Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii iliyopo mezani. Nitajielekeza zaidi katika Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo. Kwanza naunga mkono hoja ambayo imewasilishwa hapo na Mwenyekiti wangu wa Kamati na ameeleza mambo mengi, nitajadili mambo kadhaa.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa Uvuvi haramu ambapo Kamati imeeleza kwamba kuna uvuvi mkubwa haramu ambao unaendelea kwenye Mabwawa yetu kama Mtera pamoja na Maziwa na nini hasa kinafanyika huko na madhara ambayo yamekuwa yakijitokeza kutokana na huu uvuvi haramu. Kwa mfano, tatizo kubwa ambalo limeonekana, kumekuwa kuna uvuvi wa kutumia hizi taa za solar ambapo Serikali iliruhusu aina fulani ya taa, lakini wenzetu kwa sababu ya kupata faida ya haraka haraka wamekuwa wakitumia taa ambazo hazitakiwi na hivyo kupelekea kuvua mazalia ya Samaki, wale Samaki wadogo kwa mfano Sato ambao wanafuata mwanga na hivyo kuendelea kuangamiza kabisa mazalia ya Samaki hizi. Kwa kweli, jambo hilo tungeomba Serikali ichukue hatua madhubuti kwa haraka sana kuweza kudhibiti, maana vinginevyo uchumi huu unaotokana na Samaki hatutakuwa nao.

Mheshimiwa Spika, pia matumizi ya zile nyavu ambazo hazitakiwi kama kokoro ambapo kuna uwanda tu fulani ambao hawa Wavuvi huwa wanakwenda kuvua, ni rahisi sana kwa Serikali kwenda kudhibiti katika ule uwanda ambao haya makokoro huwa yanakwenda kutumika huko. Kwa kweli Serikali isipokuwa makini tutashangaa baadae kwamba uchumi huu wa samaki tutakwenda kuua kabisa na wananchi kuweza kukosa kipato.

Mheshimiwa Spika, imetokea tatizo lingine ambapo samaki wamekuwa wakifa hasa kwenye Bwawa la Mtera, lakini inaonekana kwamba kuna kilimo ambacho kinaendelea kandokando ya Mito ambayo inapeleka maji kwenye haya Mabwawa. Sasa hiki kilimo kwa mfano, kilimo cha Nyanya kuna madawa mengi yanayotumika, haya madawa yanayotumika ndiyo inakuwa sumu ambayo inaingia kwenye mabwawa na kwenda kusababisha samaki kufa. Kwa hiyo, Serikali ione ni namna gani inaweza kudhibiti watu wanaolima kandokando aidha kwenye Mabwawa yenyewe au kwenye mito inayopeleka maji kwenye mabwawa hayo ili kuendelea kutunza uchumi unaotokana na samaki.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni ujenzi wa mabwawa. Tunafahamu kwamba mabadiliko ya tabianchi yanazidi kukua na hii imesababisha sehemu nyingi sana maji kukauka, sasa ujenzi huu wa mabwawa ningeshauri kwamba Serikali kwa kushirikisha Wataalam wa Kilimo, Watalaam wa Maji na Watalaam wa Mifugo wakae kwa pamoja, wawe na design moja. Watengeneze design ambayo hii inaweza kuwa shared ili mtu wa maji anavyotengeneza atumie design hiyo, mtu wa kilimo siyo kila mmoja alete design yake, wakati mwingine tumeona changamoto kubwa kwa hawa wajenzi wa haya mabwawa hayajengwi kwa viwango lakini imekuwa ni shida ni malalamiko badala ya kuwa faida inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri tuendelee nalo, lile zoezi la kuweka hereni kwenye mifugo ni zoezi muhimu sana. Kwanza linaisaidia nchi kujua kwa uhakika wake kwamba tunayo mifugo kiasi gani katika nchi. Zoezi lile lilisimamishwa lakini nimekuja kugundua wakati mwingine ni maslahi yetu sisi wanasiasa, pengine mimi Kiswaga nina ng’ombe 200 sitaki wajulikane ninaweza kuleta sababu kwamba hizi hereni hazifai. Tuangalie kuna changamoto zipi, kama ni gharama za hizo hereni tunaweza tukajadili lakini ili tuweze kufahamu kwamba nchi ina mifugo kiasi gani ni muhimu sana hili zoezi la utambuzi wa heleni likaendelea, maana tunasema kuna mifugo kule Ngorongoro asilimia karibu 50 sio mifugo ya Watanzania lakini tukiweza kutambua kwa kutumia hizi hereni tutaweza kujua kama nchi, mifugo yetu ni ipi na ni mifugo ipi inaingia huko Misenyi ikitoka nchi ya jirani. Kwa hiyo, hilo zoezi ningependa kushauri liendelee ili kusaidia tufahamu kwanza tunamifugo lakini kudhibiti hii mifugo haramu ambayo pia inatoka nchi za jirani.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ambayo nimeona ni muhimu pia ni kuendelea kupanga matumizi bora kwenye upande wa vitalu vya mifugo. Hilo liende sambamba na kutunza maeneo ambayo yamehifadhiwa na Serikali kwa ajili ya ufugaji. Kwa mfano, maeneo yote ya NARCO mimi ninasikitika ninapoona maeneo ya NARCO yanaanza sasa kugawiwa kwa Wawekezaji waweke viwanda au pengine kilimo. Kwa sababu ukiangalia wingi wa mifugo tuliyonayo nilifikiri kwamba tunaweza tukatoa mifugo huko inako haribu mashamba ya watu, tukairudisha huku kwenye hizi NARCO zetu, kwenye hivi viwanja kama tutaweka mipango mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashauri Serikali na wenzangu mlioko kwenye Baraza la Mawaziri, msijadili kugawa maeneo ya wafugaji kwenda kwa wakulima au kwenda kujenga viwanda haitusaidii! Tuna mifugo mingi inakwenda huko holela, kwa hiyo tuirudishe huko kwenye ranchi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde thelathini malizia muda wako umekwisha.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Jambo lingine pengine kwenye kilimo imetokea changamoto kwenye ucheleweshaji wa mbolea. Kwa kuwa, tunafahamu mahitaji ya wakulima, ningependa tufanye planning mapema. Kwa mfano, sasa hivi mbolea ya kukuzia hatuna, sasa kwa vile tunajua mahitaji basi tuwe na stock in advance, tuwe na akiba ili muda unapofika wananchi wasihangaike na mbolea.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)