Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Nianze kwa kuipongeza na kuishukuru sana Kamati yetu ya Mambo Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Vita Kawawa na Wajumbe wote kwa ushirikiano mzuri ambao wanaendelea kutupa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona leo umesoma mabadiliko ya Waheshimiwa Wabunge kwenye Kamati, matarajio yangu Wajumbe wa Kamati hii wataendelea kuomba kubakia hapa kwa sababu tutawa-miss sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie mambo kama matatu mpaka manne kwa harakaharaka. La kwanza ni suala ambalo Waheshimiwa Wabunge, wengi wamelizungumzia kuhusu changamoto ya msongamano wa Wafungwa Magerezani na Mahabusu, ambapo mbali na maoni ya Waheshimiwa Wabunge lakini hata Kamati na yenyewe kwenye taarifa yake ililizungumza hili. Walieleza sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha jambo hili, moja katika mambo ambayo Kamati ilizungumzia ni jinsi ambavyo tuna upungufu wa Magereza nchini lakini wakaeleza vilevile masuala ya kutotumika ipasavyo kwa huduma hizi za Parole pamoja na wategemezi wa adhabu za kifungo kwa maana ya kutokutumia zile adhabu mbadala na nyingine ni hoja ya Wahamiaji haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na hizi hoja, nitachukua furasa hii kujaribu kueleza hatua ambazo Serikali tumechukua katika kukabiliana na hoja hizi ambazo ni sahihi kabisa. Mbali ya hoja hizi suala la msongamano magerezani ni pana zaidi na upana wake unatokana na hatua ambazo Serikali tumechukua kuliangalia hili, lakini kuangalia kwa ujumla wake utendaji kazi wa Vyombo vyetu vya Usalama kwa ujumla wake na ndipo tukaja na mpango kabambe wa kufanya maboresho makubwa katika vyombo hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapofanya reforms katika jambo lolote changamoto yake ni kwamba, unaweza usipate matokeo haraka, inahitaji ustahimilivu na uvumilivu katika kupata matokeo kwa sababu inahusisha tafiti mbalimbali, inahusisha vilevile marekebisho ya mifumo, marekebisho ya sheria, marekebisho ya mazoea, marekebisho ya aina mbalimbali. Kwa hiyo, naomba nitoe mfano mmoja wa hii kauli yangu ambayo nimeizungumza ya umuhimu wa kuliangalia kwa mapana yake zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama siku mbili nyuma nilipita hapa kwenye Kituo cha Police Central, Dodoma na sikuwa nimemwambia mtu yeyote kama naenda, nilipita tu nikasimama, nikaingia ndani, nikawaambia naomba nizungumze na hawa mahabusu walioko huku ndani. Kwa hiyo nikaingia kwenye mahabusu, nikajaribu kuwauliza hivi kuna mahabusu yeyote hapa anahitaji kueleza jambo lolote kwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakajitokeza waliokuwa na hoja zao mbalimbali. Mmoja ambaye nataka nimtolee mfano hapa, aliyejitokeza akalalamika kuonewa na Jeshi la Polisi. Akasema bwana mimi nimekamatwa hapa nimekaa mahabusu muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofanya utafiti baada ya kuzungumza naye na utafiti mbalimbali kuhusiana na yule mtu, niligundua yule mtu aliwahi kufungwa miaka 30 Ruvuma kwa kosa la ubakaji na alikaa miaka michache gerezani akapata msamaha. Baada ya kupata msamaha, hivi karibuni amekamatwa kwa tuhuma za kubaka watoto wa madrasa, sio mmoja, sio wawili, sio watatu, sio wanne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sio Mahakama, kuna utaratibu wake wa kuweza kutoa hukumu, lakini mazingira ya uchunguzi wangu mimi wa juu juu umenipa imani juu ya umuhimu wa yeye kuendelea kukaa mahabusu. Nina uhakika hata kama ataachiwa leo hivi, pengine akienda huko wanaweza wakamuua wale wazazi wa wale watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nini maana ya kutoa mfano huu? Maana yangu ni kwamba, hata utaratibu huu wa misamaha, utaratibu huu wa parole ambao Waheshimiwa Wabunge wanaulalamikia kwamba tunaufanya kwa kusuasua, na wenyewe unahitaji maboresho na kuangaliwa, kwamba, je, utaratibu tunaoutumia hautoi mianya kwa watu wengine ambao hawastahili kutumia fursa hizi? Kwa hiyo, pengine mambo haya ambayo tunayafanya yanasababisha kuonekana tunachelewa kutumia hizi fursa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa ni kuhusiana na wahamiaji haramu. Ni kweli, tatizo la wahamiaji haramu ni kubwa sana. Hatua ambazo tunaendanazo mpaka sasa hivi ni nzuri na za kuridhisha, kwa sababu, hivi sasa tunavyozungumza wahamiaji haramu hawa wa Ethiopia waliko gerezani wanakadiriwa kufika 2,673. Katika kipindi cha mwezi Januari na Februari tu peke yake ambapo mwezi Februari ni tarehe za mwanzo tu, tarehe 7, leo tunazungumzia wahamiaji waliorudi kwao Ethiopia kwa miezi hiyo miwili wanakadiriwa kufika 1,538.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipozungumza leo asubuhi nimewasilishiwa release orders za kusaini wahamiaji ambao wako tayari kuondoka 397, hivyo kufanya jumla ya wahamiaji haramu wa Ethiopia 1,903 ambao wanaondoka kwa miezi miwili. Sasa hii ni hatua kubwa sana. Hatua hizi zimesababishwa na nini? Kwanza ni jinsi ambavyo tumelichukulia kwa uzito tatizo hili na kuweza kutoa maamuzi ya muhimu sana. Maamuzi yenyewe ni kuhakikisha kwamba tunaiondoa nchi ya Ethiopia katika nchi ambazo zinatumia utaratibu wa Visa Rejea. Sasa tumefikia katika hatua nzuri kwa sababu tayari tumeshabadilisha kanuni na hivi sasa tunapozungumza tayari GN Namba 37 ya mwaka 2023 imeshatangazwa na hivyo basi, utaratibu wa matumizi ya Visa kwa wananchi wa Ethiopia kuja Tanzania utaendelea kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii itasaidia sana kwanza kuua hii biashara ya usafarishaji binadamu haramu. Itasaidia pia kufanya Serikali iweze kuongeza mapato kwa sababu, hawa watakuwa wanalipa Visa. Pia itaondoa ile changamoto ya kuiingiza hasara ya Serikali ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiipigia kelele. Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Bunge wamezungumza hapa juu ya takwimu kwamba, pengine kwa kipindi kifupi tu kulingana na takwimu zao tumepoteza karibu shilingi bilioni 5.6, wakashauri wahamiaji hao waondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuondoa wahamiaji haramu kwa kutumia gharama za Serikali ni changamoto kubwa. Kwa sababu tulipiga hesabu kwa hawa wahamiaji ambao nimewazungumza, elfu mbili na kitu, kama ingekuwa tumewaondoa kwa fedha ya Serikali, tungetumia takribani Shilingi bilioni tisa, ambapo kama ukijumlisha na hesabu ile ya Waheshimiwa Wabunge madawati, badala ta kupata madawati 31,000 unazungumzia madawati zaidi ya 129,000. Kwa hiyo, ndiyo maana tukatumia njia mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ambazo tumetumia, ya kwanza, tumeweza kuzungumza na washirika wa maendeleo, na wameweza kuondoa wahamiaji haramu zaidi ya 504. Sasa hivi tuna utaratibu mzuri ambapo ndugu wa hawa wahamiaji haramu wenyewe wanakuja sasa kuwaondoa ndugu zao kwa gharama zao wenyewe. Ndiyo maana sasa hivi nazungumzia jitihada hizo kwamba zinakwenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hii hoja ya kuiondoa Ethiopia kwenye utaratibu wa Visa Rejea imeweza kuleta hamasa katika nchi yao kuona kwamba, sasa hivi hakuna sababu tena ya kuweza kutumia njia ya kificho kuweza kusafiri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba nilizungumzie kwa haraka haraka…
MWENYEKITI: Haya, nakuongeza dakika moja Mheshimiwa umalizie jambo lingine.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja?
MWENYEKITI: Hitimisha ndiyo. Muda wako ulikuwa umeisha Mheshimiwa. Unaweza ukamalizia lakini jambo lako moja ambalo umelisema.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jambo ambalo nilitaka nilihitimishe kwa haraka haraka ni eneo la Jeshi la Polisi na hasa katika eneo la usalama barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili kuna mambo makubwa mawili ambayo tunafanya; la kwanza kabisa, ni kufanya reform ambayo juzi nilishuhudia jinsi Mheshimiwa Rais alivyounda tume. Ile tume pamoja na mambo mengine, inakwenda kuangalia mambo mengi; inakwenda kuangalia maslahi, utaratibu wa ajira, na vitu mbalimbali. Pia kuna vitu ambavyo tayari tumeshavianza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema lazima Jeshi la Polisi liwe la kisasa ili tudhibiti uhalifu kwa ufanisi zaidi, ili tudhibiti ajali za barabarani, ili tupunguze kero au malalamiko ya wananchi kuhusu rushwa kwenye Jeshi la Polisi na mengineyo, lazima Jeshi la Polisi liwe la kisasa. Hivyo, kwa upande wa ajali barabarani kwa mfano, kuna mambo makubwa mawili ambayo wakati wowote kuanzia sasa tunaweza kuanzanayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni kwamba, tunaanza hivi karibuni kutangaza utaratibu wa kuweza kufanya ukaguzi wa lazima wa magari. Kwa hiyo, naomba kuchukua fursa hii kutoa wito kwa taasisi ama kampuni yoyote duniani ambayo inajihisi inaweza kuja kushirikiana na Serikali. Maana mambo haya yote ya modernization ya Jeshi la Polisi na majeshi mengine, hatuwezi kuyafanya kwa kutegemea bajeti ya Serikali peke yake. Kwa hiyo, kuna utaratibu ambao tunaweza tukashirikisha taasisi binafsi kwa ajili ya kwenda kukabiliananayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni jambo jema kabisa, ni kitu muhimu sana kuweza kuwa na mifumo ambayo itasaidia Jeshi letu la Polisi kuweza kubaini makosa ya uhalifu kwa haraka, ikiwemo makosa ya jinai, makosa ya ajali barabarani na mengineyo. Kwa hiyo, hatuwezi kuepuka katika karne ya leo kuwa na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kamera.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna mpango vilevile katika muda siyo mrefu kuanza utaratibu wa kuwa na mifumo ya miji salama katika nchi hii. Haya mambo niliyazungumza katika bajeti iliyosomwa mwaka uliopita 2021/2022 na katika utekelezaji wake tumefikia katika hatua ya kuridhisha. Tutaanza na Mji wa Dodoma, Mji wa Dar es Salaam, Mji wa Arusha na baadaye tutaelekea na miji mingine mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna hoja nyingine ya vitendeakazi. Katika hili Mheshimiwa Rais Samia suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua unataka kunikatisha, lakini angalau moja niliseme la muhimu kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakizungumza sana katika maswali mbalimbali hapa Bungeni wakiuliza Wizara yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, sasa hivi tunakamilisha utaratibu wa kuweza kupeleka magari katika kila Wilaya katika nchi hii. Kwa hiyo, kila Mbunge ambaye ana changamoto ya gari katika jimbo lake, sasa inaendelea kupatiwa ufumbuzi. Fedha hiyo Mheshimiwa Rais ameshaitoa na wakati wowote magari haya, taratibu za manunuzi zitakapokamilika yataingia na tutaweza kukabiliana na changamoto hiyo ya usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo yanahusu masuala ya makazi na vituo vya Polisi…
MWENYEKITI: Ahsante sana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.