Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hoja tulizokuwanazo mbele yetu. Nianze kwa kuunga mkono hoja zote mbili za Kamati ya Ardhi na Kamati ya Viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu, mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha kwa vitendo kwa kufanya The Royal Tour ambayo imeenda kuimarisha utalii katika nchi yetu. Takwimu zinaonesha kwamba watalii wameongezeka katika nchi yetu ambapo mwaka 2020/2021 tulikuwa na watalii 922,692 lakini mwaka 2022 tumekuwa na watalii 1,454,000. Hii ni takribani ongezeko la asilimia 57.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa ndani uliongezeka kwa asilimia 199.5 pale ambapo mwaka 2020/2021 tulikuwa na watalii 788,000 lakini mwaka 2022 tulikuwa na watalii wa ndani 2,363,000. Hii inatuambia nini sasa? Hii inatuambia kwamba, Serikali inapaswa kujipanga kuendelea kuwapokea hao wageni kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaonesha njia kwa kufanya The Royal Tour ili kuongeza utalii katika nchi yetu. Ndiyo maana tumeona watalii wameongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inapaswa kuendeleza hizi jitihada kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo itasababisha utalii uzidi kuendelea mbele. Iko mikakati ambayo Serikali inaweza kuendelea kuifanya ikiwemo kuimarisha na kuboresha mazingira ya watalii. Ukiangalia taarifa ya CAG inatuambia kwamba yapo maeneo makubwa ambayo Serikali inaweza kuyafanyia kazi, ikiwemo kuboresha hoteli na lodge katika nchi yetu, kwa sababu imeonekana kuna changamoto ya watalii kupata malazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, ni kuongeza vivutio vya utalii. Kwa hiyo, Serikali inapaswa iyafanyie kazi hayo mambo mawili ili kuhakikisha kwamba mapato na utalii unakua katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye hoteli na lodge zilizokuwepo ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Serikali. Ikumbukwe kwamba mwaka 1992 Serikali ilibinafsisha hizi hoteli kwa Sheria ya Mashirika ya Umma ya Mwaka 1969. Hapo Serikali ilikuwa na hoteli na lodge 23. Hizi hoteli 23, 17 zilikuwa zinasimamiwa na Shirika la Taifa na hoteli 6 zilikuwa zinasimamiwa na Shirika la Reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa na lengo zuri kwamba sasa wawekezaji waweze kuja nchini kwetu wawekeze lakini tushirikiane katika kumiliki na uendelezaji. Hili halikutokea kwa sababu hapo mwanzo wakati hoteli hizi zinaandaliwa zilikuwa zinaendeshwa kwa hasara, na pia zilikuwa na madeni mengi. Lengo lilikuwa zuri lakini tija hiyo haijaweza kufikiwa kwa sababu mwaka 2022 mwezi wa Tano Serikali iliunda Tume Maalum ambayo ilikwenda kuzifanyia tathmini hizi hoteli. Ilionekana katika hizo hoteli 23, ni hoteli 10 ambazo zinafanya kazi. Katika hizo hoteli 10 zinazofanya kazi, hoteli nne ndiyo zimefanyiwa ukarabati ambao ni sahihi, lakini hoteli sita zimefanyiwa ukarabati ambao hauridhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli sita hazifanyi kazi, kwa hiyo, hata taarifa zake za kujua uwekezaji wake ukoje, hazikuweza kupatikana. Hoteli nyingine sita hazijaweza kufanya kazi kabisa. Hii ikiwemo na Hoteli ya Embassy ambayo ipo Mjini kabisa Dar es Salaam. Hoteli ya Musoma, imeungua, ni pori, ni kichaka cha kulala popo. Hoteli ya Mbeya haifanyi kazi na nyingine nyingi katika hizi sita ambazo hazijafanya kazi na ni magofu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hoteli nyingine ya Moshi Hotel ambapo hii mwekezaji alikopa na baada ya kushindwa kulipa, TID imeuza hoteli. Kwa hali tuliyokuwanayo nchini ya hili ongezeko la watalii linalojitokeza, lazima Serikali ije na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba hizi hoteli sasa zinaweza kufanya kazi. Ifanyaje sasa? Maana kwa hali ya kawaida, hata sisi wananchi tukinunua viwanja kama hujakiendeleza kwa muda Fulani, unapaswa kunyang’anywa, lakini Sheria yetu ya Mashirika ya Umma haina ukomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ianze mchakato wa kuangalia sheria. Sheria ya Uwekezaji iwe na ukomo ili pale ambapo mtu ameshindwa kuendeleza, basi sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hizi hoteli ambazo hazijafanyiwa ukarabati tangu mwaka 1992 mpaka leo hazijafanyiwa ukarabati, ukarabati sijui ni wa miaka mingapi, Serikali irejee upya mikataba kuhakikisha kwamba hizi hoteli zinarudi, zifanyiwe ukarabati, tutafute wawekezaji wenye uwezo. Kwa sababu wawekezaji ambao wamechukua hizo hoteli wamekaa nazo miaka yote hii ni dhahiri kwamba hawataweza kutatua hii shida ya malazi tuliyokuwanayo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kipengele kingine ambacho naomba Serikali ikiangalie pia kwa jicho la pili. Tume yetu imeshauri kwamba hizi hoteli zirudishwe kwa Shirika la Reli ambalo lililokuwa linamiliki hapo awali. Kwa mfano, Hoteli ya Musoma na Hoteli ya Mbeya wamekubaliana na sasa zimerudishwa Serikalini kwenye shirika hili. Hata hivyo Shirika letu la Reli bado lina majukumu makubwa ya kuboresha miundombinu yetu ya reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba kwa kuwa Wizara ya Maliasili ni Wizara ambayo kwa sasa ina uhitaji mkubwa wa hizi hoteli; kwa hiyo, nina hakika wakipewa jukumu hili kuzisimamia wao, basi watazipa kipaumbele cha kuzitengeneza ili watalii wetu waweze kupata sehemu ya kulala. Kwa hiyo, Serikali iwarudishie Wizara ya Maliasili ili waweze kutafuta wawekezaji wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo eneo jingine ambalo Wizara yetu inaweza kuboresha zaidi ambalo nimesema ni kuongeza vivutio. Tunazo hifadhi zetu ambazo zinafanya matumizi machache. Kwa mfano, nitatoa mfano wa Hifadhi yangu ya Muyoozi ambayo ni hifadhi ya uwindaji. Hifadhi hii ina wanyama wote wakubwa watano lakini pia ina wanyama ambao wanaenda kupotea kama vile statunga ambayo ni jamii ya swala lakini na ndege shubil ambao hawapo maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Wizara ichukue umahususi wake kabisa kuanzisha utalii mwingine ikiwemo utalii wa picha kwenye hifadhi ile ili kuongeza kipato. Kuna utalii wa kuvua ambao unaweza ukafanyika ili kuongeza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti ya utalii wa uwindaji na utalii huu wa picha na wa uvuvi, huu unaruhusu jamii kupata faida ya moja kwa moja. Utalii wa uwindaji tuna faidika na CSR, sawa tunashukuru lakini hatupati faida ya moja kwa moja kwa sababu muwekezaji anakuja moja kwa moja hifadhini anawinda anaondoka. Tukipata utalii huu wa picha basi tunaamini watalii watafika katika jimbo letu katika ile Kata ya Busagara, Kijiji cha Kifura, wananchi pale watafaidika kwa sababu watakunywa maji, atanunua hiki basi watakiongezea kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wa maeneo ya pale basi watawasaidia hawa watalii kuhakikisha kwamba wanaweza kufika kule mbugani kwa hiyo tutaweza kupata mapato zaidi. Pia upo utalii wa fukwe ambao bado hatujafanya vizuri. Tukifanya vizuri kwenye utalii wa fukwe basi tutaongeza vivutio na ni dhahiri kwamba watalii wanapenda utalii wa fukwe ndiyo maana tunaona watalii wanapenda kwenda Zanzibar kwenye utalii wa fukwe kuliko huku kwetu. Basi tufanye, Wizara tunaiomba Serikali ijielekeze kwenye utalii wa fukwe ili tuweze kuongeza vivutio ambavyo vitatusaidia kuongeza pia mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna utalii wa malikale, malikale ziko maeneo mengi sana ambapo bado hazijafanyiwa kazi vizuri. Zikifanyiwa kazi vizuri hizi malikale basi zitaisaidia Serikali kuongeza mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema naishukuru sana Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kufanya kazi vizuri katika Wizara yetu ya Maliasili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara nzima kwa jinsi ambavyo wanaendelea kufanya kazi vizuri kuhakikisha kwamba Serikali inaendelea kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee tunaendelea kuomba Serikali iongezewe bajeti. Tumesema TANAPA ilikuwa na hifadhi 16, lakini sasa imeongezewa hifadhi sita nyingine lakini bajeti yake ni ile ile. Ni ukweli usiopingika kwamba huduma haziwezi kuwa vile vile na kama huduma siyo nzuri basi tunawapoteza watalii wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)