Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na dunia kwa kutupa uhai kuuona mwaka 2023. Kabla sijaendelea na mchango wangu napenda kuunga mkono hoja za Kamati yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, hoja zote za msingi ambazo zilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati, naunga mkono kwa asilimia mia moja, naunga mkono pia hoja za Kamati ya Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia changamoto ambazo zinawakabili wananchi lakini ambazo ziko nchini kwetu jinsi wanyama waharibifu ambavyo wanaweza wakaathiri wananchi. Zipo changamoto ambazo zinaikabili Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali. Wizara hii ina upungufu wa hifadhi 1,680 ambao wanatakiwa ili kuepusha wananchi wasije wakadhurika na wanyama wakali, lakini bado wanahitaji vitendea kazi kama pikipiki, helikopta kwa ajili ya movements za kule kwenye hifadhi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya matatizo, matokeo yake imekuwa mara nyingi wananchi wameweza kuumizwa na hao wanyama wanaotoka kwenye hifadhi. Pia tumekosa ufanisi zaidi wa kuangalia hizi hifadhi tunazidhibiti vipi, ningependa kujua kwamba kwanza, je, lile suala la buffer zones la mita mia tano kutoka kwenye hifadhi bado lipo na linazingatiwa kwenye hii Wizara ya Maliasili na Utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nipende tu kuzungumzia kwamba mwananchi anapopata matatizo kwa mfano ameumizwa na hawa wanyama wakali, fidia zake haziridhishi kama jinsi Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu alivyozungumza wakati anawasilisha hapo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea mwananchi ameumizwa na hawa wanyama kwa bahati mbaya kwa mfano akiwa ameuawa, mwananchi huyu analipwa kifuta machozi cha shilingi 1,000, akiwa amepata ulemavu analipwa kifuta machozi cha shilingi 500, akiwa ameumizwa kidogo anapata kifuta machozi cha shilingi 500,000.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ruhoro.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba kifuta machozi anachokisema inapotekea mwananchi ameuliwa na mnyama mkali siyo shilingi 1,000 ni shilingi 1,000,000. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taska.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nililigundua hilo kosa nikawa nimesahihisha labda msikilizaji hakusikia. Nilisema kwamba inapotokea mwananchi amefariki kifuta machozi anapata Sh.1,000,000, anapokuwa amepata ulemavu wa kudumu anapata Sh.500,000 na anapopata majeraha madogo madogo anapata Sh.200,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ukienda kwenye matangazo ya hifadhi zetu unakuta kuna hifadhi imebandikwa pale kwamba ukimgonga nyati unalipa Dola 1,900, ukimgonga twiga kwa bahati mbaya unalipa Dola 15,000, ukigonga tembo pia unalipa Dola 15,000 na wanyama wengine wameorodheshwa hapo, utakuta wamebandika hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati alivyowasilisha asubuhi, Kanuni za mwaka 2011 za Malipo ya Kifuta Jasho zinatakiwa zibadilishwe kwa sababu haziendani kabisa na hali halisi ya sasa hivi. Sisemi kwamba mwananchi akifariki alipwe labda dola 15,000, nafahamu uhai hata kama mtu kama angelipwa dola 100,000, siyo sawa na uhai lakini angalau basi kile kifuta jasho kiweze hata kufanikisha mazishi yake lakini pia kiweze kusaidia hata familia yake iliyobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifuta jasho cha shilingi 1,000,000 kwa mtu ambaye amepoteza uhai ni kifuta jasho kidogo sana na ukilinganishwa na compensation ambayo mtu analipa akiwa amegonga twiga, tembo au nyati, hivyo basi niombe haya yarekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kingine ambacho ningependa kukizungumzia ni suala la malipo ya fidia kwa hao hao wanyama. Kifuta jasho cha mtu mwenye shamba lake likiwa ndani ya mita mia tano halipwi kitu, lakini shamba likiwa umbali wa mita 500 mpaka kilomita moja analipwa shilingi 25,000, lakini analipwa kwa hekari tano tu. Kwa hiyo hapa hata kama mtu shamba lake limeliwa la ekari 100, atalipwa ekari tano tu kadiri ya sheria inavyosema. Niombe sheria hizi zibadilishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie hapa ni suala la utalii. Utalii unaenda vizuri, tunampongeza Mheshimiwa Waziri wa Utalii lakini pia tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour, wageni wengi wamekuja nchini lakini tuna matatizo makubwa ya mahoteli, mahali pa kulala wageni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo Serikali ilikuwa inamiliki hoteli 23. Hoteli hizi Serikali ilizibinafsisha, lakini katika ubinafsishaji kuna watu ambao walibinafsishiwa hizo hoteli ambazo hazifanyi kazi mpaka leo na wengine walizozichukua zinafanya kazi kwa kiwango cha chini ambacho siyo standard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna uhitaji wa hoteli nafikiri hoteli hizo kama zisingeuzwa zingeweza kutusaidia. Naunga mkono hoja ya Kamati ya kusema kwamba hoteli zote ambazo hazifanyi kazi, zimefanya vibaya, zichukuliwe na Serikali ziweze kutafutiwa wawekezaji wapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Hoteli ya Embassy, tangu ilivyobinafsishwa ina takribani miaka 14 haijawahi kufanya kazi na kule ndani kila kitu kimeharibika, lakini pia zipo Hoteli za Kunduchi Beach na Mikumi Lodge hazifanyi kazi na mwekezaji aliyepewa hoteli hizo ni mwekezaji mmoja, ambaye amepewa Hoteli za Embassy, Kunduchi Beach pamoja na Mikumi ameshindwa kuzikarabati hizi hoteli kwa takribani miaka 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi mtu kama huyu ni mtu ambaye tayari automatically amevunja ule mkataba wa ubinafsishaji. Sioni sababu ya Serikali kuanza kumbembeleza kumwandikia barua ya kuja kwenye meza ya maridhiano, kwa sababu automatically huyo mtu ameshavunja mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wageni wengi wanakuja. Niseme tu, Sera ya Ubinafsishaji wa Hoteli kwa wakati ule labda ilikuwa nzuri, lakini haikuleta tija kwa Taifa letu. Hivyo basi, naomba kama Mwenyeketi wa Kamati alivyosema, tunataka action, hatutaki majadiliano, tunataka hoteli hizo zirudi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu Wizara ya Ardhi. Waliozungumza mbele yangu nawaunga mkono kwa hoja walizozizungumza, lakini napenda kuzungumzia suala la fidia. Kuna hizi kampuni ambazo zinapita zikipima. Wanapomkuta mtu ana shamba lake, kwa mfano shamba la ekari 100, hana hela ya kupima, wana tabia ya kusema kwamba tutakupimia bure halafu utatupa sehemu ya viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Ardhi ilete utaratibu, ijulikane kabisa kampuni kama inapima bure italipwa viwanja vingapi? Kuliko kama ilivyo sasa hivi, makampuni yanakwenda kule, yanafanya negotiation, matokeo yake wanawadhulumu wananchi. Unakuta mwananchi ana shamba lake la ekari 100 anapimiwa viwanja, anaonekana kwamba yule aliyepima kachukua viwanja 30 akagawanya sawa kwa sawa na mtu mwenye ardhi yake. Hiyo siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na kanuni ambayo itatoa mwongozo kwamba iwapo mwananchi ana shamba lake, anataka kupimiwa, basi kanuni inasema kwamba labda ni asilimia 100 ya viwanja; kama amepima viwanja 10, labda hiyo kampuni ichukue kiwanja kimoja. Siyo kampuni ipime viwanja 10 ichukue viwanja saba au sita, inagawana sawa na mwenye mali, naona siyo sahihi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)