Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti lakini nachukua nafasi hii kwanza kupongeza Kamati zote Mbili zilizowasilisha leo kwa kazi nzuri ambazo zimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa kweli jioni hii ningependa nishauri katika maeneo Manne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni eneo la mitaji katika sekta ya kilimo. Kumekuwa na kiu ya muda mrefu hasakwa sekta binafsi ambazo zinahitaji zipate mitaji kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo, hasa vijijini. Tatizo kubwa kwa nini wamekuwa hawapati mitaji wanayohitaji, ni kwa sababu Sheria zetu za Ardhi Sheria Namba 4 na Sheria Namba 5 zinazuia uwezekano wa watu kutumia kama dhamana vijijini kwa ajili ya kupata mitaji; hasa kutoka kwenye benki. Hii ni kwa sababu, ardhi haijapimwa. Hata hivyo hili nimekuwa naisema mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tupitishe Sheria ya Vijiji Namba 5 mwaka 1999, Mpango ulifuata ulikuwa ni mkakati wa kutekeleza Sheria za Ardhi ambao ulianza kutekelezwa Mwaka 2000. Hata hivyo Mpango ule au Mkakati ule ulikuwa na miaka mitano. Walikuwa wamesema kwamba ndani ya miaka mitano vijiji vyote vitakuwa na mipango ya matumizi ya ardhi. Hata hivyo hadi leo hii tunavyozungumza hapa vijiji ambayo vina mipango ya matumizi bora ya ardhi ni vijiji 2,310. Ina maana kuna vijiji 10,000 havina mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu katika Wilaya ya Sikonge vijiji ambavyo vina mipango ya matumizi bora ya ardhi ni vijiji tisa tu kati ya vijiji 71. Maana yake ni kwamba tumekuwa tunazuia uwezekano wa kupata mitaji kutoka kwenye sekta ya ardhi kwa sababu ya sheria zetu. Nilikuwa natoa wito kwa Serikali, naomba Serikali ije na mkakati maalumu wa aidha kupima vijiji vyote, kwa sababu wastani wa kupima kimoja ni milioni 15 hadi 20; kwanini wasipange wakapima vijiji vyote kwa awamu mbili au tatu wakamaliza ili kusudi watu wetu wawe wanapata mitaji kutoka kwenye sekta ya ardhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo ningependa kushauri ni mfuatano wa mipango kwenye sekta ya miundombinu. Sasa tunajenga SGR, tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere na naipongeza Serikali SGR ya Tanzania hata watu wa nje wakija wanaona Kiwango, yaani standard ya SGR ya Tanzania inaizidi kwa mbali kiwango cha SGR za nchi Jirani, kwa hiyo, hiyo naipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mfuatano na hasa kwa sababu tunadhani kwamba mpaka ikifika mwaka 2030 tutakuwa tumemaliza vipande vyote vya SGR, kama Mungu atatuwezesha. Hiyo hiyo itakuwa ni muda mfupi wa kutumia kuliko walivyotumia wenzetu walivyokuwa wanajenga miaka ile ya wakati wa Ukoloni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano, ujenzi wa reli ya kwanza nchini hapa kutoka Tanga mpaka Arusha ulitumia muda wa miaka 36. Kwa maana ya kipande cha kutoka Tanga mpaka Moshi ni miaka 18 na Kipande cha Kutoka Moshi Mpaka Arusha ni Miaka 18. Hata hivyo kama tutaweza sisi kujenga SGR vipande vyote kwa muda wa miaka 13 au 15 itakuwa ni achievement ambayo ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye mfuatano, wenzetu wakoloni katika utawala wao wa miaka 71 mfuatano wao ulikuwa unajulikana. Walianza na Tanga – Moshi – Arusha, wakaja Dar es salaam – Tabora – Kigoma, wakaja na Tabora – Mwanza, wakaja na kaliua – Mpanda halafu wakajenga vireli vya kuunganisha. Kilosa – Mikumi, Manyoni – Singida, Mtwara – Nachingwea, Ruo- - Chilungura hadi Masasi, Msagali – Kongwa, Murwazi hadi Ruvu kuunganisha Reli ya Kati na Reli ya Tanga; na hiyo ndiyo iliyokuwa ya Mwisho ya Tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa baadaye baada ya uhuru baadhi ya reli tulizing’oa kwa sababu mbalimbali; lakini wenzetu walikuwa na mfuatano mzuri. Hata hivyo kwenye mfuatano huo baada ya uhuru walikuwa wanataka kuendelea kujenga reli mbili. Kulikuwa na Reli kutoka Arusha – Ufyome - Mbulu Kupitia Kondoa hadi Dodoma. Je, kama wakoloni walikuwa na mpango huo je, sisi baada ya kupata uhuru tuliona kwamba haufai tukaamua kuuacha kabisa? au tuna mpango gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kulikuwa na Reli nyingine ya kutoka Arusha kupita Mount Kilimajaro Magharibi mpaka Jado Kenya kwa ajili ya kuunganishe na ile Reli ya Kenya Kwenda Uganda, nayo hivyo hivyo baada ya Uuuru tuliiacha. Je, kwenye mipango ya sasa hivi tunaona kwamba hizo Reli bado hazifai au namna gani kwenye mfuatano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni kuhusu Tume ya Mipango. Tume ya Mipango ni Tume muhimu sana kuwepo ndani ya Serikali. Tulifanya kosa kuiondoa. Sasa mimi naomba Serikali ije na mkakati mzuri wa namna gani Tume ya Mipango i-operate ndani ya nchi ili itusaidie kuratibu mipango yote na itusaidie kwenye eneo la ufuatiliaji na tathmini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ningependa kushauri Serikali ni kuhusu wakandarasi. Wakandarasi wetu tumekuwa hatuwapi jukumu la uwajibikaji kwenye viwango (standards). Katika nchi nyingine kama Malaysia wana taasisi mbili ambazo zinasimamia kwa mfano barabara wana taasisi mbili tu. Taasisi ya kwanza ni taasisi ambayo inatafuta fedha za barabara. Hiyo taasisi ndiyo inayoingia Mkataba wa ujenzi. Halafu taasisi ya pili ni ile ambayo inasimamia viwango, quality control. Yaani anaingia Mkataba huku akienda huku anasimamiwa na quality controller ambaye anasaini naye mkataba mwingine unaitwa quality covenant. Kwa hiyo, yule Mkandarasi anakuwa amepewa wajibu wa kuhakikisha kwamba ile barabara anayoijenga quality ni wajibu wake. Akijenga quality mbaya yeye atalipa in full. Sasa sisi tumekuwa hatuwapi wajibu wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa napenda kushauri, wataalamu wetu wananisikia huko, wahakikishe kwamba waende hata Malaysia wakajifunze jamaa zetu wanavyofanya kule namna ya kusimamia ile quality control ili uwe wajibu wa Mkandarasi kuhakikisha kwamba ana-deliver kitu ambacho kina kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa mkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, ahasante sana.