Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati zote mbili ambao wamewasilisha leo kwa taarifa zao nzuri. Pia kipekee niwapongeze Wajumbe wa Kamati hizo.
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala ya TAMISEMI na katika Kamati yetu tulipata bahati ya kuzikutanisha Kamati mbili. Kamati yetu ya Utawala ya TAMISEMI pamoja na Kamati ya Ardhi na tulikutanisha Kamati zote mbili baada ya karibu kila halmashauri tuliyokwenda kwenye ziara, tulikuta kuna migogoro mikubwa sana ya ardhi. Tulifanya kikao cha pamoja, lakini mwisho tulikuja na maazimio ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti ameyazungumza kwenye hotuba yake.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka kuzungumza kidogo kuhusu migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma. Wananchi wa Jiji la Dodoma wanateseka sana na migogoro ambayo ilitengenezwa. Tunayo maeneo ambayo yalipimwa awali kama mashamba ya mjini. Waliopimiwa wakatoweka, baada ya miaka 30 Dodoma imetangazwa kuwa jiji, wakarudi lakini maeneo hayo yaliyopimwa kama mashamba Serikali haikuyafanya kuwa mashamba yakageuka yakawa vijiji. Dodoma ilipokuwa Makao Makuu likaibuka wimbi la kupima maeneo kupata viwanja. Dodoma wakaenda kupima maeneo kwenye hivyo, kupata viwanja, matokeo yake wanasema hayo maeneo ni mali yao kwa sababu walishayapima wakati wenyeji wa maeneo hayo walikuwa bado hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, haikuwa imefanyika land acquisition kabla ya kutengeneza hizo broad acres au hizo town farms ni mashamba ambayo ya mjini kuwapa hawa watu na hawa watu walitoweka hawakuyaendeleza. Wenye mashamba yao wananchi wenyeji wa pale wakaendelea kuishi kwenye maeneo hayo. Wamekuja wamepima wanasema haya maeneo sasa ni ya jiji.
Mheshimiwa Spika, ninao mfano mmoja, mwananchi mmoja alikuja anaitwa Daudi Samamba kwenye stendi hii ya kuelekea Bahi. Kushoto kwake kuna go down ya Banj, kulia kwake kuna stendi wamepima jiji. Yeye amebaki katikati ana heka 15, wamekwenda wamepima pale wamemnyang’anya wanasema haya maeneo ni ya jiji, lakini wote wa kushoto na kulia ambao tayari wamekwishabinafsisha, wamebinafsisha kwa kuuziwa na huyo huyo kama mwenyeji. Matokeo yake huyu mtu amekwenda kwa Mkuu wa Wilaya, amekwenda kwa Mkuu wa Mkoa, amekwenda kwa Kamishna. Kamishna ameelekeza kwamba wamtafutie eneo lingine mbadala.
Mheshimiwa Spika, huyu mwananchi akapelekwa Kikombo karibu kilometa 60 kutoka hapa mjini. Kule anaenda kuambiwa alipie tena ardhi kama mnunuzi mpya. Umemnyang’anya mwananchi kutoka kwenye prime area, hukumpa fidia heka 15, unampeleka kumpa viwanja vitano ambavyo havifiki heka moja halafu una mwambia anunue ardhi. Huu ni udhulumaji, huu ni wizi na huu ni uonevu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Kamati yetu imekuja na mapendekezo kwamba, hauwezi ukalitengeneza tatizo halafu ukaachwa pale pale kutafuta suluhu ya tatizo hilo. Maafisa waliohusika kwenye kutengeneza tatizo la migogoro mikubwa ya ardhi katika Jiji la Dodoma, bado wapo na ndiyo bado wanawasikiliza walalamikaji. Wizara ichukue hatua, hawa watu wawekwe pembeni, watafutwe watu ambao kutoka sehemu nyingine ambao hawana interest, waweze kuwasaidia hawa wananchi wa Dodoma ambao wanateseka wengi kwa sababu watu wanaoshughulika ni wale wale ambao wametengeneza tatizo hilo. Wananchi wapo na nadhani jambo hili linaeleweka vizuri kwenye Kamati.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tulikuwa na Kamati ya Mawaziri Nane. Walikuja Geita Mjini lakini mchakato unaujua vizuri. Tulianza kwa kutengeneza mchakato wa Wabunge kuleta maoni, Viongozi wa Wilaya kuleta maoni. Kwa hiyo yako maeneo ambayo sisi kama Wabunge na wawakilishi tuliamini kwamba haya yamekuwa sababu ya mgogoro wa kila siku. Wamesema baadhi ya Wabunge hapa kwamba watu wanakamatwa sana na Maaskari wa Maliasili na Maaskari wa Misitu. Nikisema maeneo haya tayari yamekwishakuwa sehemu ya makazi. Pale Geita Mjini tuna msitu wa Osindakwe. Msitu wa Osindakwe umepoteza sifa ya msitu kwa sababu tayari kuna watu wanakaa mle ndani.
Mheshimiwa Spika, tulipendekeza msitu ule urudishwe kwa wananchi kama yalivyo maeneo mengine hasa kwenye taarifa ambayo Mheshimiwa Rais ameidhinisha, eneo lile linazuiliwa kwamba ni chanzo cha maji. Hakuna kisima, hakuna bwawa, hakuna mto, hakuna chochote. Kwa hiyo kila siku wananchi wanakamatwa pale na kutozwa faini na kunyanyaswa kwamba kuna chanzo cha maji wakati ni katikati ya mji na hakuna kitu chochote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu hapa, kuna migogoro mingine tunaitengeneza wenyewe. Tunaleta manung’uniko bila sababu za msingi kwa sababu watendaji wengi wanalazimisha kushikilia maeneo ambayo tayari walishindwa kuyazuia yakapoteza sifa.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Kamati yetu ilizungumza na Wizara ya TAMISEMI. TAMISEMI wanaisimamia TARURA. Tunaipongeza Serikali kwa kuongeza fedha kutoka shilingi bilioni 200 kwenda karibu shilingi bilioni 800. Bado kuna tatizo kubwa sana la barabara. Pale Geita mjini tunao mradi wa TACTIC. Tumeuzungumza sasa takribani mwaka wa tatu, wa nne. Kuwepo kwa mradi huu kunasababisha hata kwenye mgao wa fedha zingine za maendeleo, inapofika habari ya Geita Mjini unaambiwa kwamba ninyi mna barabara ya TACTIC, lakini mradi hauanzi, mradi haukamiliki. Nilianza kuuzungumza mimi wakati wa awamu ya kwanza ya ubunge wangu, sasa nakwenda awamu ya pili ya ubunge wangu, mwaka uko katikati.
Mheshimiwa Spika, ombi langu, jambo hili kama lipo, yafanyike maamuzi ya mradi huu uweze kuanza haraka ni pamoja na ujenzi wa Stendi ya Geita Mjini iko ndani ya mradi huu. Fedha tuliambiwa zipo, wamekwishakuja watu wa upembuzi yakinifu kutembea zaidi ya mara 10. Sasa mwisho unajiuliza, kama gharama hizi za kulipa posho watu njoo rudi, njoo rudi ni sehemu ya package hii, si mwisho itafika nusu wamelipana wao kwa ajili ya kuja kukagua eneo? Kwa sababu umeshakuja zaidi ya mara 10, kila siku unakuja unaenda, unakuja unaenda, mradi hauanzi.
Mheshimiwa Spika, ombi langu, mradi huu kama upo, uanze na kama haupo ijulikane kwamba huu mradi haupo. Hakuna kitu kinatesa wananchi kama unaambiwa mradi huu utaanza kesho halafu unachukua tena mwaka mwingine mradi haujaanza.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kusema ni jambo la ajira. Tunaishukuru sana Wizara ya Utumishi, Ofisi ya Rais, imerahisisha zoezi la interview. Tumepeleka kwenye kanda, lakini hoja yangu iko pale pale, kama tumeweza kupeleka kwenye kanda, zamani tulikuwa tunasafirisha watu kwenda mpaka labda Dodoma kutoka nchi nzima, tulizungumza hapa tukasema tuna watu wengi ambao wanatafuta kazi wenye sifa, shida imekuwa ni nafasi. Ile database ambayo imetengenezwa na Wizara ya watumishi ambao wamekwishafanya interview wasilazimike watu kufanya interview zaidi ya mara mbili au mara tatu.
Mheshimiwa Spika, tunaona, PCCB wanatangaza nafasi miezi mitatu, miezi mingine mitano wanatangaza tena, wanaoomba ni 8,000. Wanaochukuliwa ni 200, maana yake ni nini, wanao-qualify wapo zaidi ya 1,000.
Hatuna sababu ya kuendelea kila siku tunatangaza jambo lile llile kwa sababu tunaingizia watu gharama, hasara halafu unakuta mtu anafanya interview moja mara 20, maswali yale yale na wanakwambia ni very simple questions. Mtu anaulizwa maswali yale yale lakini hafaulu mtihani anafanya mara 10. Sasa tutengeneze hii kanzidata, mtu akifanya mtihani, aki-qualify pawe na cut off point ikitokea mahali kuna nafasi zimetangazwa na zipo, waitwe walio-qualify hata kama mwanzo walikuwa wameitwa watu 100, sasa zimepatikana 200, waulizwe je, bado una-interest na kazi hii? Kuliko kila tunapokuwa na ajira tunatangaza upya, tunaita watu wapya, tunaita new brains kutoka shuleni, watu wamekaa mtaani wana miaka minne, wamefanya mtihani mara 10, wakienda kupambana na vijana kutoka chuo kikuu juzi wanashindwa, watu wanazeeka na vyeti ndani.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)