Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo nami kuchangia taarifa za Kamati zetu mbili zilizowasilishwa. Naunga mkono Kamati zote na kupongeza kazi nzuri iliyofanywa. Mchango wangu utajielekeza kwenye Kamati yetu ya Bajeti ambayo mimi pia ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze alipomalizia Mheshimiwa Mpina wakati wa mchango wake akirejea jedwali Na. 2. Kwa kuwa mchango wake umekuwa ukijielekeza kuigusa Taarifa ya Kamati na Kamati nzima ya Bajeti, ninachotaka kusema ni kwamba ukiangalia jedwali Na. 2 kwenye Taarifa yetu ya Kamati ukurasa wa 10, Serikali kwa mwaka huu wa fedha ulioishia 2022 haikukopa zaidi, kwa sababu ilitarajiwa mapato na matumizi kuwa shilingi trilioni 37.99 na walifanikiwa kupata shilingi trilioni 36.924. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye mikopo ya kibiashara kutoka nje Serikali ilitarajia kukopa Shilingi trilioni tatu ikakopa Shilingi trilioni 1.8 ikaziba nakisi kwenye mikopo ya kibiashara ya ndani. Kwa hiyo, imefanya tu ku- offset. Kwa hiyo, hakukuwa na changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ni kuhusu matumizi nje ya bajeti. Sheria ya Bajeti ya Kifungu Na. 43 kinaipa mamlaka Serikali kuwasilisha taarifa hiyo Bungeni, lakini kwa kuwa mwaka wa fedha unaendelea ndiyo kwanza miezi sita, ninaamini kama kuna matumizi yaliyofanywa nje ya vifungu vilivyoidhinishwa na Bunge, bado ipo fursa Bunge hili hili kufanya mchakato utakaowasilishwa na kujadiliwa. Kwa hiyo, hakuna dhambi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine utajielekeza kwenye masuala mazima ya mapato na matumizi ya Serikali. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inaendelea vizuri kwenye makusanyo ya mapato. Tumeona namna gani Serikali ikijitahidi. Nataka niseme katika mapato ya ndani ambayo yalikusanywa kwenye mwaka wa fedha ulioshia Juni, 2022 zaidi ya Shilingi trilioni 24, kati ya trilioni 25, asilimia 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhamana inayotumika kulipia mishahara shilingi trilioni nane, kulipia deni la nje ambalo halijakopwa sasa shilingi trilioni nane, matumizi mengineyo Shilingi trilioni tano, unaona kama Serikali isingefanya maarifa mengine, fedha kwenye miradi ya maendeleo isingewezekana. Ninaposimama hapa, naipongeza Serikali kwa kupeleka zaidi ya shilingi trilioni 11 kutoka kwenye mapato ya ndani shilingi trilioni 11.55 kati ya shilingi trilioni 11.59, asilimia 99 kwa mara ya kwanza kwenye miradi mbali mbali na tumeiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, kulikuwa na hoja hapa, kwa kuwa Serikali labda ililipa SYMBION shilingi bilioni 356 pengine imechangia mfumuko wa bei, sikatai. ila je, hizi shilingi trilioni 11 zinazoenda kuchochea miradi ya maendeleo zinazowafikia wakandarasi wa kawaida, zinazosababisha ajira wa mafundi mchundo, kwa akina mama ntilie, zina mchango gani? Ni wazi kwamba pamoja na changamoto ya mfumuko wa bei lakini kama Serikali isingepeleka fedha nyingi za kutosha kutekeleza shughuli mbalimbali, ninaamini hali ingekuwa mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasimama kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kupambana na mfumuko wa bei, lakini imejielekeza kutekeleza miradi na wananchi wetu kupitia hiyo miradi wanapata pesa ambazo wanaweza kununua bidhaa ambazo bei yake imepanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeona jitihada kupitia ruzuku ya mbolea. Wametenga shilingi bilioni 150, lakini mpaka sasa hivi shilingi bilioni 190 zimetumika. Napenda kuthibitisha, mimi nimeona Mkoa wa Pwani mbolea ya ruzuku wananchi wakiipata na wakifurahi na wakiipongeza Serikali. Hiyo yote ni kushusha bei. Leo wananchi wanapata mbolea kwa nusu ya bei iliyokuwepo, yote hii ni mikakati ya kushusha bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kufufua Kampuni ya Mbolea Tanzania na kuipatia mtaji ambayo imenunua mbolea na imeanza kusambazwa tarehe 25. Maana yake hata wale wafanyabiashara, waingizaji wa mbolea nchini watakapoona bei imeshuka kwenye Kampuni ya Serikali watashusha bei wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali sasa, hebu waangalie kwenye muktadha mzima wa chakula, hawawezi kuiitumia Bodi ya Mazao Mchanganyiko, nao wakanunua vyakula wakauza ili iweze kuchochea ushindani na kuweza kupunguza bei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaipongeza sana Serikali kwa mpango huo na kwa ruzuku inayoendelea kwenye mafuta. Ninaona dhamira njema ya kushughulikia mfumuko wa bei nchini kutokana na kazi mbalimbali wanazofanya. Sambamba na hilo, katika mwaka wa fedha unaoendelea Serikali iliondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye malighafi ya mbegu zinazozalisha mafuta hapa nchini na faida yake tumeona. Sasa hivi mafuta ya kula ya lita tano yanayozalishwa hapa nchini ni shilingi 27,000/= kutoka shilingi 35,000/= au shilingi 45,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, kwa niaba ya wanawake, watumiaji wa mafuta ya kula kwa hatua hizo. Niendelee kuwatia moyo waendelee kupambana kubuni, na Wabunge ndio washauri wa Serikali, tuisimamie Serikali, lakini sisi tutakapokuwa wa mfano kukataa kwa sababu ambazo ziko wazi, dunia nzima inasema Vita vya Ukraine na Urusi vimesababisha hali ngumu ya uchumi, sisi nani tukatae? Dunia nzima inashuhudia ukame, nchi yetu haijapata mvua misimu miwili, chakula kimezalishwa kidogo, kwa nini tukatae sababu za namna hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ijikite kwenye matumizi ya mkopo wa shilingi trilioni 2.4, huu unaoendelea sasa, kwenye sekta ya kilimo, sekta ya uvuvi, sekta ya nishati na sekta ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati tumetoa mapendekezo mengi lakini dhima ya mkopo huu ni kuwezesha, kuzalisha mazao kuongeza mauzo nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni. Kuzalisha mazao ambayo yangeweza kuzalishwa hapa nchini tuache kuagiza nje ya nchi. Kwa hiyo, niwaombe Wizara zinazohusika mpaka sasa kama tulivyosema kwenye Kamati, mkipambana na mkopo huu ambao hauna riba, una grace period ya miaka mitano na nimpongeze na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya, inaweza ikasaidia kushusha mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii, naunga mkono hoja.(Makofi)