Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja zilizowasilishwa mezani. Kwanza kabisa naomba niliambie Bunge lako mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye sekta ya utalii, ili tuweze kuwa na utalii imara kwenye nchi yetu tunahitaji kujiandaa na kuwa na huduma bora kwa wageni ambao tunahitaji kuwapokea, ikiwemo barabara, malazi, hoteli ziwe nzuri, safi, wahudumu, watu wanaowapokea bandarini na wengineo wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama nazungumza hapa kwa masikitiko makubwa. Serikali naona kwenye jambo hili la utalii hawajaamua kumsaidia Rais. Kwa sababu haiwezekani Hotel na Lodge 23 zikabinafsishwa kwa wawekezaji halafu kuwe kuna hotel 10 tu ndiyo ambazo zinafanya kazi ndani ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi hotel zingine zinafanya kazi gani? zimeendelea kubaki kuwa magofu ukiziulizia unaambiwa zinafanyiwa repair. Mwaka jana tulipokea wageni Milioni 1.4 katika Taifa letu na hii imetokana na juhudi za Mheshimiwa Rais, halali maskini mama wa watu, anahangaika kuitangaza Tanzania lakini leo wageni wanakuja tutashindwa mahali pa kuwalaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna hoteli 10 tu ndiyo zinafanya kazi, hizi hoteli zingine zimekuwa magofu sisi tunategemea hilo Pato la Taifa tunalipata wapi? Ukiangalia kwenye hizi hoteli ambazo zimebaki maana yake tumepoteza ajira za watoto wetu, ni asilimia ngapi ambayo imepotea. Hizi hoteli zingekuwepo maana yake tungetengeneza ajira lakini na pato lingeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia hiyo taarifa ya hoteli wanakuambia kwa kipindi cha miaka mitano wamekusanya mapato ya Bilioni 60. Lakini ukisoma mchanguo wa Bilioni 60, Bilioni 16 zinaenda kwenye PAYE ambayo yoyote akiwekeza lazima alipe wafanyakazi na lazima hiyo kodi alipe. Faida inayopatikana hapa kwa miaka mitano hamna kitu! Sasa kama imeshindikana kwa Serikali kuzisimamia hizi hoteli wakatafute wawekezaji ambao wana nia njema ya kumsaidia Rais ndani ya Taifa hili. Haiwezekani nguvu za Taifa zinapotea, hoteli zimejengwa kwa fedha za walipakodi na wao bado wameacha tu hoteli zinaninginia hazijulikani zinafanya kitu gani, maana yake ni nyumba wanaoishi watu wengine.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri hapa na kwenye Kamati tumeshauri jambo hili pia, wakapitie upya mikataba na watuletee taarifa haraka iwezekanavyo kwa hoteli ambazo zimebakia ziweze kupewa wawekezaji wengine ili tuweze kupokea wageni wengi ndani ya Taifa hili na tuweze kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza sana kwenye bajeti za taasisi za TAWA pamoja na TANAPA. TANAPA ndiyo wametuletea Serengeti awards na wanazo hifadhi 22 wanao uwezo wa kuleta awards nyingi sana ndani ya Taifa hili, lakini wewe unawaambia watu hawa wanakuletea tuzo, wanaleta wageni, wanatangaza Taifa lako, halafu unakwenda kuwanyima bajeti kila siku zinavyokwenda, unategemea wanaweza kufanya kazi ipasavyo? Kelele, kero na changamoto za wanyamapori zinazoendelea wataweza kuzidhibiti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye bajeti yao ya miaka minne miradi ya maendeleo 2019/2020 walipewa bilioni 70, mwaka 2020/2021 wakapewa Bilioni 69, mwaka 2021/2022 walipewa bilioni 64.5, mwaka 2022/2023 wamepewa bilioni 60. Kila siku zinavyokwenda mnawashushia fedha mnategemea hawa watu wataweza kuleta changes? Kama hatuhitaji utalii bora tufunge tuendelee na biashara zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri pia Serikali kwenye suala la Bonde la Kilombero liweze kupandishwa hadhi kwenda kuwa Hifadhi ya Taifa ili tunusuru mradi wa Mwalimu Nyerere ambao umepoteza fedha nyingi za Taifa hili kila mtu anajua pia ukasaidie Taifa hili kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Wajumbe wenzangu wa Kamati mimi siungi mkono mradi wa bilioni 345 ambazo zitakwenda kulipwa na walipa kodi wa Taifa hili. Wenzangu wamechambua vya kutosha kwenye mradi huu, lakini hapa kitu ambacho kinanisikitisha kwamba dola milioni 71.9 zinakwenda kutolewa leseni za makazi. yaani unachukua dola bilioni 71 unakwenda kuzipeleka kwenye makaratasi lakini watu hawana migogoro ya ardhi kila siku inaendelea. Kodi watu hawawezi kukusanya vizuri, vijiji havipimwi, leo umechukua fedha umezipeleka kwenye leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siungi mkono kiukweli na uwezekano niwaambie kwa sababu huu mradi ni wa miaka mitano, fedha zimeshakopwa tayari, tuliongea na Wizara wakati wa Kamati tukiwa chumbani na tukawaambia wakasema fedha zimefika na ninyi mnachotakiwa mtupe baraka tu, tunatoa baraka kwenye jambo kama hili la kuhatarisha maisha ya Watanzania? Mimi nadhani wakaupitie tena mradi, kukopa ni jambo lingine lakini kupanga matumizi ya huo mkopo pia ni jambo jingine. Kama tunahitaji kulisaidia Taifa hili ni vema wakarudi wakakaa kitako waupitie mradi vizuri wakau-review, waweze kuwasaidia Watanzania ambao fedha hizi tutakwenda kuzilipa kwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la mwisho kuhusu Watendaji wa Sekta ya Ardhi. Kumekuwa na migogoro mingi sana ya ardhi kwenye masuala ya kupima, kupanga na kupata leseni na watu kupata hati ama vile vibali vya kupanga. Hapa Dodoma unapokendwa Watendaji wamekuwa na jeuri sana, sasa hawajui kwamba wamekalia vile viti kwa ajili ya kumsaidia Rais, wao kama wamekuwa na jeuri hawawezi kuwasaidia Watanzania mtu ukishindwa kazi si uache? Kwa nini unaendelea kuingangania? Watu wanakwenda kwenye ofisi na wanawaomba mahitaji, jinsi wanavyowazungusha na wengine wanaambia live wawape rushwa kitu ambacho siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mnyonge ameweka shamba lake amekwenda amepimiwa, sasa kutoa kibali ili aweze kuuza shamba lake nalo wanamzungusha utafikiri wao wamemsaidia kununua hilo shamba! Haya mambo hayana afya na hayawezi kulisaidia Taifa letu. Ninashauri sekta ya ardhi iende ikaji-reform kuanzia Watendaji wakakae chini na wasijaribu kufanya makosa kwamba wakiona mtu kafanya makosa Dodoma wanampeleka Serengeti, kwa hiyo, ule uchafu wa Dodoma aondoke nao akauhamishie na awaambukize watu wa Serengeti hilo jambo hatutakubali na wala hatutaliunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)