Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kama walivyosema wengine nichukue nafasi hii kwa kweli kuipongeza sana Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kwanza kwa umakini wao. Nimefanya nao kazi kwa muda sasa, ni Kamati ambayo kwa kweli weledi wake kwenye uchambuzi wa masuala ya madini hautiliwi shaka na ni watu ambao wanaenda kwenye details kwenye haya mambo yanayohusiana na Sekta ya Madini. Kwa kweli wametusaidia sana kama Wizara kuona namna gani tuipeleke mbele sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa niaba ya wenzangu Wizarani kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Kitandula na Makamu wake Mheshimiwa Gulamali pamoja na Wajumbe wote kwa namna ambavyo wamekuwa wakitusaidia sana katika kutusimamia kwenye kuendeleza Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamesemwa mambo kadhaa na nisingependa kuonekana kama najibu. Nataka tu kuchangia hoja ya Kamati na nataka nizungumze mambo matatu. Jambo la kwanza, imeelezwa hapa juu ya upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu vya uchenjuaji au refinery zetu za dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kwa msaada wa Bunge hili. Wakati tunaanza kujenga refinery hapa nchini, changamoto na matishio ya refinery hizi kupata malighafi ilikuwa je, hawa refiners watapata dhahabu kutoka kwa wachimbaji? Kwa sababu bei wanayoweza kununua inawezekana kwenye soko ikawa ya juu zaidi kuliko wanayonunulia wenyewe. Kwa hiyo tulichofanya na tulileta hapa Bungeni tukapitishiwa na Bunge ni kutoa vivutio kwa ajili ya refineries hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kivutio cha kwanza tukashusha mrabaha wa dhahabu. Dhahabu ukitaka kwenda kuuza kwenye refinery, badala ya kuchajiwa 6% ya mrabaha, yule anayeuza kwenye refinery anachajiwa 4% peke yake na hii inatusaidia kuwapa nafasi wachimbaji wale kupeleka dhahabu na kulipa mrabaha kidogo zaidi na viwanda hivi viweze kupata malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ambalo ni muhimu Bunge tukalielewa na tusiliogope. Kwa kawaida kama una kiwanda kutafuta malighafi kutoka nje ya nchi siyo dhambi, actually ni jambo zuri sana. Kiu yetu ni kuifanya Tanzania kuwa hub ya biashara ya madini. Ni vizuri tukatengeneza mazingira rafiki ya kuwavutia majirani zetu walete madini yao hapa ndani waweze kufanya refinery na mwisho wa siku waweze kusafirisha. Advantage tuliyonayo sisi kama Taifa ni kwamba madini yanayochimbwa Tanzania kwenye masoko ya kimataifa hayatiliwi mashaka kwenye ethics zake. Yamechimbwa kwa kufuata utaratibu kwa kuzingatia haki za binadamu na kwa hiyo ukienda kwenye masoko ya kimataifa duniani yananunuliwa kirahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia rasilimali zetu za ndani, lakini hatutaacha kuwavutia wengine kwa ajili ya kuja kuuza madini yao hapa kwetu. Yako Mataifa hayana hata shimo moja la dhahabu lakini yana refinery na yanatumia rasilimali za Mataifa mengine kwa ajili ya kufanya biashara. Fursa kama hiyo hatuwezi kujifungia tu ndani tukasema kwamba sasa sisi tutatumia madini yetu peke yetu halafu tufanye refinery mengine tuyaache. Ndiyo maana tunatoa wito na mataifa mengi yamekuja hapa kujifunza, tunatoa wito kwa majirani zetu kuleta madini yao kwa ajili ya kuja kufanya refining kwetu hapa nchini kwa sababu kwanza watapata bei ya uhakika. Wanunuzi wapo, masoko yapo na mifumo ambayo ni rahisi zaidi ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko lingine limezungumzwa juu ya leseni ya Peak Resource. Peak Resource wako Ngwara na Mheshimiwa Mulugo pamoja na Mheshimiwa Neema wanalizungumza kila wakati. Ni kweli kwamba tuliwahi kuwaalika kwa ajili ya kwenda kufanya signing. Tulivyofika siku ya signing wenzetu wakataka tubadilishe kipengele kimoja kwenye mkataba na kipengele ambacho tulikuwa tunabishania ni kimoja tu, kwamba uchimbe hapa uongeze thamani ya madini hayo hapa nchini. Wao wakawa wanataka wachimbe hapa wakaongeze thamani na tayari walishanunua eneo la kujenga hicho kiwanda London. Tukakubaliana Hapana, tunahitaji hicho kiwanda kijengwe hapa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, imetuchukua muda, baadaye tumekubaliana. Naomba niwape taarifa watu wa Ngwara, Mheshimiwa Neema na Mheshimiwa Mulugo. Habari njema tuliyonayo ni kwamba timu ya majadiliano imemaliza hiyo kazi, mikataba hiyo sasa iko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya vetting na muda siyo mrefu tutafanya ceremony ya signing kwa ajili ya mkataba huo wa rare-earth element.

NAIBU SPIKA: Haya Mheshimiwa Waziri malizia sekunde 10.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nataka nimalizie tu lile la STAMICO na kuwasaidia wachimbaji wadogo. Ni kweli amesema Mheshimiwa Manyinyi, wachimbaji wetu wadogo wameongeza tija kubwa sana kwenye uzalishaji. Wametoka kwenye 4% ya mapato yote tunayopata mpaka 40%. Tumeamua kuwasaidia kwa kuwanunulia mitambo kwa ajili ya kuwafanyia utafiti kwenye maeneo yao na kuwapatia leseni ili waweze kuchimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuwashukuru Kamati na kwa kweli tutaendelea kuwapa ushirikiano na tunaomba Kamati waendelee kutupa ushirikiano ili tuweze kusukuma sekta yetu hii mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.