Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia taarifa ya Kamati mbili; Kamati ya Miundombinu na Kamati ya Maji na Kilimo.

Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza katika Kamati ya Miundombinu na nimeipitia taarifa hii lakini nimebaini kwamba kuna eneo ambalo halijaguswa vizuri na hii inahusiana na Taasisi ya TEMESA. TEMESA ni taasisi ya Serikali inayosimamia masuala ya mechanical, electrical pamoja na masuala ya vivuko. Kwa kweli utendaji wa Taasisi hii ya TEMESA umekuwa siyo wa kuridhisha na huko tunapotoka kwenye Halmashauri zetu, magari yanayopelekwa TEMESA badala ya kwenda na kupona yanarudi yakiwa mabovu, gharama zinakuwa ni kubwa sana, TEMESA imekuwa ni dalali wa taasisi binafsi na gereji binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa leo nataka nijielekeze katika masuala ya menejimenti ya vivuko. Mimi ni Mbunge wa Jimbo ambalo ni lazima uvuke maji kwenda kufika katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Katika hizi siku za karibuni kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa wananchi wa Kigamboni kuhusiana na upatikanaji wa vivuko salama vyenye uhakika kwenda katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Hivi karibuni tumepata kivuko ambacho kilikwenda kukarabatiwa cha MV-Kazi kimrudi lakini nacho kimerudi na changamoto kubwa sana pamoja na gharama ya bilioni 4.4 kukitengeneza kivuko kile.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunategemea kupeleka panton kubwa MV-Magogoni Kenya, mimi kama Mtanzania nasikitika sana, tunao wazalendo ambao wanaweza wakavitengeneza hivi vivuko lakini kwa sababu ya taratibu tu za manunuzi tutakitoa kivuko chetu tutakipeleka Mombasa tutapeleka fedha za kigeni na tunakwenda kuua ajira, wakati huo huo tunasema tunataka tutengeneze ajira ndani ya nchi yetu. Hili mimi nilitamani sana Kamati ya Miundombinu ifanye mapitio ya mchakato wa manunuzi ya upatikanaji wa Mkandarasi wa utengenezaji wa MV-Magogoni.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kampuni ya wazalendo ambayo imetengeneza boti zetu, inatengeneza meli zetu, tunasema kwamba haina uwezo wa kukarabati boti, hilo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nimalizie kutoa ushauri na nilitamani sasa hili nalo tuliongeze katika maazimio yetu kwamba TEMESA iangaliwe upya, kimfumo na kiutendaji. Nilitaka kushauri na kama Bunge lako nalo litatukubalia hususan katika upande wa vivuko. Pale kwangu Kigamboni wanavuka watu takriban watu 60,000 mpaka 80,000 kwa siku, yanavuka magari zaidi ya 2,000 lakini ni wazi kabisa usimamizi na uendeshaji wa vivuko vile umekuwa ni changamoto kubwa sana na iko siku tutapata maafa makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, imekuwa karibia kila wiki panton zinazimika baharini zinavutwa, mageti yanashindwa kufunguka yaani ni tafrani, haipiti wiki bila kupata malalamiko makubwa kuhusiana na vivuko vile. Sasa tusisubiri mpaka maafa yanatokea. Mimi nashauri kwa kuwa TEMESA wameshindwa kusimamia masuala haya ya vivuko ni vema vivuko hivi sasa vikapewa watu binafsi waweze kuvisimamia, kuviendesha na Serikali iweze kupata gawio kutokana na vivuko hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwamba katika moja ya Azimio la Bunge lako basi suala la TEMESA katika usimamizi wa vivuko liweze kuangaliwa na huduma hizo ziweze kupewa watu binafsi. Ninakushukuru sana. (Makofi)