Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika hizi Kamati zetu tatu. Mimi leo nitachangia sehemu mbili tu; sehemu za kilimo na sehemu ya mifugo kwa sababu hizi zote, hawa maafisa ugani, nani wako kwenye TAMINSEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niseme, nataka niwaambie ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Tunazungumza sana habari ya mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei kwa sasahivi ni lazima uwepo; na kwa nini upo? Ni kwa sababu miaka hii miwili, mitatu ya nyuma kwanza kidogo palikuwa na shida ya mvua na vilevile vyakula vilikuwa bei ya chini. Kwa hiyo mkulima hakuweza kupata pesa ya kulima eka nyingi anavyohitaji. Mkulima atalima eka nyingi anazohitaji, akiwa na eka 100 ili alime zote lazima alichokivuna kiendane sambamba, ili auze, kiendane sambamba na eka anazoweza kulima mwakani. Akipata kidogo badala ya kulima 100 zile alizonazo atalima 20. Kwa hiyo automatically mazao yatakuwa machache na bei itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkulima akipata bei kubwa, kama ya mwaka huu, na mnaona wenyewe, kwa mfano Jimboni kwangu Gairo na majimbo mengine yote, wamelima takriban mashamba yote, hata mkipita njiani mnaona watu wamelima mashamba yote. Kwa hiyo, mavuno yatakuwa mengi na bei automatically itashuka. Lakini hapa habari ya kusema kwamba kuna mfumuko wa bei, lima na wewe, kama alivyosema Mheshimiwa Katani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ukalalamikia mfumuko wa bei, nasikiasikia hata huko nje. Unasikia maharage yamepanda bei, yule pale Mheshimiwa Mwijage amelima shamba la maharage, safari hii amepata maharage ndiyo maana anachekacheka tu, kapata hela nzuri, miaka yote anapata hasara. Kwa hiyo, lazima tusichanganye mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima, kama alivyosema Mheshimiwa Katani, mkulima tumuache auze anavyotaka yeye kwa sababu yeye ndiye amelima, tusimpangie. Na Serikali nayo tusiilaumu sana kwa sababu Serikali nayo hailimi, ila tumshauri tu Mheshimiwa Waziri atoe chakula kama alichosema kwenye Halmashauri na aangalie watu wa kuwapa. Apeleke tu pale sokoni, asimpe dalali kwa sababu dalali naye ataminya baadaye naye atauza bei kubwa. Kwa hiyo wangalie namna ya kutoa kile chakula ili kishuke bei. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama kweli tuumize watu asilimia 70 wakulima wa nchi hii kwa sababu tu ya kutetea watu asilimia 30, halafu hawa asilimia 70 tunaowaumiza ni kwa ajili ya jasho lao, haiwezekani kitu kama hiki. Na mimi ninataka kama kuna Mbunge yeyote anataka mkulima hapa ashushe bei ya mahindi hebu tusimame hapa, Wabunge wangapi wanataka wakulima washushe wasimame hapa tuwaone hapa? Muone hapa kama mtapata kura hata mbili majimboni huko. Ndio ukweli huo, tusiingilie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninamshangaa Mheshimiwa Bashe ana maneno mengi tu, aah ngoja, mimi hapa, wakulima, wambie ukweli kwamba hatuwezi tukaingilia masuala ya mkulima, muacheni mkulima auze anavyotaka. Na ninawahakikishia kwa mwaka huu kwa bei hii mtaona kuanzia mwezi wa saba, wa sita, vyakula vitashuka mpaka mtashangaa. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Hawa wafugaji nao sasa wamekuwa wanasumbuliwa yani, wamekuwa sasa kama hawaishi kwenye maeneo ya nchi yao. Mimi nilishangaa nilijua labda Waziri wa Mifugo atakuja na mpango wa kupima maeneo ya ufugaji akazanie huko, yeye anakazania heleni. Maana ng’ombe nao sasahivi wamekuwa masharobaro, wanatakiwa wavae heleni. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hizo heleni zimejaribiwa pale, nimeona Pandambili, zimejaribiwa Katavi. Mimi napenda sana kufanya research; nimezichukua, hata sasahivi nina heleni nne pale, lakini ukizi-track; nimewapa mpaka watu wa IT; hazioneshi ng’ombe kama yuko Dodoma. Maana ukichukua heleni si ni lazima ng’ombe aonekane yuko Dodoma? Hazioneshi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, yaani wanaokazania heleni wanataka ziishe ndani ya mwaka mmoja, wakati vitambulisho vya taifa vinatakiwa viishe miaka 11 havijaisha. Yaani vitambulisho vya taifa havijaisha ila heleni ziishe. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, naikubali taarifa. Imekaa vizuri. Haiwezekani kitu kama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nina wasiwasi, jamani, huyu Mama yetu, Mheshimiwa Rais, mambo kama haya hajui; lakini ninataka niseme ana kazi ya ziada upigaji an chi hii uko waziwazi. Sisi wengine tunajua na bahati nzuri tunawajua mpaka hao wenye hizo tenda, tunawafahamu. Kama kweli kule Katavi walikofanyia majaribio watuambie ng’ombe wangapi waliokufa? Ng’ombe wangapi ambao waliwaona wamechepuka wameingia labda kwenye hifadhi au kwenye nini, kama wanayo hiyo taarifa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii wazungu ulaya wanatumia, lakini wanajua kila kitu. Hapa Kenya hawatumii, Uganda hawatumii, South Sudan hawatumii, eeh, hapa tunataka sisi tunaanzisha vitu ambavyo havina mfano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ng’ombe mlianza na chapa, chapa imekuja imeshindikana. Mmekuja kengele, kengele imekuja imeshindakana. Sasa mmekuja na heleni, heleni ikishindikana mtataka wavae shanga za kiuno; eeh! ndiyo maana yake hiyo. Ikitoka hapo mtataka wavae vikuku vya miguu; maana yake sasa tunawavisha ng’ombe hawa. Mimi nasema, kwa suala kama hili msiichafue hii Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoweka mipango. Kama mipango ni mizuri mna harakanayo ya nini? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu Mheshimiwa fanyeni uchunguzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Sekunde 30.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, fanyeni uchunguzi. Yule mwenye tenda hiyo wale wanaotaka kuzigawa ndio wanakaa na hawa watu wa Wizara ya Mifugo wanaongea, waklimaliza kuongea ndipo wanaenda kuwashauri wale wafugaji. Haya ni mateso makubwa sana, mimi sikubaliani kabisa na hii heleni. Ahsante. (Makofi)