Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie nikiwa mchangiaji wa mwisho na ninajua mara nyingi mchangiaji wa mwisho hutampigia kengele utamuachia tu atiririke wee! mpaka amalize. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na ningependa nizungumzie masuala ambayo yamewasilishwa na Mwenyekiti wetu, haraka niseme naunga mkono hoja zote mbili kwamba mimi kwangu ni asilimia mia moja kwa mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mpenzi wa kusoma sana hizi Journals za mambo ya kiuchumi, hivi karibuni nikasoma jarida moja linaitwa Africa can end poverty wakiwa na maana kwamba Afrika inaweza ikaondokana na umaskini, pale nikavutiwa na andiko moja la Ndugu mmoja anaitwa Waly Wane huyu ni Daktari wa Uchumi katika taasisi moja inaitwa Development Research Group. Huyu aliandika akajiuliza swali is Tanzania raising enough tax revenue? Alikuwa anajiuliza yeye katika thesis aliyokuwa anaandika kwamba hivi Tanzania inakusanya kweli kwa uhakikia kodi inayotosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni andiko la siku nyingi kidogo la tarehe 4 Februari, 2013. Sasa katika kusoma kwangu nikasema ngoja nifananishe na hali halisi hapa kwetu. Nichukue kwanza nafasi kusema kweli ya kuipongeza Serikali kwa maana ya TRA kwa maana mwaka 2021/2022 mapato ya ndani Serikali imeweza kukusanya trilioni 24.35 dhidi ya lengo la trilioni 25.6 na hii ni sawa na asilimia 95 Kamati imetoa pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi na juhudi kubwa iliyofanywa hawa akina Ndugu Waly Wane swali lao bado halijajibiwa. Nimejaribu kuangalia pia mapato yetu na mienendo ya jinsi tunavyofanya mipango yetu swali la Waly Wane bado halijajibiwa. Sasa nikasema hebu niangalie Kamati imeliangalia vipi suala hili, kwa mujibu wa maelezo ya Kamati kama ilivyo katika paragraph 2.1.7 kuanzia ukurasa wa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui nilijibu hili swali ama Bunge litajibu lakini tusikilize Kamati inasema nini, na maneno haya aliyasema hata Mheshimiwa Esther, kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hawatumii machine za EFD, maana yake ni kwamba kuna upotevu hatukusanyi, kumbe sasa swali la Ndugu Waly Wane tunaanza kuliona kwamba kweli alivyouliza ni kwamba kweli hatukusanyi inavyopasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie jambo la pili baadhi ya Halmashauri zetu haziwasilishi fedha benki, hizo fedha zinakwenda wapi kama haziwasilishwi benki maana yake zinapotea, hazikusanywi na Serikali maana yake jibu ni kwamba hatuzikusanyi Serikali haipati mapato yake. Hata ukija kwenye masuala ya fedha ambazo hazikusanywi kutokana na madeni ambayo yamelimbikizwa, hilo nalo ni suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye idadi ya watu ambao wameandikishwa walipa kodi, watu Milioni Nne ndiyo wako katika kanzi data, watu wanaolipa ni nusu yao maana yake hata Mheshimiwa Esther aliuliza je, kama hao wengine Milioni Mbili waliobaki wangekuwa wanalipa tungekuwa tunapata kiasi gani? Hilo nalo ni swali la Ndugu Waly Wane anauliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye masuala mengine ya watu wanao file returns - marejesho ya kodi kwa njia ya ki- electronic, wapo watu ambao wameonekana hawafanyi hivyo maana yake hatuzikusanyi fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tax audit ambazo zinachelewa, hili tumelisema hapa Bungeni, inachukua miaka mitatu, minne kwa TRA kwenda kufanya tax audit, fedha za Serikali zimekaa pale hatuzikusanyi, na hilo nalo ni suala vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kuanzishwa kwa Ofisi ya Msuluhishi wa Kodi ambapo pengine masuala ya Kikodi yasingekwenda TRAB na TRAT kule yangeweza kusuluhishwa lakini bado haijamalizika. Hata haya mashauri yaliko katika hizi mahakama za TRAB na TRAT hazina muda. Zinaweza zikakaa muda wote ule, hakuna specific period kwamba ikifika muda fulani mashauri yamalizike, Serikali ipate fedha zake au mfanyabiashara arudishiwe fedha zake. Haya ni mambo ambayo tungependa tuyaone kwamba ni concern kubwa kwamba ni vitu vinavyotugusa. Kwamba laiti kama vitu hivi vitafanyika kwamba ni dhahiri kabisa inaweza tukapata fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie kule Mtaa wa Nyamwezi pale Dar Es Salaam, ambao umejaa maduka mengi sana. Pale wale Maafisa wa Kodi ambao wanasimia ile block wapo Maafisa Watano tu na mtaa ule mpaka wakiumaliza kuutembelea maana yake watahitaji hata mwaka mzima. Yawezekana kuna wafanyabiashara wengine hata hawapitiwi kabisa kuweza kupeleka taarifa zo za kikodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ni kisema hivyo maana yake kilio cha kupatikana kwa wafanyakazi wa kutosha wa TRA bado kiko pale pale, tusipokuwa na wafanyakazi wa kutosha TRA hatuwezi tukakusanya ela. Najua Serikali imejitahidi sana kuongeza idadi ya Wafanyakazi wa TRA lakini hakika hiyo inaanifanya nifikirie jambo moja. Kule kwenye Kata zetu, kila kata kuna Afisa Maendeleo, kila kata kuna Afisa Ugani, Kuna Afisa Elimu tunashindwa nini kuweka kila kata Afisa wa kodi. Tunaona taabu ya nini tuanze na Dar es Salaam tuangalie yale maeneo ambayo yanashughuli za kiuchumi nyingi ili tuweze kuwakia wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya anasema maneno haya ni very famous anasema kama huwezi kuliwa huwezi kula, ukitaka kula lazima uliwe, sasa sisi tena hawali watu wabaya wanakula watu wetu, Watanzania wakiajiriwa watatusaidia kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,hili linanipeleka vilevile kwenye utaratibu mwingine, naomba Serikali iweke katika mitaala yake hata kuanzia primary school, somo la uzalendo na ulipaji wa kodi. Watu wetu wakue wakiwa wanajua umuhimu wa uzalendo na umuhimu wa kulipa kodi. Hii pia itatusaidia kwa sababu kama tunatafuta fedha za kutosha na huku tunajua fedha za kutosha zinatoka katika private sectors, private sector kwa maana ni biashara, leo kulikuwa na swali linaulizwa hapa linahusiana na blueprint tuko nchi ya 141 na hili nalisema sana mwisho nitapewa jina la blueprint. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko 141 Serikali inaulizwa lini mtatuletea taarifa ya utekelezaji, majibu yanayoletwa hapa yaani saa nyingine tunaheshimu Serikali yetu lakini saa nyingine unashangaa unaweza ukasema ni ya kisiasa mno! Tunataka taarifa zile za kufanya ufanyaji wa biashara Tanzania uwe mwepesi, watu waweze kutupatia kodi, sasa hilo pia nalo lina ugumu gani? Haya mambo mengine unayazungumza na mimi kwa sababu hili eneo la fedha ni la Ndugu yangu Mwigulu, najua ni mwananchi mwenzangu, yaani najizuia kwelikweli kutumia maneno mengine yasiyofaa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba nilikuongeza dakika kidogo lakini nadhani tumefika mwisho.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Haya ahsante.

MWENYEKITI: Nakushukuru kwa mchango wako.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)