Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye taarifa ya mwaka ya Kamati ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha Februari 2022 hadi Januari 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea masuala kama matatu, muda ukiruhusu masuala manne. La kwanza masuala ya lugha katika mahakama zetu. Kama wanakamati walivyosema, mimi sipo kwenye Kamati hii lakini kama Wanakamati walivyosema, mimi niko katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata nafasi ya kuongea na wawekezaji walio wengi; wakati tunapitisha sheria mpya ya uwekezaji, moja ya jambo lililojitokeza kama concern kubwa ya wawekezaji ilikuwa ni kwamba; kuwa na sheria kwa Kiswahili ni jambo jema lakini ni vizuri sana sheria zile badala ya kungoja translation, zikatafsiriwa halafu wawekezaji wakapewa au zikatumika kuwavuta wawekezaji kwa kuzisoma huko waliko, ilionekana ni vyema na itakuwa na tija kama sheria zetu zitakuwa kwa Kiswahili na Kingereza. Hilo linaendana na dhima nzima ya kutaka kuona kwamba tunapata wawekezaji na kwa kweli tuko katika ushindani wa wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata mifano mingi iliyoonesha kwamba kuna nchi nyingi ambazo zimekwenda kwenye lugha zao kutunga sheria lakini vile vile zimetumia lugha ya Kingereza kama moja ya lugha ambazo zitatumika pamoja na lugha ya nchi ile. Nchi kama Rwanda na India zina utaratibu huo. Kwa hiyo mimi niungane na kuiomba sana Serikali kwamba kwa maslahi mapana ya kuangalia kwamba tunakwenda kuwa-include watu wote na vile vile tunajaribu kupunguza migogoro. Tukumbuke kwamba tafsiri ya sheria kwa lugha moja kama itatumika na watu wengi kuna uwezekano mkubwa, pamoja na kwamba sisi tunaifahamu lugha hiyo ikaleta mgogoro kwenye tafsiri. Ukishakuwa na mgogoro ni gharama. Kwa hiyo ni vizuri basi wazo hilo likatiliwa maanani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; kuna suala la taasisi ambayo iko katika utekelezaji na inasimamiwa na Wizara hii, Taasisi ya Baraza la Biashara. Taasisi hii ya Baraza la Biashara imeundwa kwa mujibu wa Waraka Namba Moja wa Mheshimiwa Rais wa mwaka 2001. Moja ya changamoto ambazo Kamati imeziona katika baraza hili ni suala zima la maamuzi kutotekelezwa. Baraza hili halikutani kila siku, halikutani kila mwezi linakutana kwa mwaka mara mbili; na ni baraza ambalo limeundwa kwa ajili ya kuwa ni forum ya dialogue kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maamuzi yanapokuwa yamefikiwa yanataka utekelezaji. Haitakuwa inatutendea haki kama nchi iwapo tutakuwa na baraza kama hili. Litafanya maamuzi yanayotaka utekelezaji, maamuzi hayo yasitekelezwe. Niombe sana Serikali, kwamba ihakikishe kwa kweli baraza hili likishafanya maamuzi, maamuzi yale yanatendewa haki. Tulichobaini kingine katika utafiti wangu wa haraka ni kwamba wanapokwenda kwenye kikao kingine wanaanza kuongelea regulations mpya ambazo zimetungwa ambazo hazi- encourage uwekezaji; kwa hiyo imekuwa kama vicious cycle. Kwa hiyo ningeomba sana baraza hili lifanye kazi kama vile ilivyokusudiwa na Waraka wa Rais, kwa maana ya kuwa ni dialogue, forum ya maongezi na forum ya kutatua matatizo na changamoto za wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilipenda niongelee ni suala zima la Ofisi ya Mashtaka. Kamati imetuambia hapa kwamba ofisi hii imefanya kazi kwa mafanikio. Kuna ukweli pengine kama imefanya kazi kwa mafanikio, lakini vile vile wameonesha kwama bado kuna matatizo hasa ya ucheleweshaji wa utekelezaji wa hukumu. Suala hili ni suala ambalo lina impact kwenye kutenda haki na kwenye kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Hii ni kwa sababu sisi tunaangaliwa na mataifa mengi pamoja na tunaangaliwa na wawekezaji kwamba ni nchi ambayo inathamini sheria zake. Sasa hukumu inapotoka na inapokuwa DPP ameshindwa kesi ni suala la governance kwamba hukumu hiyo itatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende mbali zaidi, hatuwezi kufumbia macho, kwamba ofisi hii ya DPP imekuwa na sintofahamu nyingi kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake. Jambo hili limeongelewa na Mheshimiwa Rais mwenyewe, na amekwenda mbali zaidi akataka akaunda Tume ya Jinai ili iweze kwenda kuangalia haki jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi hii ni ofisi muhimu sana katika utawala bora. Nipende kumuongelea Jaji Samatta ambaye wengi tunamfahamu, ni jaji ambaye alifanya kazi kama DPP miaka ya 1970 lakini akawa Jaji Mkuu ambaye alistaafu mwaka 2007. Yeye alisema maneno yafuatayo; “DPP na maofisa walio chini yake ni watumishi wa nchi ambao wajibu wao ni kulinda maslahi ya umma, yakiwemo yale yanayohitaji mtu asiyeonyeshwa na ushahidi kuhusika na utendaji wa kosa la jinai hashitakiwi na mshtakiwa ambaye ushahidi dhidi yake hauthibitishi kwamba alitenda kosa hatiwi
hatiani.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya ni ya msingi sana na ofisi kama ingezingatia maneno haya nadhani tusingekuwa na sintofahamu ambazo Mheshimiwa Rais ameziongelea kwa kina. Nipende kusema, wahasibu wao tunasema wanajumlisha na kutoa lakini wanasheria wana mambo matatu. Unaangalia facts, unaangalia evidence, una-apply law. Inasikitisha kuona kwamba inawezekanaje tukawa na ofisi ya DPP ambayo inakwenda kwenye kesi, inashindwa kwa sababu kesi ambayo hawatakiwi washindwe, hawatakiwi hata waipeleke mahakamani kwa sababu hizo ni basic principles za sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipende kusema kwamba suala la kutokutekeleza hukumu ingekuwa ni vizuri hii Tume ya Haki Jinai itakapofanya tathmini yake ichunguze kwa kina kuona maofisa ndani ya ofisi ya DPP ambao kwa makusudi wanafanya mambo ambayo yanaitia nchi hasara na inasababisha wao washindwe kesi halafu inapofika kwenye kulipa, wao wenyewe tena hawataki kutekeleza hukumu kwa kutolipa. Jambo hili lina madhara kwenye uwekezaji wa nchi, lina madhara kwa kuonyesha kwamba sisi hatuwezi kutekeleza mikataba; na hukumu ni kama mkataba ambao mahakama imeutoa ili utekelezwe kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.