Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye hii hoja ya Kamati ya Viwanda, Biashara, Uwekezaji pamoja na Mazingira. Kwa maksudi ya kuokoa muda nitachangia kwenye suala la Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze kwa malengo ya kusaidia nchi na ninaomba nieleweke vilevile kwamba mchango wangu unalenga kuisaidia nchi tuipendayo ya Tanzania na kumsaidia Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Hivyo ndivyo ninatakiwa nieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la mradi wa Liganga na Mchuchuma ulianza mapema sana mwaka 2007 tena kwa Waraka Na. 14/2007 wa Baraza la Mawaziri. Katika kutafuta watu watakaofanya hii kazi Kampuni 48 zilijitokeza. Wakati naendelea nina-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kwa hiyo naongea mambo ambayo nayafahamu vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni 48 zilijitokeza kwa ajili ya kuomba kufanya hii kazi, ni kampuni moja tu peke yake ambayo ilikuwa tayari kuchukua project ya Liganga na Mchuchuma, kampuni zingine zote 47 zilitaka zifanye makaa ya mawe peke yake. Hii kampuni peke yake ambayo ilijitokeza yenyewe ifanye miradi yote miwili Liganga na Mchuchuma ambayo ilikuwa ni Sichuan Hongda ya China.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kampuni baada ya kutokea, kampuni hii ikaanza kazi na tayari Serikali ikaamua kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara itengeneze timu maalum yenye uwezo wa kusimamia hili jambo. Timu iliyotengenezwa High Technical Committee ilikuwa ina-include watu wafuatao: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaisoma hii High Technical Committee kukuonesha kwamba waliokuwa wanashughulika na jambo hili siyo mazuzu, ni watu wenye uelewa, ni watu wenye elimu, ni watu wenye heshima katika Taifa letu la Tanzania. Ilitengenezwa committee hii ambayo wa kwanza alikuwa ni Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini ndiye alikuwa Mwenyekiti; pili, alikuwa Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini; Tatu, alikuwa Mkurugenzi wa Viwanda kutoka Wizara ya Viwanda, mwingine alikuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), mwingine alikuwa Kamishna wa Sera kutoka Wizara ya Fedha, mwingine alikuwa Mchumi Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo na Miundombinu, Mwingine alikuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Ukuaji kutoka Wizara ya Mipango na Uwezeshaji, mwingine alikuwa Afisa Mipango Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwingine alikuwa Mkurugenzi wa Mikataba ya Kimataifa kutoka Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, mwingine alikuwa Mkurugenzi wa Export Processing Zone Authority na mwingine alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Investment Center na mwingine alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO na mwingine alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mwingine alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndiyo waliochaguliwa kuwa technical team ya kuongoza hili suala la Liganga na Mchuchuma, hawa siyo watu wadogo. Nataka kuondoa notion kwamba eti Serikali iliingia kwenye mikataba bila kujua no! Hawa watu ni wataalam, waliochaguliwa kwenye technical team ili kwamba waongoze suala la Liganga na Mchuchuma kufikia mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maksudi ya kuisaidia nchi yetu na vizazi vijavyo wakakubaliana huyu Sichuan Hongda - Mchina kwa ubia na Shirika la NDC la Serikali walikubaliana mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikubaliana kwenye mkataba wao wa awali kwamba Serikali ya Tanzania kupitia NDC ichukue asilimia 20 na huyu bwana achukue asilimia 80. Sasa baadae kukawa na ubishani kidogo kwenye hiyo percent, kwamba hapana ni kidogo sana baadae wakakubaliana kwamba iwekwe annex kwenye huo mkataba kwamba Tanzania baadae ina uwezo wa kununua share ikafikia asilimia 50, ili kwamba sisi kama Taifa tuwe na hamsini na huyu mwekezaji awe na hamsini, that was very good.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikufungue macho, mradi huu una jumla ya thamani ya dola bilioni tatu. Kama nchi ya Tanzania ingeweza kuchukua share ya asilimia 20 maana yake tungepata dola milioni 600 kila mwaka. Lakini mradi huu unadumu kwa muda gani, mradi huu kwa mujibu wa deposit unadumu kwa muda wa miaka 100. Kwa hiyo, Taifa la Tanzania lingepata dola milioni 600 mara miaka 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa tumefanikia ku- score kwamba tutanunua share zingine ili Taifa letu liwe linapata asilimia 50. Kama Taifa letu lingekuwa linapata asilimia 50, kila mwaka tungekuwa na uwezo wa kupata dollar 1.5 billion kila mwaka mara miaka 100! Narudia tena mara miaka 100 - this is documented. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni makosa ya hali ya juu sana kuona bado mradi huu haujaanza mpaka leo, wenye uwezo wa kuipa Serikali fedha nyingi kiasi hiki kwa mambo ambyo nitayeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotokea ni kwamba huyu mwekezaji alikuwa tayari na Serikali kupitia NDC tukasaini performance contract, tukakubaliana naye tayari kwa ajili ya kuanza. Baada ya kusaini performance contract, mwekezaji akawa na wasiwasi baadae akasema bwana mimi naomba mnipe incentive zaidi kwa sababu ya uwekezaji wangu mnipe incentive zaidi ili kusudi niweze kupeleka huu mradi.
Kwa hiyo, Serikali ikasaini tena performance contact ya pili na huyu mwekezaji kukubaliana na hizo incentives ambazo huyu mwekezaji alikuwa ameomba. Performance contact ya pili ilisainiwa 30 Juni, 2014 tukasaini sisi wenyewe kwamba tumekubaliana naye ili apate incentives zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo inabidi sasa hizi incentive alizoomba mara ya pili ziwe gazetted. Haziwezi kufanya kazi bila ya kuwa gazetted na Wizara ya Fedha. Hazijawa gazetted mpaka leo kwa nini? Hazijawa gazetted mpka leo, matokeo yake tunaanza kusema kwamba huyu mwekezaji ni tapeli, huyu mwekezaji hajulikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kukupa ushahidi, Kamati hii ilisafiri kwenda mpaka China ikamtembelea huyu mwekjezaji, ikafika kwenye ofisi zake, ikafanya due diligences, ikapaona alipo. Inawezekanaje tunaweza kusema leo tuache mradi huu wenye uwezo wa kutupatia 1.2 billion dollars mara miaka 100.
MHE. CHRISTOPHER OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKLITI: Mheshimiwa Ole-Sendeka, taarifa.
T A A R I F A
MHE. CHRISTOPHER OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana Baba Askofu. Ninaufahamu mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kama ninavyo kifahamu kiganja cha mkono wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mradi ambao Serikali ikitekeleza ni mradi wa kifisadi ni mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kwa hali mkataba ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo ni wa dola bilioni tatu na ilitakiwa ikopwe dola bilioni 2.4 kwa kugawana kati ya Kampuni ya Tanzania na Kampuni ya China halafu Wachina waje na bilioni 600 tu. Kwa kuleta kwao bilioni 600 iwastahili wao kupata asilimia 80 ya mapato wakati deposit ni yetu lakini ile bilioni 2.4 tunalipa sawa kwa sawa. Kama tunalipa sawa kwa sawa kwa nini mapato hatugawani sawa? Kwa nini mimi Tanzania nipewe 20 kwa chuma changu chote cha Liganga halafu kampuni ya Wachina ichukue asilimia 80? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nikwambie huu ni mpango wa kifisadi mchana kweupe. Nataka nikwambie kama kuna kampuni ilikuwa inapiga deal ya kuiumiza nchi hii ni kampuni hiyo ya Chuan Hong Da. Nataka nikwambie hoja ziililetwa hapa Bungeni na waliokwenda China watuambie nani aliwapeleka na ripoti ya China ije hapa. Hawa ni mafisadi mchana, mimi nitaweka mezani ushahidi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Josephat Gwajima unaipokea hiyo taarifa?
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana kaka yangu nimwambie waziwazi anaongea bila kujua anachoongea. Mimi hapa nina document ninaweza ku- supply document kwenye Bunge lako moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisikilize kwanza sisi wenyewe kama Serikali tumesaini arbitration document…
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Nyongo taarifa.
T A A R I F A
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu kaka yangu Mchungaji kwamba mradi huu bahati nzuri mimi nimekwisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara na kwa bahati nimekwisha kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, deposit iliyopo Liganga na Mchuchuma makaa ya mawe kuna tani zaidi ya milioni 400 na mradi mzima kwa maana ya chuma pamoja na makaa una cost dola za Kimarekani bilioni tatu. Mwekezaji amekuja na milioni 600 tu; bilioni 2.4 tumpe guarantee ya Serikali tukope naye, hilo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na incentives alizokuwa anaziomba ambazo Mheshimiwa Mchungaji anazisema, mradi ule ulikuwa uzalishe megawati 300 za umeme, megawati 250 alitaka Kumuuzia TANESCO na katika kumuuzia TANESCO alitaka aweke mtambo wa kuzalisha umeme na mtambo ule alitaka tumlipe capacity charge, at the same time amuuzie TANESCO umeme kwa senti dola 11. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo tungesema tuukubali ulikuwa unakwenda kutafuna nchi yetu kwa sababu deposit ni yetu, chuma ni yetu, tulikuwa na uwezo wa kumpa hata STAMICO akachimba akaweza kuuza ule mkaa na akazalisjha umeme na aka-supply kwenye chuma ambapo ni kilometa 80 kutoka kwenye makaa ya mawe kwenda kwenye chuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iutazame tena mradi huu upya, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Josephat Gwajima unaipokea hiyo taarifa?
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa yake, labda nimpe shule zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ulikuwa ndani yake na miradi kama mitano; mradi wa kwanza ni kuchimba chuma na kutengeneza chuma; mradi wa pili, kuchimba makaa ya mawe; mradi wa tatu, kutengeneza umeme megawati 600; megawati 300 na megawati 300 ziingie katika Gridi ya Taifa; mradi unaofuata wa nne, kutengeneza barabara ya lami kutoka Mchuchuma kwenda Liganga. Hiyo ndiyo miradi iliyokuwepo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza ninaomba kama anafikiri mimi ninabahatisha mikataba iletwe hapa Bungeni uone maajabu yaliyopo. Kwanza tayari tuko kwenye matatizo na kama angeweza kunisikiliza ushauri wangu mpaka mwisho ingeokoa taifa hili kupelekwa arbitration. Tutapigwa halafu tutaumia wakati kuna njia ya kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ufanye hivi, huyu mtu ambaye sisi tulimuona ni tapeli, ilikuwaje tukasaini mikataba hii? Ilikuwaje tukaenda mpaka China kutembelea kampuni yake na tuka-approve? Imekuwaje viongozi hawa niliowataja wote wakuu wa mashirika ya umma wakasaini na mpaka leo mkataba uko valid, ilikuwaje? What happened?
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima kuna taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
T A A R I F A
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri anaoutoa Mheshimiwa Gwajima, lakini nikitambua taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Ole-Sendeka, taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Nyongo, naomba kumpa mzungumzaji taarifa nikitambua yeye ni Mjumbe wa Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwamba tuliyoyawasilisha kwenye Kamati ndiyo maelezo mahususi ya Serikali na kupitia mchanganyiko huu unaoonekana mbele ya Bunge lako ndio Serikali yetu kupitia viongozi wetu wakuu wote, Rais wa Awamu ya Nne, Rais wa Awamu ya Tano, Rais wa Awamu ya Sita wakiwa na lengo la kutekeleza mradi huu, lakini kwa maslahi mapana ya Taifa ndipo walipoelekeza mikataba hii iweze kufuatiliwa kwa sababu kama anavyosema Mheshimiwa Gwajima addendum iliyosainiwa, GN haiwezi kutolewa kwa sababu iko kinyume na sheria za nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yangu naomba pia aweze kuipata Mheshimiwa Gwajima ndio maana wale uliowasoma waliokuwa kwenye timu mpaka sasa wako kwenye vyombo vya uchunguzi wanafanya kazi kujiridhisha ni nini kilichotokea mpaka kufikia hapo walipofikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa hii Mheshimiwa Gwajima. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Gwajima kwa dakika moja naomba uhitimishe hoja yako kama unapokea taarifa au hupokei.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubali kwamba maelezo aliyotoa Mheshimiwa Waziri, ni wajibu wake wa Kiserikali kufanya hivyo, lakini mimi msimamo wangu uko pale pale na natoa angalizo namna utakavyofanya kwenye namna ya kusitisha mkataba na huyu mwekezaji, iangaliwe kwa umakini sana kwamba Serikali isije ikaumizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi kwa makusudi ya kulifanya Bunge lako na kamati yetu iwe sawa sawa niko tayari kuwasilisha document zinazoonesha kwamba hapa tulipo si pazuri sana. Nakushuru sana. (Makofi)