Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika taarifa hizi ambazo zimewasilishwa; Taarifa ya Kamati ya Ukimwi na taarifa ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ninayo furaha kubwa kuipongeza Hospitali ya Muhimbili kwa kuanzisha huduma ya Puto. Nadhani niwahamasishe wale watu waliozidi uzito ule uliokithiri, waende wakaweke. Kimsingi tumeona ushahidi kwa Peter Msechu, ndani ya wiki tu amepunguza kilo saba. Kwa hiyo, nawahamasisha sana Watanzania wenzangu, Wabunge wenzagu kutumia hii huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nirejee kwenye hoja zangu za msingi kuhusiana na Kamati ya UKIMWI na udhibiti wa dawa za kulevya. Ninarejea kwamba katika Mji wangu wa Tunduma, Mbozi na kanda nzima hii ya barabara ya Tanzam, ni moja ya maeneo yanayoathirika sana na masuala ya UKIMWI. Maeneo yote ambayo yana vituo vya ulazaji wa malori, watoto wa maeneo yale wengi wamekuwa wanatumika ndivyo sivyo, wanaharibiwa sana. Sijajua ni kwa nini madereva hawa na makonda wao wamekuwa ni watu wasio na huruma au watu wasiokuwa wa kujali kuangalia kwamba watoto wanaowaharibu ni kizazi kijacho. Kwani wanaweza wakawa wanawaharibu wale, lakini kwa sababu tunachangamana, kwa hiyo, wanapowaharibu wasidhani kwamba watoto wao wanakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu, TACAIDS waje na mkakati maalumu wa ku-control hawa madereva wanaoharibu watoto wetu kwenye hivi vituo ambako malori yanalala. Kwa sababu kanuni na sheria ndogo ndogo zipo na zinatungwa. Kitendo cha kusababisha uharibifu wa Watoto na kuwasababishia maradhi, ni kosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe tu watu wa TACAIDS kwenye hili watutazame. Watoto wetu wanaharibika sana, wanaacha shule kisa, Shilingi mia mbili mia mbili wanazokuwa wanapewa. Kwa hiyo, kwa hili naomba pia waweze kuliangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naona miradi mingi imelenga kuwasaidia wale wanaojiuza, wale ambao wanafanya ushoga na vitu kama hivyo, lakini kuwatazama wale watoto wanaotoroka shuleni na kwenda kuwakimbilia wale wa malori wapate chochote kwa sababu aidha ya njaa na nini miradi mingi katika maeneo hii haijazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya kwa namna ambavyo imekuwa ikiendelea kupamba na tumekuwa tukiona Kamishna wa madawa ya kulevya ambavyo amekuwa akiendelea kutoa taarifa mbalimbali kwamba wamekamata dawa kwa kiwango gani na ni watu gani wanahusika, japo wengine wamekuwa wanakasirika wakitajwa lakini ukweli ni kwamba madawa ya kulevya ni kitu ambacho kama nchi tumeendelea kukipinga na hatukitaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kusema nini kwenye upande wa madawa ya kulevya kwamba waraibu ni watu ambao kwa namna moja au nyingine tuna wa-term kama ni waathirika, ni watu ambao wameshakuwa dhaifu hawawezi kujitegema kiuchumi bila kuwa-supported, sasa mpaka saa hizi hatujaona mkakati ambao upo wa kuhakikisha kwamba katika kila Halmashauri kumekuwa na mratibu wa masuala ya madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Halmashauri ndiyo kiungo cha Serikali Kuu na kule wananchi chini, kwa hiyo watusaidie kuweza kupata Waratibu kwenye Halmashauri zetu ambao wao watakuwa wanaendelea kusimamia haya masuala ya vilevi na madawa ya kulevya ili kupunguza vijana wetu na watoto wetu kuona kwamba masuala ya vilevi kama fasheni. Kwa sababu wakati mwingine masuala ya uvutaji bangi, masuala ya unywaji wa pombe uliokithiri au matumizi ya madawa ya kulevya yamekuwa yakiambatana na tabia hizi wanazoita tabia za kisasa za kuona kwamba haya mambo ni fasheni. Kwa hiyo, kama tutakuwa na waratibu kule ina maana kwamba watakuwa na programu zao kupitia Halmashauri za kufanya unasihi pia kuweza kufanya hamasa kwenye jamii ya kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niseme tu kwamba nitakuwa sijajitendea haki kama nitashindwa kuongelea kuhusu Wilaya ya Songwe na mradi huu wa Peak Resources wa kuzalisha madini adimu ya magnet ambayo Tanzania nzima yamepatikana katika Kata ya Ngwala Wilayani Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliongea hili na kwa uchungu mkubwa nikiiomba Serikali yangu wawape Peak Resources leseni, ni miaka minne tangu utafiti umekamilika. Ni kitu gani kinawafanya wao washindwe kutoa leseni kwa Peak Resources. Wamekuwa wanafanya majadiliano, makubaliano ni miaka minne ni majadiliano gani hayo yasiyoisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Songwe tunaamini kabisa kama ule mradi ukianza kufanya kazi wanawake wetu wa Mkoa wa Songwe kipato kitainuka. Wataweza kuuza hata mayai, wataweza kuuza hata kuku. Watusaidie kampuni hii ya Peak Resources iweze kupata leseni, maana tumekuwa tunafuatilia amekaa hapa Mheshimiwa Mbunge wa Songwe Mheshimiwa Phillipo Mulugo kila siku analia na hicho kitu, kuna wakati amejibeba toka Songwe kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea hiyo leseni, lakini bado hiyo leseni hawakuweza kupata, sasa you can imagine kwamba ni kwa namna gani alifurahi siku hiyo na ni kwa namna gani siku aliweza kupata huzuni ya kukosa hiyo leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini hakuna mjadala unaoweza kwenda zaidi ya miaka mitano mnajadiliana tu namna ya kufanikisha hilo suala, wakati ni kitu ambacho kina maslahi kwa Taifa! Imagine magnet Tanzania nzima inapatikana Songwe, mbona madini mengine wanapewa haraka haraka dhahabu na mengineyo. Hapa nimeona kwamba wanaenda kutoa leseni za helium why not katika huu mradi wa Peak Resources?
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie forum hii kuwaomba Serikali watupe leseni kwenye hiyo kampuni ya Peak Resources ili madini yaanze kuvunwa. Nitaendelea kuwahamasisha wanawake wa Jimbo langu waione hiyo fursa itakayopatikana kule kulingana na uwepo wa hii kampuni kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiendelea kufanya kazi zake. Ahsante. (Makofi)