Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na mchango wangu mahususi nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa maelekezo na wananchi 1,142 wa Jimbo la Ngara waliokuwa wanadai fidia muda mrefu baada ya mashamba yao kuvamiwa na maji wakapata hasara kubwa, kulipwa Shilingi Bilioni Tatu na Milioni Mia Tisa. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara ninamshukuru Rais wetu kwa upendo mkubwa alionao kwa Watanzania na kwa fedha hizi ambazo amezituma Ngara ni ushahidi na ushuhuda kwamba Rais wetu anawapenda na kuwajali Watanzania, ndiyo maana sisi wananchi wa Jimbo la Ngara tunatambua jambo la Mama na tuko nae hadi 2030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo kuna watumishi mbalimbali wa Serikali walishiriki kwenye mchakato wa kuhakikisha wananchi wangu wanapata fidia hiyo. Mathalani Waziri wa Nishati Mheshimiwa Januari Makamba amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ngara wanapata fedha yao.

Vilevile Mkuu wa Wilaya ya Ngara Mheshimiwa Kanali Mathias Kahabi nae amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha tunachakata hizi fedha na wananchi 1,142 wanapata shilingi bilioni tatu na milioni mia tisa. Kwa upendo mkubwa tunamshukuru Mheshimiwa Rais, tunamshukuru Mheshimiwa Makamba pamoja na Mkuu wetu wa Wilaya kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nielekeze mchango wangu kwenye ile sheria kandamizi ambayo inawalipa wananchi kiduchu pale ambapo mashamba yao yanakuwa yamevamiwa na kuliwa na wanyama wakali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba dunia nzima mabadiliko ya tabianchi (climate change) yanafahamika. Mabadiliko haya yanasababisha kuongezeka kwa joto duniani ambalo linaathiri uoto wa ardhi uliopo, uoto wa asili pamoja na kuleta mvua za rasharasha, matokeo yake huko porini majani hupungua na wanyama kuanza kuhangaika kutafuta mahali pa kupata malisho. Hii ni miongoni mwa sababu kubwa zinazofanya tembo wasiweze kukaa porini na badala yake wanahainga kwenda kutafuta chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa tembo wanapotoka huko porini pamoja na simba wanafanya uharibifu mkubwa mbali na kuharibu mazao, wanajeruhi wananchi, wanasababisha mauaji ya watu pamoja na mifugo yao. Mathalani wananchi wangu wa Jimbo la Ngara wanaokaa kwenye vijiji vya Ngoma, Wakalemela, Kamuli pamoja na Mrusagamba wameathiriwa sana na wanyama tembo kwa kushindwa kukaa kwenye hifadhi na kwenda kwenye maeneo ya wananchi na kusababisha uharibifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Kanuni inaitwa The Wildlife Conservation Dangerous Animals Consolation, Regulation of 2011. Hii ni kanuni ambayo inawaumiza Watanzania, kama ambavyo wachangiaji wa kamati hii wameshaeleza tokea asubuhi, ukienda kwenye regulation 4(1) utakuta kwamba sheria hii imeeleza kwamba kama mwananchi analo shamba lenye ukubwa zaidi ya heka tano na shamba lile tembo wakalivamia na wakala lote wakalimaliza, sheria hii inasema kwamba mwananchi yule atalipwa tu hekari tano pekee hata kama alikuwa amelima hekari 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uwekezaji kama uwekezaji mwingine. Kilimo ni biashara kama biashara nyingine, mbali zaidi kanuni hii imesema mwananchi huyu atalipwa Shilingi Laki Moja kwa hekari moja. Naomba Waheshimiwa Wabunge mfikirie, mwananchi wamekopa pesa ameandaa shamba, amenunua mbegu, amepanda, hajavuna tembo wanakuja wanaharibu shamba lake, halafu sisi tunaoona wanyamapori ni bora kuliko Watanzania, tunasema kwamba acha mashamba yaharibike sisi tembo waweze kuishi kwa kula mashamba ya watu halafu tunafidia Shilingi Laki Moja Moja kwa heka moja, siyo sawa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna jambo tunatakiwa kulifanya kama Bunge ni kuhakikisha hii kanuni tunaiitisha inafanyiwa marekebisho na badala ya kutoa kitu kinaitwa kifuta jasho na kifuta machozi, sheria hii iende ikatoe full compensation kwa sababu wananchi hawa wanakuwa wamewekeza kwenye mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea eneo hili sheria hii inasema kama wanyama hawa hasa tembo wametoka porini wamekuja kwenye shamba lako wakafanya uharibifu kwenye robo ya shamba ama nusu ya shamba, sheria inasema wewe mwananchi hutakiwi kufidiwa kitu chochote. Sasa wananchi wa kawaida wanajiuliza ina maana tembo akishafika kwenye shamba la migomba wakila nusu kile kilicholiwa inakuwa siyo migomba tena inakuwa ni mitipori au ni nini? Tunajiuliza hivi basis ya hii sheria wakati inatengenezwa ilikuwa na maana gani? Tunawatesa Watanzania (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania ameweka fedha yake pale tembo wakila sisi tunafurahi kwa sababu kule porini kuna njaa basi tembo amekuja amekula migomba ya mtu anarudi akiwa ameshiba, wewe unaleta mtalii unakusanya fedha lakini mkulima anaendelea kuumia! Jambo hili siyo sawa. Ninaomba Bunge hili miongoni mwa maazimio ambayo Bunge linatakiwa lichukue iwe ni kwenda kubadilisha hii kanuni badala ya kutoa kifuta jasho pamoja na kifuta machozi iweze kutoa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa maazimio ambayo Bunge linatakiwa lichukue iwe ni kwenda kubadilisha hii kanuni badala ya kutoa kifuta jasho pamoja na kifuta machozi iweze kutoa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafuatilia muda wangu bado kabisa; ukiangalia kwa mfano pale ambapo wanyama wamesababisha madhara makubwa hasa kuuwa, wenzangu waliyotangulia kuchangia wameshasema kwamba ikitokea mwanadamu ameuliwa na mnyama mkali, fidia iliyowekwa na kanuni hii ni shilingi milioni moja. Sasa mimi najiuliza assume sisi wote hapa tulipo ni Wabunge, umefanikiwa umemuoa mke wako mzuri, umezaa naye watoto wawili au watatu, mtoto wako anatoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine katikati anakutana na tembo ama anakutana na simba, yule mtoto analiwa halafu unakuja kukutana na Serikali wanakuambia pole sana kwa kupotelewa na mtoto wako, tena mtoto wa kwanza au wa pili ila tutakuja kukupa kifuta machozi shilingi milioni moja, haingii akilini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kuwafuta machozi wananchi wetu tunawatia hasira, twende mbele ukiachana na hapo anapokuwa amekufa mwanadamu, anapopata ulemavu wa kudumu hebu fikilia kwanza kwa mfano ukipoteza reception na ulikuwa hujaolewa na hutopata mchumba tena, sheria inasema upewe shilingi laki tano. (Makofi)

Sasa mimi najiuliza hivi hizi sheria wakati zinatengenezwa mwaka 2011 factors ambazo tunaziona sasa hivi zilikuwa ni zile zile au zimebadilika? Na ndiyo maana napenda kushawishi Bunge hili hizi kanuni ziende zikafanyiwe marekebisho ili ziende zikatende haki kwa Watanzania, wananchi wetu waweze kupata compensation inayolingana na madhara wanayokuwa wameyapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo linachekesha kwenye kanuni hii, inapotokea labda ametoka simba porini, halafu yule simba ameingia kwenye zizi la mifugo na ndani ya lile zizi la mifugo kuna mbuzi, kondoo halafu yule simba akaenda akawala wale mbuzi na kondoo sheria yetu inasema yule mwananchi kwa upande wa mbuzi atatakiwa kufidiwa shilingi 25,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 25,000 ni fedha sawa ya kununua jogoo tena kipindi kingine ukikutana na jogoo lilotulia shilingi 25,000 haitoshi. Sasa unajiuliza mwananchi amepata hasara. amepoteza kondoo, amepoteza mbuzi, Serikali inakwenda kumlipa shillingi 25,00 kwa kila mfugo uliyopotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanawaumiza Watanzania na kipindi kingine Watanzania hawana pa kulalamikia ndiyo maana wanatutuma sisi tuje hapa tuwasemee na ndiyo maana ukienda kwa upande wa ng’ombe, thamani ya ng’ombe mmoja ni kuanzia shilingi 700,000 mpaka shilingi milioni tatu. Sheria inasema inapotokea mifugo ya mwananchi imeliwa na wanyamapori hasa simba, sheria inataka mwananchi yule apewe shilingi 50,000 kwa kila mfugo uliopotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wangu wa Ngara wa maeneo niliyoyataja mwanzoni walishasema ng’ombe wakiliwa hii fedha haiwasaidii chochote badala yake inawapa fedheha, mwananchi anapoteza mifugo miwili, mifugo tatu halafu Serikali inakuja kulipa fidia ya shilingi 50,000 kwa kila mfugo, wananchi tunawaumiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kwa unyenyekevu mkubwa Bunge lako tukufu liazimie twende tukafanye mabadiliko ya hizi sheria pamoja na hii kanuni, tuwafute Watanzania machozi kweli, tusiende kuwadanganya huku moyoni tunafurahia kwamba sisi tumeshaona kwamba Mifugo na yale mashamba ni vyanzo vya chakula kwa wanyama wetu waliopo porini, pengine tunawaza hivyo, lakini kama hivyo ndivyo sivyo ninaomba Bunge liazimie sheria hizo ziende zikafanyiwe marekebisho na wananchi wetu waweze kupata compensation ambayo kwa kweli ni nzuri na iliyotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mchango wangu unaishia hapo. (Makofi)