mtaweza kujenga nyumba za walimu ili walimu wetu hawa waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho nizungumze habari ya afya na yenyewe tunaipongeza Serikali mmefanya kazi vizuri, miundombinu ya afya imejengwa vizuri vituo vya afya vinajengwa, zahanati tunaona zinajengwa na kwa kweli kazi inayofanyika maana yake tunaenda kuwajali Watanzania kuhakikisha kwamba wana afya bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja kwamba miundombinu hii ya majengo yanajengwa lakini bado tuna changamoto ya vifaatiba; vifaatiba kwenye zahanati zetu na kwenye vituo vya afya hatuna mimi nikupe mfano tuna Kituo cha Afya cha Mtande kimekamilika toka mwaka 2019 lakini mpaka leo hakina vifaatiba pale, sasa hiko ni kimoja ambacho ni Kituo cha Afya cha Mtande, lakini tuna Kituo cha Afya cha Makongolosi kimekamilika, tuna Kituo cha Afya cha Matwiga, na sasa hivi tunaenda kukamilisha Kituo cha Afya cha Kambikatoto vyote hivi havina vifaatiba, tuombe sana Serikali inapofanya mambo haya...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana ya pili hiyo kwa mchango mzuri sasa mchangiaji wetu wa mwisho.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru na naunga mkono hoja.