Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikupongeze wewe kwa kuiunda Kamati hii ambayo tunafanya kazi nao kwa karibu sana chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Tunawashukuru Wajumbe wa Kamati kwa sababu wakati wote ambao tumekuwa tukipokea maoni ya Kamati hii tumekuwa tukifanyia kazi ipasavyo. Unaweza ukaona hakuna hoja nyingi kuhusu Wizara yetu. Zipo hoja tano ambazo Kamati imeibua na moja ambayo Mheshimiwa Festo Sanga ameizungumza mdau wa karibu sana katika sekta hii ya michezo na sisi tunamshukuru sana kwa ukaribu wake.

Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kwamba wakati Mheshimiwa Rais anaianzisha Wizara hii alizingatia yale maelezo ambayo Rais wa Awamu ya Kwanza aliyatoa wakati anaanzisha Wizara ya Vijana na Utamaduni. Tutahakikisha kwamba yale maono na fikra za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaziendeleza na tunatambua kwamba anguko la sekta zetu ambazo tunazisimamia hasa Sekta ya Utamaduni ni anguko la Taifa letu. Kwa hiyo tutapambana kuhakikisha kwamba yale maono ya wazee wetu, viongozi wetu waasisi wa Taifa hili tunayalinda na kuyasimamia ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wadau katika sekta zetu hasa sekta za michezo, kwa kuona namna ambavyo Serikali inafanya kazi kubwa katika kuboresha sekta hii. Nawashukuru wadau kwa kukubali mapinduzi makubwa ambayo tunakwenda nayo katika Sekta ya Michezo, Sanaa na Utamaduni.

Mheshimiwa Spika, nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba, leo tumepokea taarifa kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi ambazo zinafanya vizuri sana hasa katika ligi bora Afrika na Tanzania. Kwa takwimu ambazo zimetolewa leo ni ligi namba tano katika ligi bora kabisa Afrika, kidunia Tanzania ni ligi namba 39 kwa ligi ambazo zinafanya vizuri kabisa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha tunaendeleza yale ambayo viongozi wetu Mheshimiwa Rais anatamani yatokee katika sekta hii. Nikiri kwamba tuko katika mapinduzi makubwa kwenye sekta hii na tunatambua kwamba hii ndio sekta ambayo Serikali tunatumia kama nguvu shawishi yaani soft power ya nchi. Hivyo, tutahakikisha maelekezo ya viongozi, maelekezo ya Kamati na maelekezo yako tunayafanyia kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, tunayo mambo matano ambayo yameibuliwa, lakini nianze na hili suala la kuhusu Kiswahili (BAKITA) kama ambavyo wewe mwenyewe ulivyosema. Niseme tu kwamba maneno yote ambayo uliyazungumza yaliyowasilishwa ni maneno fasaha na sanifu kama ambavyo yamewasilishwa kwa mujibu wa sarufi ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, katika Kiswahili kuna kauli tano za msingi zinazoathiri maumbo ya vitenzi, kauli hizi ni kama ifuatavyo: -

(a) Kauli ya kutenda;

(b) Kutendwa;

(c) Kutendewa;

(d) Kutendana; na

(e) Kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sarufi za Kiswahili zina kanuni ya kubadilisha vitenzi kuwa nomino na katika kukamilisha mchakato huo, kiambishi ā€œuā€ huwekwa mwanzoni na kiambishi ā€œgā€ huwekwa mwishoni. Kwa hiyo yale ambayo yamezungumzwa ni Kiswahili fasaha na sanifu kama ambavyo naomba nielekeze hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Kamati iliibua mambo kadhaa, jambo la kwanza, ilikuwa ni msingi wa uibuaji wa vipaji; jambo la pili, ni ujenzi wa viwanja kwa ushirikishwaji wa wadau; jambo la tatu, ni kuhusu vazi la Taifa; jambo la nne ni kuhusu mdumdo wa Taifa (beats); na jambo la tano, ni kuhusu Chuo chetu cha Malya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Festo Sanga aliuliza kuhusu hatua ambayo Serikali imefikia katika ujenzi wa viwanja. Sisi kama Serikali tumefanya kazi kubwa sana ya kuwashirikisha wadau katika kuibua vipaji. Hata hivyo, nichukue fursa hii katika kushukuru Maafisa Utamaduni kote nchi nzima ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa na kazi nzuri sana ya kutambua vipaji katika maeneo yetu. Tunatambua katika vijiji, vitongoji, kata na wilaya kuna vijana wengi sana wenye uwezo na wenye vipaji vikubwa, lakini hawatufikii kwa ukaribu kwa sababu ya maeneo waliyopo. Tumekwishawaagiza na tumefanya vikao kadhaa na Maafisa Utamaduni ambao tumewekeana mikakati ya namna gani tunaweza kwenda kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaibua vipaji.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza sana Watanzania ambao wanatumia vipaji vyao kama mtaji wao hasa wale Ramadhan Brothers ambao wamefanya kazi kubwa kutangaza nchi yetu, kutangaza utalii wa Tanzania, vile vile na wadau wengine wadau wengine ambao wamekuwa wakiibuka, akiwemo bwana Mandoga amekuwa akifanya kazi nzuri, nje ya mipaka ya Tanzania, anaitangaza vizuri Tanzania. Hata hivyo sisi kama wizara tunawapongeza sana kwa kazi kubwa na kazi nzuri ya kuendelea kuitangaza nchi yetu kupitia vipaji walivyo navyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishaanzisha mchakato wa mtaa kwa mtaa. Tunatambua kwamba katika nyakati ambazo tulikuwa tunaanza mchakato huu hatukuwa na bajeti ya kutosha. Tunaishukuru Kamati kwa kuendelea kutupigania, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia. Basi tunaamini kabisa katika bajeti ijayo tutakuwa tumeweka kifungu maalum kuhakikisha kwamba tunakwenda kwa kasi sana kuhakikisha kwamba tunafika kila mtaa. Dhamira yetu na dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kwenda mtaa kwa mtaa kusaka vipaji, vipaji vya mpira lakini na vipaji vingine.

Mheshimiwa Spika, eneo hili la ujenzi wa viwanja, nichukue fursa hii kumshukuru sana Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa ushirikiano wa karibu ambao tumekuwa nao. Pia nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu, tunatambua kwamba inawezekana huko nyuma hatukuwa na mipango mizuri, inawezekana ndio sababu ya kwa nini tumechelewa kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa viwanja unaanza. Hata hivyo, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mipango imekamilika, michoro imekamilika na tunaishukuru Wizara ya Fedha kwa kuridhia sisi kuendelea kwa hatua ya kutafuta mkandarasi na hatua nyingine.

Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba zabuni ya ujenzi wa uwanja wa Dodoma tayari imekwishatangazwa. Vile vile dhamira yetu sisi kama Serikali, kama Wizara ni kwenda kujenga uwanja wa kisasa ambao Afrika hakuna. Kwa hiyo tutajenga uwanja wa kisasa kweli kweli hapa Dodoma na Zabuni tumekwishaitangaza. Kwa hiyo mategemeo yetu mwezi wa tatu tutamkabidhi Mkandarasi site kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja wa mpira wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa viwanja vya sanaa, tayari zabuni tumeitangaza na hata Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuingia kwenye tovuti ya Serikali wakaweza kuona zabuni ya uwanja wa sanaa tayari imekwishatangazwa. Hata hivyo, Mkandarasi wa ujenzi wa viwanja changamani; vya Dodoma pamoja na Dar es Salaam tayari amekwishapatikana. Kwa hiyo, tunategemea wakati wowote mchakato wa ujenzi utaanza. Kwa hiyo, naomba niendelee kuwatia matumaini Watanzania. Sisi katika Wizara hii tumekwishakubaliana kufanya kazi kwa bidi, tumekubaliana mimi na wasaidizi wangu kufanya kazi usiku na mchana.

Mheshimiwa Spika, tutawathibitishia Watanzania kwamba yale mapinduzi ambayo wanatamani kuyaona yatatokea katika nyakati ambazo Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mabadiliko hayo.

SPIKA: Sekunde thelathini, kengele imeshagonga.

WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa tu kwamba ule mchakato wa ujenzi wa shule 56 tayari umekwishaanza. Tumekwishaanza kule Tabora na tutakuwa na shule saba za mfano za kuanzia na naamini kufikia mwezi wa Machi au Aprili, Mkandarasi atakuwa amekwishapatikana kwa kuwa tayari wizara ya Fedha imekwishatupatia fedha za kuanzia. Tunamshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi kubwa na nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba, Watanzania wana matumaini makubwa sana na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi katika wizara tutahakikisha tunafanya kazi usiku na mchana katika kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta hii ya Michezo, Sanaa na Utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja ya Kamati iliyotolewa mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)