Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa ambayo wote tumeyashuhudia katika hiki kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njombe tumeshuhudia madarasa mapya mazuri, karibu madarasa 38 lakini tumeona maeneo ya afya, vituo vya afya vikiendelea kujengwa kwa kasi kubwa, lakini kubwa kuliko yote katika azma ya kazi iendelee tumeshuhudia hospitali yetu kubwa ya rufaa ikipata fedha zote ili iweze kukamilika na huduma iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza na kuchukua hatua kubwa sana ambayo ilikuwa ni kilio kikubwa cha wananchi wa Njombe kutupatia barabara ya Itoni mpaka mpakani mwa Njombe na Ludewa. Tunaambiwa sasa barabara hiyo inakwenda kuanza kujengwa kwa sababu mchakato mzima wa manunuzi umekamilika na mkataba umesainiwa. Kwa hiyo, nishukuru sana kwa jambo hilo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu uwekezaji. Nashukuru sana Serikali kuendelea kufungua milango na kuboresha mazingira ya uwekezaji, tumeshuhudia kwamba miradi zaidi ya 300 yenye gharama ya karibu Dola Bilioni 8.4 tunazungumzia Shilingi Trilioni 18, hili ni jambo kubwa sana kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kwamba bado tunaomba sana Serikali iendelee kupitia sheria na sera za uwekezaji ili ziweze kuendana na hali halisi. Tunadhani kwamba baadhi ya maeneo na mitazamo ya kisera inawezekana imepitwa na wakati hasa unapoangalia miradi mikubwa ya kimkakati kama Liganga na Mchuchuma. Tuondoke kule kwenye kuangalia zaidi kodi peke yake tuende kwenye kuangalia faida kubwa, tuangalie multiplier effect. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaliongelea Liganga na Mchuchuma kwa sababu nina uhakika tutapata nafasi hapo mbele na kwa vile Waziri mhusika ameshatuambia kwenye Kamati kwamba ataongea nasi kutupa update ya suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuendelea kuchangia kwenye eneo la kilimo, tumekuwa na changamoto kubwa sana ya mbolea na imeongelewa hapa, nipenda kushukuru sana Serikali kwa suala hili kwamba sasa kilio kikubwa cha Watanzania kimepata kusikika na Serikali imeamua sasa kwamba tutakuwa na mfuko wa pembejeo. Katika bajeti hii wananchi watapunguziwa maumivu, katika hali ya bei kupanda haya ni maamuzi makubwa sana na tumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, utashi wa kisiasa katika jambo hili ulihitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njombe ni moja ya maeneo yanayokuwa kwa haraka na takwimu zinaonyesha wazi ni Mkoa ambao una mchango mkubwa sana kiuchumi na hasa katika maeneo ya vijijini. Kwenye kilimo asilimia 90 ya wananchi wa Njombe ni wakulima na mchango mkubwa wa pato la Taifa unatoka katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa zaidi katika Mkoa wa Njombe tunahitaji miundombinu wezeshi kwa kiasi kikubwa. Serikali yetu imekuwa na miradi mikubwa miwili ambayo inafadhaliwa na wafadhali ya kusaidia maeneo ya kilimo kutengeneza miundombinu wezeshi. Kwa bahati mbaya sana Njombe haikuwemo katika maeneo hayo au katika miradi hiyo, kwa sababu ambazo zimeelezewa kwamba ni Njombe Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njombe Mjini ni Jimbo lakini asilimia 70 ya Njombe Mjini ni vijiji ambapo ndipo uzalishaji mkubwa unapotoka. Napenda kuiomba sana Serikali pamoja na kwamba hatupo kwenye miradi hii mikubwa ya fursa za kiuchumi ya kufungua miundombinu wezeshi, tupate fedha za kutosha na ninawashukuru kwamba katika bajeti iliyopita tulichangiwa fedha za kutosha kiasi cha Shilingi 1.5 Bilioni kwa ajili ya maeneo ya vijijini. Ninaomba na mwaka huu tuweze kuangaliwa ili miradi ya kufungua maeneo ya vijijini na uzalishaji yanayokuza ajira kwa kiasi kikubwa, yaweze kupata fedha na barabara zetu ziweze kukabaratiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu, tunashukuru Serikali kama nilivyosema tumeona makubwa lakini napenda kusema kwamba bado tuna changamoto kubwa ya watumishi, tuna tatizo la watumishi kiasi cha Walimu kwa upande wa Shule za Msingi karibu 350 hiyo ni gape ambayo tunayo. Tunashukuru Serikali na maamuzi ya Serikali kuwaajiri Walimu 32,000 tuna matumaini makubwa sana nasi katika kipindi hiki tutaangaliwa kwa jicho la karibu kwa vile tuna uhitaji mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo lipo pia kwenye afya, tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika afya. Lakini kwenye afya napenda kusema watu wa Njombe Mjini ni watu wa kujituma ni watu wa kufanya maendeleo, katika kilimo na katika kujitolea. Katika Mji wa Njombe tayari tulishajenga Vituo vya Afya kabla hata Serikali haijatoa mkakati wa kuwa na kituo cha mkakati cha afya katika kila Kata. Tuna vituo ambavyo vinakuja vimeshakamilika na vinangoja vifaa tiba na watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuangalia kwa karibu ili maeneo haya vituo hivi ambavyo vimeshakamilika kwa asilimia 90 na vinangoja tu vipate vifaa tiba viweze kuangaliwa ili huduma ziweze kumfikia mwananchi kwa karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa umeme tunashukuru tunaendelea na mradi REA, lakini napenda kusema ni vizuri Serikali ikajitahidi tuweze kupata fedha za kutosha mradi huu ni mzuri na tunaelewa kwamba ndani ya miaka hii mitano vijiji vyote vitapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe realistic kwa speed ambayo REA wanakwenda nayo tunaanza kupata wasiwasi kwamba tutafanikiwa kukamilisha kupata hii miradi yote ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuongelea jambo moja kubwa ambalo wananchi wa Njombe tuna wasiwasi nalo, aliongea Mheshimiwa Chumi hapa kuhusiana na nguzo za umeme, uchumi wa Njombe ardhi nzima ya Mji wa Njombe au Mkoa wa Njombe asilimia 30 ni miti ambayo ndani ya miti hiyo tunatoa nguzo na ndiyo tumesaidia nchi hii kuweza kuendelea na miradi mikubwa ya REA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa habari tuliyoisikia kwamba wenzetu wa TANESCO wanataka kuanza kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi, jambo hili pamoja na kwamba la kibiashara lakini halina afya, litakwenda kuongeza umaskini kwa wananchi wengi ambao tayari wameanza kujikomboa na wanajitolea na kufanya kazi kwa bidii kujenga maisha yao, itapunguza mapato ya Halmashauri zetu kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Halmashauri ya Njombe kwa mwaka tunapata kutoka katika msitu karibu Shilingi Bilioni Mbili ambazo zinakwenda kusaidia maendeleo ya wananchi. Vile vile tuna viwanda Sita ambavyo vinashughulikia nguzo na katika muda mfupi huu viwanda vimeongezeka katika nchi ya Tanzania, kwa sababu sera zimefunguka na wawekezaji wanazidi kuja na kuna wawekezaji wa ndani hapa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya TANWOOD peke yake katika miaka miwili iliyopita imelipa zaidi ya Shilingi Bilioni Nne kama corporate tax, lakini inaajiri wafanyakazi wengi karibu 200 na inalipa mishahara ambayo ni mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujiajiri kuna Watanzania wananchi wa Njombe wengi wanajiajiri katika sekta ya misitu. Napenda sana kuiomba Serikali ifanye maamuzi ikizingatia kwamba katika Ilani yetu ya Uchaguzi tunataka kuwawezesha watanzania waweze kujitegemea wao wenyewe na sekta ya misitu inatoa hiyo fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umeisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)