Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie. Kwanza nichukue nafasi hii kupongeza sana Ofisi ya CAG kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha kwamba Bunge hili linakwenda siyo kama kipofu, bali tunakwenda huku tukiwa tunaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo nataka niongee kutoka kwenye ripoti ya CAG, nami ni Mjumbe wa Kamati. Kwanza kabisa, yapo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameshaongea. Cha kwanza nilichotaka kuongea ambacho CAG amekiongea na kinaonesha wasiwasi, nami binafsi pia nikapata wasiwasi, kwanza ni kuhusiana na fedha za ruzuku ya maendeleo ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, CAG anasema pesa za maendeleo zinazopelekwa kwenye Halmashauri zetu baadhi yake zinaonekana zimepelekwa bila kupitishwa au kupatiwa idhini kutoka kwenye Bunge hili. Wasiwasi wangu unaanzia hapo. Zipo zaidi ya Halmashauri 19 ambazo zimepelekewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 47 bila idhini ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu kubwa hapa kama Wabunge ni pamoja na kuisimamia Serikali na kupitisha hizi bajeti za Serikali. Sasa nashindwa kuelewa, ni kwa nini fedha hizi shilingi bilioni 47 zipelekwe katika Halmashauri, hata kama nia ni njema, ndiyo zipelekwe katika hizi Halmashauri bila Bunge kujua au kuidhinisha matumizi yake kwenye hizi Halmashauri?

Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu unakuja, pale ninapojiuliza, wenzetu Serikali wana mpango gani na Bunge? Je, wanataka kutunyang’anya ajira zetu? Kwa sababu sisi kazi yetu ndiyo hiyo, tuje hapa tupitishe bajeti, tuwahoji na kadhalika. Sasa unapokwenda moja kwa moja unapeleka fedha hizi bila kunipa mimi, una nia gani? Kwamba unanifuta kazi yangu, au una mpango gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, fedha zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo zikiwa pungufu. Hapa naipongeza Serikali. Zaidi ya Halmashauri 163 zimepelekewa shilingi bilioni 500 kama ruzuku ya miradi ya maendeleo, lakini wamejitahidi kwa sababu upelekaji wa miaka mitano mfululizo ni wastani wa asilimia 46; lakini kwa mwaka 2020/2021 wamepeleka asilimia 62 kwenye ruzuku ya miradi ya maendeleo. Hapo tunawapongeza na tunaona nia njema ya Serikali, lakini bado kuna upungufu wa asilimia 38 zaidi ya shilingi bilioni 300 ambazo hazijapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaiomba Serikali iangalie namna, kwa sababu tunapopeleka fedha hizi kwenye miradi ya maendeleo ndivyo tunavyokwenda kuchakachua uchumi kule chini kwa watu wetu. Halmashauri tatu zenyewe zimepelekewa fedha kama ambavyo jinsi tulikuwa tume-plan bila kuwa na mambo yoyote meusi ndani yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili; ili tuendelee tunahitaji watu; lakini tunahitaji watu tu, tunahitaji watu walioongezewa thamani. Hatuwezi kuendelea kama tuna watu ambao hawana thamani kubwa. Taarifa ya CAG inaonesha bado yako madai kwa watumishi wa umma wa nchi hii. Wanatudai mishahara shilingi bilioni 63. Yapo madeni ya malimbikizo ya posho, likizo kwa watumishi milioni karibu 96,650,000,000. Hawa ndio rasilimali watu tunaotegemea kwamba wafanye kazi kubwa kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatutaweka uwekezaji kwa watu hawa, ina maana utendaji wao ndio maana unakuwa ni duni. Watu hawa ndio tunaopelekea mabilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo, halafu hujampa fedha yake ya nauli anapokwenda likizo, ndio maana unakuta sasa wana-temper na mifumo, wanafanya mambo meusi meusi ili angalau waweze kufidia ule upungufu na makali wanayopata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeelezwa hapa, Manispaa moja tu ya Ilemela kwenye mitando tayari wame-temper na shilingi bilioni karibu nane, zimefutwa vocha za karibu 822 kwenye mfumo bila utaratibu unaoeleweka. Tumeelezwa hapa, Ubungo wameingiza figure kwenye mfumo ambao Mwenyekiti wangu wa Kamati amesema tu kwamba ni shilingi milioni 500 ambayo haieleweki yaani. Ukiwauliza, wanakwambia ilikuwa ni namba ya simu. Unashindwa kuelewa, namba ya simu gani inaanza na kodi ya 500? Ni ujanjaujanja na ubadhirifu ili kuhakikisha kwamba wanakuja ku-temper na fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoangalia, na kuwaangalia watumishi wa umma, hatuwezi kufanya mambo makubwa yakaenda sawa sawa na maendeleo kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna malalamiko ya kikokotoo kwenye nchi hii…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, …

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wake, lakini nadhani Bunge hili pia linapaswa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu baada ya CAG kuwa ametoa taarifa hiyo na hasa kwenye malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishajipambanua kwamba anahitaji rasilimali watu iweze kupatiwa haki na stahiki iweze kutekeleza wajibu sawa sawa; mpaka tarehe 31 Januari, Serikali ya Awamu ya Sita imeshalipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma 116,792. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haikuishia hapo. Katika hayo malimbikizo ya mishahara imekwishakutumia fedha za Kitanzania shilingi bilioni 199.365. Kwa hiyo, tunampongeza CAG kwa kazi nzuri, lakini hapo hapo pia tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona jambo hilo na kulipa stahiki za watumishi wa umma. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba unilindie muda wangu, lakini nashukuru kwa taarifa hiyo ya Serikali na naipokea. Hata hivyo tunayojadili hapa ni ile iliyoishia Juni, 2021. Kama wamekwenda hatua hiyo, tunawapongeza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwaombe, suala lingine linaloleta malalamiko, pamoja na mambo mengi tuliyoambiwa kuhusiana na kikokotoo, lakini kikokotoo kile ndani ya watumishi wa umma kinasumbua. Tunaomba Serikali ione namna ambavyo itakaa na watumishi wa umma na kuona wanafanya kazi kwa moyo bila kuwa na malalamiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kukaa hata na Jeshi la Polisi tu, wakielezea hali yao ya utendaji wa kazi wanakwambia sisi hatuna hata muda wa kupumzika kusema tutatafuta hela ya ziada kwa ajili ya kuweka kibanda. Tunategemea tukilipwa mafao yetu ndiyo tuweke kibanda. Leo ukiniambia unanipa kidogo halafu unanilipa kidogo kidogo unakuwa hunisaidii. Tunaomba Serikali ikakae ili kuendelea kupunguza malalamiko haya kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka kuongea, upo ubadhirifu wa mikataba ambayo Halmashauri zetu zinaingia, na uwekezaji ambao Halmashauri zetu zinaingia. CAG ameelezea. Yapo mambo ambayo Halmashauri zinafanya bila upembuzi yakinifu, kwenda kuwekeza miradi ya ujenzi wa mastendi na masoko. Unakuta kwa sababu tu Halmashauri hii imejenga soko, na wengine wanataka wakajenge soko na wangine wanataka wakajenge stendi na wengine wakaige kitega uchumi hiki, lakini bila kuangalia mazingira yao yanaendana na hicho kitega uchumi wanachotaka? Ndiyo maana yapo majengo mengi sana yamejengwa kwa gharama kubwa lakini hayatumiki ipasavyo kwa sababu Halmashauri zetu hazifanyi upembuzi yakinifu wa kujua mradi ule kama unaweza ukawa sahihi kwa mazingira yao na kama watu wao wanauhitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali iwasimamie. Hizi Halmashauri, Wizara husika, isimamie. Ile ya kwamba tunakwenda kujifunza mahali fulani, Waheshimiwa wanasafiri wanakwenda kujifunza mahali, anachukua tu ile utaratibu wa kujenga Machinga Complex ya Dar es Salaam anataka labda ajenge Iringa, wakati ni tofauti kabisa. Yaani Machinga wa Iringa ni tofauti kabisa na Machinga wa Dar es Salaam, na hawawezi kuendana katika biashara zao wanazozifanya. Kwa hiyo, hii imeipotezea Serikali mapato hela nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia zipo taasisi nyingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya, nakuongezea sekunde 10.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo taasisi nyingine ambazo nazo zinasababisha Halmashauri zetu kupata hasara. Taasisi kama TEMESA ni za Serikali, lakini nazo zimekuwa funza kwenye Halmashauri zetu. Kwanza, ukitaka kupeleka gari TEMESA watakuandikia vifaa vya bei kubwa kuliko hata kwa Mangi, unakwenda unatengeneza kwa gharama kubwa, wanakufungia kifaa kimekufa, yaani hawaeleweki. Kwa nini tutumie TEMESA kama tunajua kabisa hii inatuletea tatizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna NHIF, kila wakati kwenye hela za vituo vyetu vya afya wanatafuta visingizio vidogo vidogo, kwamba hawa wameshindwa kujaza fomu…

NAIBU SPIKA: Ahsante. (Kicheko/Makofi)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)