Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia taarifa za Kamati hizi mbili. Mimi nitajikita zaidi katika Kamati hii ya Miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nizipongeze Kamati zote hizi mbili kwa sababu mwaka huu wametuletea kwa namna gani kwenye Kamati zao yale maazimio ya Bunge yaliyopitishwa wakati kama huu yametekelezwa. Kwa hiyo, niwapongeze sana Kamati zote mbili na naamini kamati nyingine zote zitakuja na utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika, tukianza na mapendekezo ya Kamati ya Miundombinu kwenye ukurasa ule wa 25 kwenye maoni yao ya jumla wamezungumzia sana katika suala zima la ulipaji wa fidia. Ni dhahiri tumeona hapa bajeti zinapitishwa za ujenzi wa barabara mbalimbali, lakini bila kuangalia kwamba barabara hizo zinahitaji kulipiwa fidia bila kujengwa. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake utekelezaji wa mradi ule, Mheshimiwa Mbunge anatoka hapa anakwenda kueleza kwenye jimbo lake kwamba barabara fulani itajengwa katika bajeti ya mwaka huu, lakini kumbe ili barabara ile ijengwe ni lazima ilipiwe fidia.

Kwa hiyo niwapongeze sana Kamati hii ya Miundombinu kwa kuona suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi lipewe nafasi kubwa na Serikali itenge fedha ili sasa miradi yetu ambayo tutaisimamia bajeti iweze kuwekwa iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, zipo barabara kadhaa ambazo zimeathirika katika kutokulipiwa fidia, lakini fedha za ujenzi wa barabara zimewekwa. Ile barabara ya Mbagala Rangi Tatu mpaka Mwandege inahusika na tatizo hili na wananchi wamekuwa wakisota sana kuhakikisha wanalipwa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, niendelee niiombe Serikali wazingatie mapendekezo ya Kamati hii ya Miundombinu katika suala zima la ulipaji wa fidia.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Kamati wameelezea namna ambavyo mradi wa mwendokasi umeweza kufanya kazi pale katika Jiji la Dar es Salaam. Katika taarifa wamesema ukurasa wa 10, Serikali ione namna ya kutatua changamoto za mradi huu. Mradi huu wa mwendokasi pale Dar es Salaam umekuwa na changamoto kubwa, ukisoma ndani ya taarifa unaona changamoto ambazo zipo katika mradi ule.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto, baada ya miundombinu ya mradi ule kujengwa hasa katika eneo la Mbagala limeenda kuzua taharuki kubwa sana kwa wananchi. Mimi ushauri wangu pamoja na ushauri huu wa Kamati, niiombe Serikali inapoanzisha miradi hii mikubwa iwasiliane na mamlaka zote mbili zinazohusiana na ujenzi wa barabara. Kwa mfano TANROADS wanapojenga barabara kubwa, wakijenga na mifereji maeneo ya kuelekezea maji ya katika mifereji wanawategemea TARURA waweze kuyafikisha katika maeneo maji yanapotaka kufika.

Mheshimiwa Spika, lakini utakuta TANROADS wanafanya kivingine na TARURA nao wanafanaya kivingine, mwisho kinachotokea sasa TANROADS wanafanya kazi nzuri ya kujenga barabara, lakini mwisho wa siku sasa uwezo wa TARURA wa kuweza kuyachukua yale maji ambayo yamekusanywa na TANROADS unakuwa ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe sana Serikali wakati wa kujenga barabara hizi kwenye majiji yetu basi wawasiliane na hizi mamlaka mbili zinazohusiana na ujenzi wa barabara. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, la mwisho, naona kengele inagonga na muda unaisha niiombe sasa Serikali maazimio yote yaliyotelewa katika Kamati hii ni maazimio ya msingi sana. Niombe iende ikayatekeleze ili sasa tija kwa wananchi iweze kuwa na umuhimu mkubwa sana, ahsante sana. (Makofi)