Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia ripoti zetu za Kamati zetu hizi mbili na specifically nataka nichangie ripoti ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukurasa wa kumi na moja wa taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wetu wa Kamati hii unaongelea habari ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika halmashauri nchini. Wanasema Bunge limeazimia kupitia upya miongozo ya namna ya kutekeleza miradi hii, na kwamba Kamati imejulishwa na Serikali kwamba tayari imeshafanya mpango wa kushirikiana na UNCDF kwa ajili ya kuandaa mipango hiyo mipya ili miradi hii iweze kutekelezeka fairly.
Mheshimiwa Spika, miradi hii ya kimkakati ni kielelezo kinachoishi, kinachoonesha namna gani kama Taifa hatuko sawa katika ugawaji wa rasilimali za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, miradi hii ya kimkakati ni kielelezo kinachoishi, kinachoonesha kwamba kama Taifa hatuko sawa katika ugawaji wa rasilimali zetu, nitaelezea.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi hii ya kimkakati sharti lake kubwa la kwanza lilikuwa ni halmashauri itenge fedha, halafu ipeleke andiko. Kwa jinsi halmashauri zetu zinavyotofautiana kimapato mathalani unapozungumzia Halmashauri ya Handeni Mjini own source yetu hata milioni 700 haifiki, tutaigawaje gawaje hiyo fedha mpaka tupate fedha ya kuwekesha ili Serikali ije kutuunga mkono kupata mradi wa kimkakati. Hiyo ndiyo kusema wale giants wote wataendelea kupata miradi hii, halafu sisi ambao siyo giants tutaendelea kukosa miradi hii. Tunatengeneza Taifa ambalo linawapendelea wengine na kuwatweza wengine. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa naomba na naiomba sana Serikali huu mwongozo wanaouandaa kwanza pana kitu cha ajabu sana, mimi nilifikiri kwamba mwongozo wanamna ya kugawanya miradi hii Wizara tu ingeweza kufanya kwa maana Serikali tu inaweza kufanya. Yaani sisi kuandaa muongozo wawape Mradi uende mpaka tulete UNCDF? Yaani ndiyo Serikali mmefikia hapo? Yaani kwamba ninyi hamuwezi kufikilia kabisa namna gani tugawanye fairly mpaka tulete hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu jinsi ilivyo unavyogawanya kwa kupeleka kwenye miji mikubwa peke yake unasababisha vijana wetu kutoka Handeni na maeneo mengine ya Tanzania wahame kwenda kwenye hii miji mikubwa, unaenda kusababisha mrundikano pale, watoto wetu wanatafuta ajira pale, vijana wetu wamejaa Dar es Salaam, wamejaa Arusha, wamejaa Mwanza wametoka kwenye vijiji huko kwa sababu hatupeleki miradi hii.
Mheshimiwa Spika, nitaongelea kwa pamoja na mradi huu wa TACTIC maana ni yote hii ni miradi inayokwenda sambamba. Mradi huu wa TACTIC unatupa master plan kwenye mradi, unatupa barabara, unatupa soko na unatupa stendi, cha kushangaza hii miji inayosema ni giants na inayopewa hii miradi ya kimkakati ndiyo hii hii tena ambayo ipo kwenye TACTIC na imepewa kipaumbele ya kwanza, yaani kule kwenye mmewaweka tena kwenye TACTIC na ambako nako watapata soko, halafu unaacha miji kama Bunda inashangaa shangaa, Handeni Mjini tunashangaa shangaa, Ifakara tupo tupo tu, Kondoa, Mafinga, Makambako tunatengeneza Tanzania gani hiyo ya kujenga Dar es Salaam kila siku?
Mheshimiwa Spika, lazima tufike mahala rasilimali za nchi yetu tuzigawe kwa usawia na hili niwaombe wenzetu wa TAMISEMI wakae na watu wa Wizara ya Fedha, kaeni na watu wa Wizara ya Fedha kama fedha hizi tulizonazo zetu za mapato ya ndani na hizi tulizokopa World Bank hazitoshi kuendeleza miji yetu, kaeni na Wizara ya Fedha ili twende tukatatue tatizo hili kwa kutumia Sera za Kikodi. Hivi nani hapa anaweza akasimama aniambie eti Mbuga ya Katavi siyo bora kuliko Serengeti? Katavi iko vile leo ni kwa sababu miundombinu iko mibovu tu pale. Kwa nini hatugawanyi rasilimali hizi kwa kufuata huo uhalisia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali na hususani TAMISEMI waachane na hii habari ya kuzunguka nchi nzima eti wanatambua vyanzo vya mapato. Sasa ukienda Handeni unatambua vyanzo vya mapato? Utakuta sisi ni mnada tu pale kila siku sisi ni mnada tu. Kutengenezwe district economic profiles kwa nchi nzima ambazo zitaonesha…
MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Nhamanilo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Isack Kamwelwe.
T A A R I F A
MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumpa taarifa mzungumzaji anaeendelea kwamba mwongozo wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha TAMISEMI wameelekeza halmashauri zinazokusanya mapato chini ya bilioni moja kwenye mapato yake zitenge asilimia 20 tu ya maendeleo, lakini zile ambazo zinapata zaidi ya bilioni tano zinatenga asilimia zaidi 50 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa hiyo, unachozungumza kama Handeni milioni 700 asilimia ishirini tu zitaingia kwenye maendeleo, lakini zingine zote ziingie kwenye OC. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Nhamanilo unaipokea hiyo taarifa hiyo?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, namuheshimu sana mzee wangu, kama amenisadia nashukuru sana unajua nina moto hapa. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Reuben, unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Isack Kamwelwe?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ninaipokea taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachokisema tusiwe waumini wa vyanzo vya mapato, tunachotakiwa ni kutengeneza district economic profiles na siyo hizi ambazo mmeweka kwenye website eti district economic profile inaongelea tu watu, eti kuna watu idadi kadhaa, idadi kadhaa tengenezeni district profiles ambazo zinaangalia potentials za eneo husika ili mjue ni mradi gani mkiwapelekea unawa-boost. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunacho Chuo cha Mipango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha upo, chuo hicho mnacho wenyewe kwa nini makitumii kupanga? Kwa nini hamkitumii kutengeneza hizi Districts profile kwa ajili ya kuangalia potentials za uchumi wa kila eneo ili tupeleke fedha maeneo hayo kwenye miradi hii ya kimkakati tuka- boost eneo lile? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninatamani sana na ninashauri kwenye maazimio yetu tuongezee azimio, ikiwa tu hii miradi ya kimkakati ambayo Serikali imekuwa ikiiendesha miaka yote hawakuwa hata na mWongozo mpaka leo, na yenyewe ni ya bilioni kama 200 na kitu, je, itakuwaje kwenye huu mtadi mkubwa wa TACTIC ambao ni wa karibu bilioni 600? Wanauendeshaje? Ile tu ya kujenga soko, stendi, hapa na pale hawakuwa hata na mwongozo, huu mkubwa! Ni nani aliyewaambia kwamba, hii first tire inatakiwa iwe hii Miji, kwa nini isiwe Handeni na sehemu nyingine? Tuweke azimio la kwamba mradi huu wa TACTIC ukapitiwe upya na upangwe kulingana na namna ambavyo Halmashauri zinazohitaji kusaidiwa kwa uharaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa nimalizie…
SPIKA: Sekunde 30, malizia.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa nimalizie ni hapohapo kwenye kuangalia sera za kikodi kulingana na eneo husika. Kwa mfano, Tanga tunalima mkonge, kwa nini isiwekwe sera ya kikodi kuliendeleza eneo la Tanga kwenye uzalishaji wa mkonge? Mathalani, Mwekezaji yeyote atakayewekeza Tanga ndani ya miaka hii 20 hatatozwa corporate tax. Eeh! ni mfano tu, si watu wote wataenda ku-flock huko? Kwa mfano, Katavi unasema Mwekezaji yeyote atakayejenga hoteli corporate tax yake tutamtoza tano siyo kwamba watu watapeleka hoteli huko? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama watu wa Serikali wamechoka kufikiria wapishe hizo siti wakalie watu wengine wafikirie. Baada ya kuyasema haya nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi/Kicheko)