Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema amenipa kibali nami niweze kusimama kuchangia kwenye Bunge hili Tukufu. Awali ya yote ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu, ambapo ametusaidia sana kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mbeya. Kwenye hospitali ile ametupatia fedha kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili ya kujenga jengo la upasuaji, lakini pia ametoa milioni 800 kwa ajili jengo la emergence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jengo lile tuna upungufu. Nilikuwa naomba sana, jengo lile halina wodi ya wanawake. Ninaomba sana kwenye bajeti hii tusiache kuweka fedha kwa ajili ya kujenga jengo la wodi ya wanawake, ni matatizo. Hii ni kwa sababu wanawake wanapata tabu sana maana wakiuguwa sehemu ya kuwalaza wanawake inakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchangia suala la TASAF. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu inatoa fedha kwa ajili ya watu wasiojiweza na wazee. Ninaishukuru na kuipongeza sana na Serikali.

Mheshimiwa Mwneyekiti, hata hivyo hatujaiangalia kwa mapana. Nimejaribu kupita kwenye kaya tofautitofauti ambazo zinasaidiwa na hizi fedha za TASAF; unapita kwenye kaya unamkuta bibi ama babu amekaa upenuni hawezi kutafuta hata kuni hawezi kuwasha moto hawezi kufanya chochote. Fedha wanaweze wakawa wamemfikishia, lakini anaweza akaa upenuni kwakwe anavizia either apite kijana ambaye akimuona ampatie fedha akamsaidie akanunue sukari. Sasa inawezekana akapita kijana ambaye ni mcha Mungu, wakati huo huo anaweza akapita kijana ambaye si mcha Mungu; hiyo pesa imeondoka anabaki tu kusikitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuishauri Serikali ninaomba sana hizi fedha TASAF ninaomba kila wilaya wafanye mpango wa kujenga hostel kwa ajili ya kutunza hawa wazee wetu. Itawasaidia sana hawa wazee. Naamini wakikaa kwenye hostel watapata huduma zote, na fedha hizi zitakwenda moja kwa moja kwenye vituo vya hosteli ili wazee wetu waweze kupata huduma stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimeuliza swali, lakini katika kuuliza lile swali nilijibiwa. Kwenye Wizara ya Ujenzi kuna sehemu ambayo sikuielewa vizuri, sehemu yenyewe ninaomba sana tuchukulie kwa uzito. Ni kuhusu hii barabara ya kutoka Igawa mpaka Tunduma hapa ninachangia, ninaomba sana hiyo barabara mtu anapotoka Dar es Salaam, anatoka Dodoma akifika Igawa kuanza safari ya kuelekea Mbeya Mjini mpaka Tunduma moyo lazima ulipuke, moyo unafanya fya’ fya’ kwa sababu anakuwa hana uhakika wa kufika salama nyumbani kwake. Yaani hakuna alama za barabarani, barabara ni finyu na ina mashimo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie hali ni mbaya sana. Mtu akitoka Mbeya Mjini anakwenda Mbalizi ni lazima aage, amuage mtu yeyote, kama mke wake hayupo ama mume wake ametoka anampigia simu, hata kama yuko Dar es Salaam amesafiri anasema natoka kidogo hapa Mbeya Mjini naenda Mbalizi. Hii ni kwa sababu ile barabara haamini kama anaweza kurudi salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo hiyo barabara ya kutoka Mbalizi kuelekea Tunduma ni finy, ajali zimekuwa nyingi sana, ndugu zetu wanakufa wengi sana kwa sababu ya barabara finyu. Ninaomba tuchukulie kwa uzito. Bunge la Bajeti ya mwaka jana nilisikitishwa sana kwamba ilitengwa bajeti ya km tano za lami; km tano kutoka wapi mpaka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante!

MHE. SUMA I. FYANDOMO: …dakika moja tafadhali. Walisema kwamba wanatafuta mkandarasi; ninaomba tuchukulie serious sana, mkandarasi atafutwe haraka ili ile barabara ianze kujengwa Mbeya tunalia jamani, Mbeya tunateseka sana na ile barabara. Madereva wanajua lakini na sisi tunaosafiri tunajua kwa sababu mioyo yetu haikai sawasawa tunapopita zile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru sana.

MWENYEKITI: Umemaliza ee!

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MWENYEKITI: Umemaliza maana nilikuwa nimekuongeza dakika moja.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Si unaongelea Mbeya Mjini!

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Ninakushukuru sana.

MWENYEKITI: Nilikuwa nimekuongeza dakika moja kwa sababu nimeona pale bosi wangu naye anapiga makofi, na mimi napenda kibarua changu.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, hata Mheshimiwa mwenyewe akifika maeneo yale lazima ashike kiti sawasawa kwamba nitafika salama, na ndiyo maana na yeye inamgusa sana ile barabara ya kutoka Igawa hadi Tunduma. Ninaomba sana; wananchi wa Mkoa wa Mbeya tuna kilio, na machozi. Naomba Serikali ichukulie kwa uzito sana, tafadhali sana sisi kule Mbeya hatuko mikono salama kwa sababu maisha ya watu wengi sana yanaathiriwa na barabara, watu wanakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali sana, naomba sana, ninaunga mkono hoja juu ya hili; lakini pia ninaomba kwa upande wa Serikali.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru sana.