Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami naungana na wenzangu wote kupongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri na ushauri mzuri sana na pongezi kubwa kwa Kamati inayotusimamia, Kamati ya Huduma za Jamii chini ya uongozi wa Mheshimiwa Nyongo, tunafanya nao kazi vizuri sana. Wanatuelekeza na kutushauri na kwa kweli hapa tulipofika kwa sehemu kubwa ni kufanya kazi pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nampongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wizara ya Elimu tunajivunia kuona kipaumbele cha elimu katika Serikali. Nitoe mifano miwili tu. Mfano, sasa hivi tunazungumzia kujenga VETA katika wilaya zote Tanzania, shughuli ambayo inaanza kabla ya mwisho wa mwaka huu, nadhani mwezi huu wa Pili tutakuwa tumeanza kazi hiyo. Hazina tayari wametuambia tunachukua fedha zote, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametuambia na kazi itaanza.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunasambaza Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 ambayo ilikuwa haijawahi kupata Kampasi ya Chuo Kikuu. Haya yote ni maelekezo ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nawapongeza sana na ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao, kwa kweli tutazingatia. Tumekuwa tukichukua kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi sana ya kusema kwa sababu mengi ya ushauri tutayabeba kama ambavyo tumeyapokea. Ila kuna jambo moja kubwa ambalo limezungumzwa napenda nilisisitize, hili ambalo tumelisikia wote hapa Bungeni kuhusu umuhimu wa walimu. Imeelezwa umuhimu wa kuwa na walimu wa kutosha na umuhimu wa walimu katika elimu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alilianzisha asubuhi kwa kueleza umuhimu wa kuwaenzi walimu wetu, nasi hilo tunalizingatia. Kama mnavyojua, Rais wetu tangu aingie madarakani, wakati tulikuwa tume-freeze employment kwa ujumla alipoingia madarakani tu tumeanza kuona, kama alivyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ajira za Walimu zimeanza na zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, tumekamilisha mwongozo sasa hivi wa kuhakikisha kwamba Walimu wanaojitolea tunaweza tukawa-engage vizuri kwa ajili ya kuchangia idadi ya walimu ambao watatosha kutoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaangalia vilevile suala la ufundishaji wa walimu. Katika mageuzi ya elimu ambayo yanakuja, jambo ambalo ni wazi kwamba tutakuwa tunazingatia sana suala la ufundi stadi; hawa wenzetu wa Zanzibar wanasema mafunzo ya amali. Kwa hiyo, tutangalia vilevile tunavyo-train walimu kuelekea huko. Nilikuwa Mtwara juzi, kuna hili moja limesemwa, nimeangalia Vyuo viwili vya Ualimu vya Mtwara. Kimoja kinaitwa Mtwara Kawaida na kingine kinaitwa Mtwara Ufundi, vimekaa vimeshikana vimepakana, lakini vyote ni Mtwara kawaida, kwa sababu ufundi haufundishwi.

Mheshimiwa Spika, tutarudi huko kwenye ufundi na kuangalia namna ya kufanya vyuo vyote viwili iwe Kampasi moja ambayo inafanya kazi na Vyuo Vikuu lakini kwa ajili ya kufundisha masomo ya kuandaa walimu kwa ajili ya Mafunzo ya Elimu ya Amali kwa sababu na fursa ile ni kubwa, karakana zipo lakini hazijatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake, suala la kuwaenzi walimu ni zuri sana. Napenda niseme hivi kwa sababu najua walimu wengine watakuwa wanasikiliza. Wamesikiwa Waheshimiwa wabunge wanavyowasemea vizuri, wamemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu anavyowasemea vizuri, tunajua kabisa kwamba hapa karibuni kumekuwa na clip zinatoka ambazo zinasababisha mpaka watu waanze kuwa na jicho tofauti kuhusu walimu. Walimu wetu popote mlipo sikilizeni Waheshimiwa Wabunge wanavyowasemea na kuwatetea na hasa tukizingatia alichosema Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kazi inayofanywa na Walimu wetu ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kuna mwalimu mmoja mfano clip yake inazunguka na napenda nimtaje hapa, anaitwa Mwalimu Yusuph Mohamed Yusuph. Huyu ni Mwalimu wa Shule inaitwa Ikorongo, iko Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara. Huyu Mwalimu anaitwa Yusuph Mohamed Yusuph, maarufu kama Yusuph Pangoma. Ana ubunifu mkubwa sana wa kufundisha, na ninatarajia wakati wa kusoma bajeti tutamwalika hapa kwa ajili ya kupewa pongezi na walimu. Wako walimu wengi sana wanafanya kazi kubwa, wanajitolea na ubunifu kwa kutegemea mazingira yale yale ambayo wanafanyia kazi. Tutaendelea kuwaenzi sana walimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi clips ambazo zimekuwa zikizunguka kama Kamati yetu ilivyosema na Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyosema hapa, kuna suala kubwa la malezi shuleni na suala la maadili ambalo ni jukumu letu vilevile. Tunashirikiana na Wizara mbalimbali; tunashirikiana na Mheshimiwa Dkt. Gwajima, TAMISEMI, tunashirikiana na Wizara mbali mbali chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, lakini ndani ya Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tuna jukumu la kufanya vilevile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema, pamoja na kwamba tumeona hizo clip, walimu wetu wengi karibia wote ni wazuri sana na wanalea Watoto wetu vizuri sana kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuendelee kuwaenzi walimu hao.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa wale wachache ambao wanakiuka maadili, unyanyasaji wa watoto kwa namna yoyote ile, kesho Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael atatangaza sasa namba ambazo zitatumika kama call center ili kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa kwamba hivi sisi tutaripoti wapi kama tukiona matukio kama haya.

Mheshimiwa Spika, mtu yeyote hasa walimu wengine ambao mkiona kuna unyanyasaji wa aina yoyote, vitendo vya uvunjaji wa maadali katika shule yoyote hapa nchini, unapiga ile namba whether unataka jina lako litajwe au lisitajwe, Serikali ipo kila mahali mpaka vijijini na kwenye vitongoji. Tukipata hiyo namba sisi tutafuatilia na kuhakikisha kwamba tunadhibiti hali kama hiyo na kuhakikisha kwamba hivi vitendo vichache sana ambavyo vinaondoa taswira kwa sababu sisi wenyewe tunafundisha kwamba samaki mmoja akioza kwenye tenga wote ameoza. Kwa maana hiyo hawa wachache wanaoharibu taswira ya walimu tutahakikisha kwamba tunawadhibiti na kwa ajili ya kulinda watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa sana hapa ni umuhimu wa hasa masomo ya hisabati na sayansi, kwa hakika. Kwa kuangalia matokeo, tukiangalia trend kwa mfano form four sio kwamba imeenda chini ukilinganisha na miaka mingine lakini bado hairidhishi. Tungependa ufaulu uongezeke hasa katika masomo ya sayansi na hisabati na nitawakumbusha tu Waheshimiwa Wabunge, ninyi mliridhia hapa Bungeni kuanzisha scholarship maalum kwa wanafunzi wanaofanya vizuri sana kwenye masomo ya sayansi. Wakimaliza form six wanasomeshwa na Serikali full time, baadaye ile scholarship tumeiita Samia Scholarship. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa ni njia mojawapo ya kuhakikisha kwamba tunahimiza watu wasome na tumesikia na tunapata mrejesho mashuleni kwamba sasa watoto wanasema ili kumwondelea mzazi wangu shida ngoja nisome sayansi na nitajitahidi ni faulu vizuri sana ili nihakikishe kwamba kweli nipata scholarship ya kwenda kusoma.

Mheshimiwa Spika, tayari wameshapata scholarship, wapo vyuoni, tutakuwa na siku moja ya kutangaza na kuonesha majina, kuonesha jinsi tulivyowachagua kwa sababu tulisema tutawachagua kwa njia ya haki kabisa kuhakikisha kwamba kila moja ambaye anaweza kupata nafasi hiyo atapata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tutazingatia katika hii walimu wa kujitolea, mwongozo na vilevile ajira zinazokuja kuhakikisha kwamba tunatoa kipaumbele kwa ajili ya walimu wa sayansi na hisabati kwa sababu kwa kweli maeneo hayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya elimu ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Waziri, swali moja tu. Hizi taarifa za huyu Mwalimu Yusuph kutoka Serengeti umezipataje?

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, huyu mwalimu nimezungumza naye vilevile na nawasiliana naye.

SPIKA: Aah, yaani yeye alikupigia akakuambia kuhusu ubunifu wake ama alijirekodi ukaona kitu? Ama ni kata iliripoti? Shule iliripoti? Kata? Yaani taarifa zake ulizipataje? Ni hicho tu.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, aliwasiliana na mimi mapema sana na baadaye niliziona hizo ambazo zimekuwa recorded anavyofundisha, nikawasiliana na wenzetu wa TAMISEMI tukam–track down, tukahakiki kweli ni mwalimu na mimi nipo constant in touch with him. (Makofi)