Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye moja ya hoja iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Bajeti. Nikitambua mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, naona nichangie katika kipengele kimoja tu kwenye ukurasa wa 50 wa ripoti ya Mwenyekiti au ripoti yetu kwenye eneo la mikopo hii ambayo sisi kama nchi tunaifurahia jinsi gani Rais wetu anaipambania. Kabla ya kufanya hivyo, nitumie nafasi hii sana kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoendelea kufanya kazi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mikopo ambayo imezungumzwa katika ripoti yetu kuna huu mkopo wa (ECF- Extended Credit Facility) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa IFM wa Dola za Kimarekani Bilioni 1.04 au sawa na Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.4. Kuna shida, Kamati inasema ina shaka juu ya malengo kama yanafikiwa, labda niwapitishe lengo kubwa kwenye mkopo huu wa trilioni 2.4 ambalo ni dirisha la pili na niwakumbushe ni dirisha la pili ambao tumepata, tofauti na lile dirisha la kwanza ambalo tulipata zile (RCF - Rapid Credit Facility) au UVIKO 19 hizi fedha ni 2.4 trillion. Fedha hizi tulizichukua kwa sababu ya lengo, lengo kubwa lilikuwa ni kupunguza urali kwa ujumla, urali wa nchi yetu katika yale ambayo tunaweza badala ya ku-import, tukaweza kuzalisha ndani na tofauti na hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kinachotokea ni changamoto kubwa sana. Ukiangalia ufanisi wa Mkopo huu mpaka sasa mkopo huu umetolewa mwezi Agosti ambao unatakiwa katika masharti yake utatolewa kwa awamu saba kwa vipindi vya miezi arobaini, lakini mpaka sasa ambapo ni dirisha linakuja mwezi wa Tatu mwakani kwa maana ya baada ya tathmini, lakini taasisi zote hizo ambazo zimepewa au maeneo yote ya kipaumbele matano, eneo la kilimo, uvuvi, nishati maji, nishati umeme, bado hakuna hata moja lililofika asilimia 30. Hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tunategemea Shilingi bilioni 760, tunaambiwa kwenye Kamati ndiyo tunatarajia tupewe ndani ya mwaka mmoja na tumepewa kwa awamu mbili; ya kwanza shilingi bilioni 349, sasa hivi tulitarajia kabla hao Wazungu hawajaja kutufanyia tathmini ili watupe second tranche, maana yake tulitakiwa tufike hata asilimia 60 au 70 sasa tuko chini ya asilimia 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakutajia kwa uchache. Eneo la kilimo, ECF kilimo, wametumia asilimia 28. Yaani fedha waliyopangiwa ni shilingi bilioni 40 wamepata shilingi bilioni 11; eneo la uvuvi, Fungu 64 katika bajeti ya shilingi bilioni 60 wamepata shilingi bilioni 1.1, yaani asilimia 1.9. Eneo lingine kama kilimo katika vipaumbele vitano wamefanya vitatu tu na vyote chini ya asilimia 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuonesha nini? Kama tumewapa kilimo eneo la umwagiliaji katika Fungu 5, shilingi bilioni 215, wamepewa chini ya shilingi bilioni 42. Sasa tunataka kujiuliza, hawa jamaa wakija kutufanyia tathmini ili tupate second tranche tutaweza kufanikiwa? Swali lingine unajiuliza, hivi mama anavyoenda kupata haya madirisha, anaenda anakutananayo kwa bahati mbaya au tayari wataalamu mnakua mnasema tunahitaji jambo fulani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani hela inapatikana ndiyo mnaanza kujipanga katika ofisi zenu. Maana kama nchi lazima tujue sasa, shida ni nani? Shida ni nyie wasimamizi, makamisaa wetu katika Wizara? Shida ni nini? Manunuzi? Shida ni nini? Kwa nini hatusogei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe kwa haraka, inawezekana hii ni tabia. Tunaambiwa palikuwa na dirisha la kwanza la RCF au UVICO 19, tuliambiwa mambo mengi sana. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Watanzania wanajua ni ile shilingi bilioni 600 na kitu ambayo ilienda kujengea madarasa 15,000 yakiwepo 12,000 na 3,000 ya shikizi. Mambo mazuri yalionekana pale, lakini hela nyingine ziko wapi? Mambo mengine ni yapi? Tunaona moja moja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa, nataka niwakumbushe; na ndiyo maana hatutekelezi hii mikopo tunayopewa. Tuliambiwa tungeweza kuwa; hela iliyoenda afya Shilingi milioni 263, tena afya kwa upande wa Wizara, nyingine zilienda TAMISEMI, lakini lengo lake lilikuwa ni kununuliwa magari 503. Yako wapi? Ndani ya magari hayo; Land Cruiser Hard Top 262, basic ambulance 373, advance ambulance 20, ziko wapi? Ndiyo maana nazungumzia malengo ya mikopo yetu, ni kweli toka mwezi Juni, 2022 tuliambiwa yangeanza kuja magari hapa ambulance, mpaka leo hakuna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dirisha la pili hili tunaendeleanalo. Changamoto za utendaji kazi chini ya asilimia 30. Rais wetu, mama yetu, ataenda atakutana na dirisha la tatu, mtamwingiza chaka tena achukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe. Tuna shida kama Taifa. Katika bajeti zetu za Serikali za kila mwaka, bajeti ya 2022/2023 ni ya shilingi bilioni 41 tumesema hapa, lakini fedha za maendeleo zinazowekwa ni takribani shilingi trilioni 15.1. Kama shilingi trilioni 15.1 tunaendelea kufurahia Shilingi trilioni 1.3, RCF tunafurahia shilingi trilioni 2.4 tena tunazifurahia, na ni kweli, ni vizuri na tunazifuatilia, kwa nini hatufuatilii shilingi trilioni 15 zile za maendeleo katika kila mwaka, kwanini hatuzifuatilii? Katika kipindi cha miaka mitano, maana yake ni zaidi ya shilingi trilioni 60. Kama nchi tumeziweka katika maendeleo, lakini hakuna follow up. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida. Tumesema hapa kwenye Kamati, shida ya Sheria ya M&E, tuliomba sera ije hapa tutunge sheria ya monitoring and evaluation ingeweza kutusaidia kama nchi kuweza kufuatilia fedha zetu nyingi zinazoshuka chini. Leo shida yetu tunafurahia mikopo, nami naifurahia, mama yangu anaitafuta, lakini zile hela zetu tunazoziweka katika maendeleo, zetu wenyewe Shilingi milioni 14 hadi 15 mbona hatuzifuatilii na zinapotea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tungeweza kuweka ring fence kwenye hela fulani tukawapelekea TARURA wenye kilometa 144,000 mtandao wa barabara. Wote hapa tunajua, tuna barabara za vumbi tunatamani ziwe changarawe au lami, kwa nini tusipeleke fedha nyingi tukazitolee macho kwenye barabara zetu za ndani za TARURA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Taifa, lazima tujitathmini sana. Mikopo tunaitaka, lakini vilevile na fedha zetu za ndani za maendeleo tuzitolee macho kwa kutungiwa sheria. Ije hapa sera, tutunge sheria ya monitoring and evaluation ili tusimamie fedha zetu zote zinazoshuka chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)