Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Pia, niwatakie Ramadhan Karim Waislam wote pamoja na Wakristo wote ambao wamefunga katika mwezi huu Mtukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na wote ambao wameweza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya na hotuba yake, vilevile niendelee kuwapongeza wote waliompongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia. Kwa kweli anafanya kazi nzuri na anatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo. Naomba Watanzania wote hasa akina Mama na akina Baba tumuunge mkono ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze hoja yangu kwa kuzungumzia jambo kubwa lililopo katika Mkoa wetu wa Iringa, kuhusiana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto. Hili ni janga la Taifa. Tulipopokea taarifa katika RC tuliona karibu matokeo 439 kwenye Mkoa wetu yameripotiwa ya ukatili wa kijinsia. Kuna Wabunge wamechangia kuhusiana na huu ukatili, hili jambo ni zito mno. Mimi naomba Serikali iangalie, hili ni tatizo kubwa ambalo tunatakiwa tuungane na tunatakiwa sasa tuanze kulifanyia kazi na itengwe bajeti kuhakikisha kwamba hili janga katika Tanzania tunaanza kulitatua ili tutengeneze watoto ambao watakuwa kizazi kizuri katika nchi yetu. Hili ni tatizo kubwa ambalo tunatakiwa tuungane na tunatakiwa sasa tuanze kulifanyia kazi na itengwe bajeti kuhakikisha kwamba, hili janga katika Tanzania yetu tunaanza kulitatua ili tutengeneze Watoto ambao watakuwa kizazi kizuri katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo niliyabaini nilipofanya ziara katika Mkoa wa Iringa na Wilaya zake zote. Sasa hivi kwanza watoto wameanza kubakana wao kwa wao, wanalawitiana wao kwa wao. Tatizo kubwa ambalo lipo hasa watoto wadogo ambao wanasoma Shule za Msingi, unakuta kwamba shule zetu nyingi za msingi hazikarabatiwi, hazina vyoo, hazina uzio kwa hiyo, unakuta watoto wanashindwa kwenda chooni wanakwenda kuomba kwa majirani, wanakwenda kwenye milima kujisaidia wao kwa wao kwa hiyo, huko ndiko ambako wanabakana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshaona kwenye vyombo vya Habari sasa hivi tunaona kwamba, karibu kila Mkoa hili janga lipo. Kwa hiyo, naiomba Serikali hebu tutenge bajeti ya kutosha tuhakikishe shule zetu za msingi zinakuwa na vyoo, shule zetu za msingi zinakuwa na uzio kulinda hawa watoto wetu ambao sasa hivi hili limekuwa ni janga kubwa ambalo linahitaji maombi hata viongozi wa dini sasa hivi watusaidie pengine ni pepo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo nilikuwa nataka kulizungumza, nilitaka kuzungumza taharuki ambayo imejitokeza katika Mkoa wetu wa Iringa na Njombe. Tunaona Mheshimiwa Chumi alizungumza kuhusiana na TANESCO kuanza kuagiza nguzo kutoka nje, leo hii tumemuona Mbunge wa Njombe Mjini na yeye ameielezea hiyo taharuki na mimi kama Mbunge wa Iringa katika hiyo Mikoa miwili, niombe kwanza kabla sijazungumza kwamba Waziri mwenye dhamana hebu akae na Wabunge, Waziri mwenye dhamana ikiwezekana hata tuende tukafanye mikutano mikubwa kwenye Mikoa yetu ya Iringa na Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikuja Iringa, ulishuhudia wewe mwenyewe ulifungua nembo yetu, ile Iringa Woodland, kama ambavyo labda wenzetu Mwanza wana Rock City sisi tuna Woodland. Kwamba, Mkoa wetu wa Iringa kipato kikubwa kinatokana na mazao ya misitu. Sasa hivi Halmashauri zetu nyingi zinategemea misitu na tuna viwanda zaidi ya 18 kwenye Mikoa hii miwili, kuna ajira nyingi sana imetengenezwa kupitia nguzo. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu uangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mapato ya Halmashauri kwa sababu, hizi asilimia 10 unaona akina Mama, Vijana na Watu Wenye Ulemavu walipata mikopo mikubwa hata Mheshimiwa Ummy alivyokuja pale Iringa kutokana na mapato makubwa yaliyopatikana kutokana na mazao ya misitu ambayo ni nguzo. Kwa hiyo, tunaomba kabisa hili jambo lisipuuziwe tukahikishe kwamba, tunakaa ili kutatua hili tatizo ili Mikoa hii iendelee kutumia misitu au hizi nguzo. Kama kuna changamoto kwa nini Wizara ya Viwanda isilete ile teknolojia ikafundisha katika viwanda vyetu ili nguzo ziwe na kiwango? (Makofi)

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Kuna Taarifa wapi? Aah! Mheshimiwa Neema Mgaya, taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Ritta kwamba, kinachosikitisha zaidi nguzo hizo hizo ambazo zinatoka Njombe na Iringa na maeneo mengine ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, zinatoka tu nje ya Tanzania zinakwenda zinarudi tena kwa mlango mwingine zije kuuzwa kwa bei kubwa, wakati nguzo ni za kwetu wenyewe Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Mheshimiwa Ritta napenda kukwambia kwamba, Mheshimiwa Waziri kuna haja ya kukaa na Wabunge wa Nyanda za Juu Kusini, hususan Wabunge wa Mkoa wa Iringa na Njombe ambao tunalima mbao hizi na kutengeneza nguzo hizi ili kuweza kuisaidia Tanzania kutotumia gharama kubwa katika gharama za nguzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile…

MWENYEKITI: Ahsante kwa taarifa Mheshimiwa Neema Mgaya. Mheshimiwa Ritta Kabati unapokea taarifa?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naipokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo kweli kabisa. Isitoshe TFS inazalisha nguzo kwa kiwango kikubwa sana, sasa na yenyewe itakosa mapato kwa sababu ni taasisi pia ya Serikali, vilevile wanawake, vijana na wananchi wa Iringa wamehamasika kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kwamba wanalima miti ya kutosha katika Mkoa wetu wa Iringa. Hiki ndiyo kipato chetu na sisi kama ambavyo wengine wanasema kuhusu korosho, wengine wanazungumza kuhusu makinikia, nasi makinikia ya Mkoa wa Iringa ni misitu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nguzo zetu hazina kiwango ndiyo hivyo nimesema kwamba, Wizara ya Viwanda ilete hiyo teknolojia ili tuzalishe nguzo zenye viwango ili tuweze kupata pato kubwa katika kutumia misitu yetu. TBS wapo na wenyewe waangalie wanatumia teknolojia gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kuhusiana na hizi asilimia 10 ambazo zinatolewa katika Halmashauri zetu ambazo wanapewa Vijana asilimia Nne, akina Mama asilimia Nne, na Watu Wenye Ulemavu asilimia Mbili. Mimi naiomba Serikali waboreshe hii mikopo badala ya kupatiwa pesa unaona katika taarifa vijana wengi sana bado kuna pesa ambazo hawajazichukua, ni kwa nini Serikali isianze kutoa vifaa au mashine ili tuwe na viwanda vidogovidogo katika Halmashauri zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano labda kwa vijana. Vijana ambao wamesomea wanaweza wakapewa mashine za kufyatua tofali na wameshajifunza na hapohapo Halmashauri ile ikaweza kuchukua tofali kwa vijana wetu. Mimi naomba kwa kweli, jambo hili liangaliwe na nitaliandika kwa vizuri zaidi ili hii mikopo ya akina mama, vijana na wanawake iweze kuwasaidia vijana, iweze kurudi iwe revolving fund. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba niunge mkono hoja, niseme tuungane wote kuhakikisha tunamsaidia Mama yetu Rais, ili kazi iendelee. Ahsante. (Makofi)