Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Taarifa hizi za Kamati hasa katika Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini. Nianze kwa kuwapongeza Kamati kuanzia Mwenyekiti, Mheshimiwa Kitandula, Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Gulamali na Wajumbe wote kwa kweli kwa kazi nzuri na taarifa nzuri waliyoitoa, lakini vile vile kwa siku zote kuwa makini katika kushauriana na sisi na kusaidiana katika kupeleka mambo mbele yanayohusu sekta yetu na taarifa yao kama alivyosema Mheshimiwa Dotto Biteko, inadhihirisha umahiri, umakini na weledi iliyonayo Kamati katika kushughulikia mambo ambayo wanashughulika nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nami ni mchangiaji siyo mjibuji wa hoja na napenda
nitambue mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Manyinyi, Mheshimiwa Nusrat, Mheshimiwa Tabasam, Mheshimiwa Iddi Kasim, Mheshimiwa Genzabuke na Mheshimiwa Issaay na niseme yale ambayo wameyaelekeza kwetu kama Wizara, basi tutayachukua na kuyafanyia kazi. Kwa kuwa muda hautoshi kuyazungumzia yote lakini niseme tu nimeyapokea, nimeyaandika na tutayashughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda haraka haraka tu kuhusu REA nafahamu ni kweli kuna malalamiko mengi na changamoto nyingi kuhusu ucheleweshaji wa Miradi ya REA. Naomba nitoe faraja kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wa Tanzania kwamba baada ya kubaini changamoto zilizopo tumebadilisha utaratibu sasa wa manunuzi, usimamiaji, ufuatiliaji na tathmini ya miradi hii. Kuanzia sasa kwa mfano, vigezo vya mkandarasi kupata mradi vitakuwa tofauti kwamba mkandarasi hawezi kupata mradi mpaka alionao walau amefikia 60%.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutakuwa na pre- qualification kama Kamati ilivyopendekeza kwamba kutakuwa na kundi la wakandarasi mahiri ambao watakuwa wamepitia vigezo na kazi zitakuwepo, atakayemaliza haraka ndiyo atapata kazi nyingine haraka. Hii itatoa incentive kwa wakandarasi kufanya kazi haraka. Sasa hivi haijalishi kama una kasi au huna kasi, unaingia kwenye tenda, unapata kazi nyingine. Kwa hiyo matokeo yake ni kwamba wakandarasi wamejilimbikizia kazi kwenye eneo letu la REA lakini kwa sababu ni wakandarasi wako kwenye madaraja na kwingineko, kwa hiyo unakuta wana kazi nyingi kuliko uwezo wa kuzifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia taarifa nyingine kwa Kamati ni kwamba rasmi sasa REA tumeajiri vijana 136 ambao kazi yao itakuwa ni usimamizi wa Miradi ya REA tu katika majimbo ya Waheshimiwa Wabunge. Hawa watakuwa hawana kazi nyingine zaidi ya kufuatilia na kuripoti kwa Wabunge na Serikalini kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa miradi hii. Hawa watakuwa ni kiungo muhimu kati yetu sisi Wizarani, REA, TANESCO na viongozi wa kisiasa ili wakati wote tuwe katika ukurasa mmoja kuhusu changamoto zilizopo na tuweze kusaidiana kuzimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwenye Miradi ya Ujazilizi; hata tutakapomaliza kupeleka umeme kugusa vijiji vyote, bado kutakuwa na vitongoji vingi vitakuwa havina umeme. Kwa mfano, kwenye vijiji sasa hivi tuko 80% lakini kwenye vitongoji tuko 44%. Kwa hiyo utaona jinsi gani kufikia vijiji tafsiri yake siyo kupeleka umeme kwa watu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali tumeamua kuja na mpango mkubwa wa kupeleka umeme katika vitongoji vyote ambao tutaufanya ndani ya miaka mitano. Ilikuwa tuanze mwaka wa fedha uliopita 2021/2022, tulipata changamoto kwa sababu ni fedha nyingi. Tutakuja wakati wa bajeti kuwaomba mtusaidie Waheshimiwa Wabunge kupitisha mpango huo kabambe na ambao utatekelezwa kwa namna tofauti kama inavyotekelezwa miradi ya sasa, kwani kwa sasa hivi ina changamoto. Kwa hiyo, mradi huu sasa utajibu maswali mengi ya ujazilizi kwa sababu utafikisha umeme katika maeneo yetu mengine yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie shilingi 27,000 na shilingi 300,000, niseme tu taarifa imekuja kwetu na kwa sababu ya muda, tunaishughulikia na tutatoa mwongozo maalum wa namna ya kulifanya jambo hili. Jambo ambalo nilitaka Waheshimiwa Wabunge walifahamu, ni kwamba, gharama halisi ya kumwingizia mtu umeme kwenye nyumba yake ni shilingi 426,000 mpaka shilingi 800,000. Kwa hiyo, shilingi 27,000 ni chini sana ya gharama halisi. Shilingi 331,000 bado iko chini sana ya gharama halisi. Kwa hiyo, Serikali inatoa subsidy kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapotoa shilingi 27,000 maana yake Serikali kupitia TANESCO inatoa ile ya ziada. Hii pesa inatoka katika shughuli nyingine za maendeleo ambazo tulikuwa tuzifanye. Kwa hiyo, ni muhimu tunapotaka hizi bei tujue gharama yake, na sisi tutakuja na mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umeme kukatika, niseme tu kwamba tunafahamu na tunakiri changamoto bado ipo. Ambacho nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kwamba hivi tunavyoongea tunayo mipango madhubuti ya kuifumua grid nzima na kuirekebisha. Kwa sababu changamoto kubwa iliyokuwepo ni miundombinu chakavu. Hili jambo ukubali ukatae, ndiyo ukweli kwamba miundombinu yetu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ilikuwa haitoshelezi mahitaji na haijafanyiwa marekebisho muda mrefu. Tarehe 15 Februari tutasaini mradi unaitwa Gridi Imara, ni miradi 26 ya takribani shilingi trilioni moja ku-stabilize grid yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tutawaalika mshiriki kwa sababu ni jambo ambalo litaenda kuanza safari ya kumaliza changamoto ya miundombinu, na uzalishaji wa umeme tunaongeza ili tusiwe na gap.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Julius Nyerere unaenda vizuri, tunashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamefika na wameona na wametushauri kuhusu namna ya kwenda vizuri. Ni kweli kulikuwa na changamoto ya transmission line, miundombinu ya kutoa umeme kule kuusambaza kuingiza kwenye grid. Mradi huu ulianza kutekelezwa Desemba 2018, lakini tulisaini njia za kutoa umeme pale Septemba, 2021 miaka mitatu, kulikuwa na gap. Ila tumeharakisha mpaka sasa kufikia asilimia 80, siyo jambo dogo. Kwa hiyo, mradi wa uzalishaji umeme utaisha pamoja na mradi wa kutoa umeme kwenye eneo lile na kuusambaza kwenye gridi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya mafuta ya Mheshimiwa Tabasam tumeyapokea. Kama mnavyofahamu, hivi juzi juzi Serikali ilisaini mkataba wa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kupakua na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Sekunde 30 malizia.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane kukubali mapendekezo ya Kamati na kuyaunga mkono na kuendelea kuahidi ushirikiano wa Wizara, Bunge na Kamati ya Bunge kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.