Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi yetu hii. Tunaona kabisa katika sekta ya nishati, umeme vijijini kuimarisha miundombinu ya umeme, ujenzi wa uzalishaji umeme katika maeneo mbali mbali, kazi inaendelea. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu lakini pia Mkurugenzi Mkuu wa REA vijijini kwa kazi kubwa ambayo wananendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mara nyingi akisimama hapa anazungumzia habari ya nishati kwamba ni mambo matatu. Jambo la kwanza anasisitiza habari ya uzalishaji na sina shida na uzalishaji, naomba nimpongeze sana kazi nzuri inaendelea kwenye uzalishaji. Jambo la pili anazungumzia habari ya usafirishaji, sina shida na usafirishaji kwa sababu miundombinu mpaka sasa inaendelea kurekebishwa na naamini baada ya muda mchache miundombinu hii itakuwa tayari imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la tatu ni suala la usambazaji wa umeme na hapa nilitaka nijikite kwenye kuzungumzia kwenye suala nzima la usambazaji. Nijikite kwenye Wilaya yetu ya Kahama. Wilaya ya Kahama ina halmashauri tatu ina vijiji zaidi ya 323, na tuna mkandarasi mmoja tu anayesambaza umeme wa REA ambaye bado mpaka sasa ana mkataba wake unaosema ni ndani ya miezi 18 awe amemaliza. Hata hivyo, mpaka sasa ni asilimia 23 tu ya kazi aliyoweza kuifanya kwenye Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Mkandarasi huyu anayesambaza uememe kwenye Wilaya ya Kahama kwa maana ya Majimbo matatu; Ushetu, Msalala na Kahama, bado uwezo wake unaonekana kuwa chini sana kwa sababu mpaka sasa ameshamaliza miezi saba na miradi bado ipo asilimia 23 tu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri na hapa niombe uchukulie Wilaya ya Kahama kama special case, kwa sababu Wilaya ya Kahama ni Wilaya kubwa ina vijiji vingi ina halmashauri nyingi. Tumeahidi wananchi wetu kwamba ndani ya miezi 18 umeme huu utakuwa umekamilika kusambaa kwenye vijiji vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani kwenye Jimbo langu la Msalala tuna zaidi ya vijiji 62 havijapatiwa umeme. Sambamba na hili tuna migodi mikubwa na midogo ambayo inaenda na inakuwa kwa kasi na inategemea nishati. Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe utakuwa shahidi ulifanya ziara kwenye Jimbo la Msalala na ulienda kwenye maeneo ya migodi, ulitembelea Ntambalale, ulitembelea Mwanzimba na maeneo mengine na uliahidi kwamba umeme baada ya wewe kutoka umeme utaenda; lakini mpaka leo Mheshimiwa Waziri bado umeme haujafika kwenye maeneo hayo. Ninaomba muichukulie Wilaya hii ya Kahama kama special case ni tofauti na Wilaya nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, wilaya nyingine utaona kijiografia eneo lao ni dogo sana tofauti na Wilaya ya Kahama. Ukichukua Jimbo la Msalala tu lenye kata 18 lina square mita nyingi sana, kazi iliyofanyika ni kata moja na maeneo machache sana mapka sasa. Kwa hiyo niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza hapa wamemuongezea tena mkandarasi huyu zile kilometa zingine mbili kwenye kila kijiji. Kazi ya kwanza bado hajamaliza na yuko asilimia 23 lakini mmeenda tena Mheshimiwa Waziri kumuuongeza tena extension ya umeme kwa kilometa mbili kila kijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wasiwasi wangu ni kwamba wananchi tumewaahidi ndani ya miezi 18 umeme utakuwa umekamilika na wamepatiwa huduma hiyo; na baadhi ya wananchi tayari wameshafanya wiring kwenye nyumba zao. Sasa kama tu kazi ya kwanza ambayo zaidi ya vijiji 323 hajamaliza, je, tumemuongeza tena kila kijiji hicho hicho kilometa mbili, kwa maana ya nguzo 40. Je, kazi hii itakamilika kwa wakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri baada ya hapa, mimi naomba tukae, tuwasiliane tuzungumze tuone namna ya kukaa mkandarasi huyo ili atahakikishie, kama uwezo ni fedha ama kuna mambo memngine basi muone Wizara mnaweza kumsaidiaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie usambazaji wa umeme kupitia TANESCO. Tunafahamu kwamba TANESCO kwa sasa bado wana fedha, Wilaya ya Kahama tuna bajeti ya fedha ya kuweza kusambaza umeme kwenye maeneo mengine. Changamoto ya sasa ni nguzo. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie kwamba kama fedha tunayo Wilaya ya Kahama lakini nguzo hazipatikani naomba Wizara itusaidie ili nguzo hizi ziweze kupatikana na wananchi waweze kupata huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nijielekeze kwenye sekta ya madini, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Madini kwa kazi kubwa ambayo anayoendelea kuifanya. Leo hii utaona mchimbaji na Mtanzania wa kawaida anamiliki leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa niseme tu, pamoja na kazi kubwa anayoendelea kuifanya kumekuwa na baadhi ya watu wanamvuta shati nyuma. Sisi kama Kamati tunaendelea kukupa moyo tunasema kwamba wale ambao wanakuvuta shati nyuma. Tutaenda kupamba nao ili kufanikisha adhma ya kuhakikisha unachangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa. Mambo ambayo yanamkwamisha Mheshimiwa Waziri, na hili nimuombe sana Waziri wa Fedha; Wizara ya Fedha imekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwenye sekta ya madini. Leo tunazungumzia habari ya umiliki wa leseni; na niwapongeze sana Mtendaji Mkuu wa Tume na Mheshimiwa Waziri, wameweza kuwapatia leseni wengi, wananchi wanajivunia kuwa na leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyosema dada yangu hapo Mbunge wa Viti Maalum hapo, Nusrati Hanje, kwamba sasa mahitaji makubwa kwa wachimbaji ni mambo mawili tu. Jambo la kwanza ni hitaji la mtaji; na hapa niombe sana BOT, ambao mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza benki kuwakopesha wachimbaji wadogo wadogo lakini benki hizo zimekuwa in reality haziendi kuwakopesha wachimbaji wadogo wadogo. Wachimbaji wadogo wadogo wanalia, leo hii wana leseni lakini wamekosa mitaji. Kwa hiyo, niendelee kuomba sana Wizara ya Fedha na hasa BOT kwenda kuhakiki kwamba ni wachimbaji wangapi ambao wameshakopeshwa fedha na benki hizi ambazo mpaka leo zinaweza kuwasaidia katika uchimbaji wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni suala linalohusu ripoti ya GST. Nipongeze sana kazi kubwa ambayo inafanywa na GST; na nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, ikimpendeza hebu tuone namna ya kutenga fedha ya kuiwezesha GST ije iweke maabara ya upimaji wa madini katika Wilaya ya Kahama ili wananchi wanaozunguka Wilaya ya Kahama, ambako ndiko madini mengi yanatoka waweze kupata fursa ya kupimiwa madini yao kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, niendelee kuomba sana muweze kutenga bajeti kubwa kuiwezesha GST iweze kununua mitambo ya drilling ili iweze kufanya tafiti za kutosha. Mchimbaji mdogo mdogo huyu anayemiliki leseni akiweza kupatiwa mtaji, akaweza kupatiwa data za kwenye eneo lake maana yake ni kwamba tutakuwa tumemkuza mchimbaji mdogo mdogo huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anapambana na mambo mengi sana kwenye Wizara hii; lakini pia aende sasa matapeli yaliyoko kwenye Wizara hii. Leo utaona Mheshimiwa Waziri watu wanatoka huko nje na briefcase wanakuja hapa. Watanzania tunaomiliki leseni na rasilimali tunabaki kuwa maskini lakini hizi kapuni nyingine; na hasa niseme tu, zile zinazotoka nje, zinakuja na briefcase pekee, lakini hapa wakiondoka wanaondoka na fedha nyingi zimejaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kuna kampuni moja, na Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kampuni hii wewe mwenyewe unaifahamu, ni QATAR Mining. Hii inachukua fedha kwenye benki zetu hizi hizi, lakini pia inachukua fedha za Watanzania. Vilevile imeanza kudhulumu hawa watu. Niombe uchukue hatua za haraka sana kwenye kampuni hii ambayo inaendelea kudhulumu Watanzania, Watanzania waweze kupata haki zao za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)