Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kabla ya yote kwanza naunga mkono hoja zilizotolewa na wote Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Katiba na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo na kukubaliana na taarifa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pili ningependa kujielekeza katika kuchangia kidogo kwenye Sheria Ndogo. Kama unavyofahamu sheria ndogo ndiyo sheria ambazo zinatekelezwa huko chini kabisa kwenye maisha ya watu ya kila siku. Inawezekana sheria moja ikazaa sheria ndogo hamsini hata mia na ndiyo zinazotekelezwa kila siku huko, na zipo sheria ndogo ambazo katika utungaji wake zimeonekana kupitia Kamati ya Sheria Ndogo kwamba zinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa jambo hili ni jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchi inayofuata utawala wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano ipo Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru ya Manispaa ya Temeke ya mwaka 2022 kifungu cha 5(5) kinampa uwezo Afisa Muidhiniwa wa kukusanya ada na ushuru kuingia jengo lolote, wakati wowote.
Narudia kuingia jengo lolote, wakati wowote kwa ajili ya kukusanya ada na ushuru. Sasa ukiangalia sheria ndogo hii inapingana na Katiba, ukisoma Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Ibara ya 16(1) Katiba inasema hivi naomba ninukuu; “Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi, familia yake na unyumba wake na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi.”
Sasa kama unampa Afisa Muidhiniwa kukusanya kodi na ushuru kuingia jengo lolote, wakati wowote maana iwe saa sita, saa saba na anawakuta wakati mwingine watu wako kwenye shughuli nyingine muhimu majira ya saa nane yeye anataka ushuru na kodi utaona kabisa kwamba sheria hii haiendani na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hiyo tu zipo sheria, ipo sheria ndogo ambayo ni Sheria Ndogo za Udhibiti wa Uchimbaji wa Madini ya Ujenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambayo ilitangazwa kwa Tangazo la Serikali Namba 564; kifungu cha 8(4) kinaweka masharti ya kwamba ikiwa chombo kama gari ambalo limekutwa na madini hayo ya ujenzi mawe/mchanga, likakamatwa na mwenye nalo hakuonekana ndani ya siku 30 basi sheria hii ilikuwa inatoa mamlaka kunadiwa hiyo gari na pesa za halmashauri ziweze kuchukuliwa.
Sasa ukiangalia gari ya shilingi milioni arobaini/hamsini ninyi mnadai ushuru wa trip moja ya mawe, kwa sababu siku thelathini mwenye nalo hakuonekana, sasa mnachukua sheria na katika kuchukua sheria mnanadi mali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 13(1) hadi (6) ambacho kinazungumzia usawa mbele ya sheria nitanukuu sheria hiyo inasema hivi; “Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yanalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.” Sasa wewe una nadi gari ya mtu ya shilingi milioni hamsini kwa madai ya trip moja ya mawe bila kumpeleka mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, Katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 13(6)(a) kinazungumza hivi; “Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa umakini na haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine kisheria kutokana na maamuzi ya Mahakama au chombo kingine kinachousika.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vifungu hivi vya Katiba na ukaangalia sheria hizi ndogo ambazo zinatungwa na halmashauri zetu, utaona kabisa kwamba zinakinzana na kutofautiana mbali kabisa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu, kuna sheria inayohusu masuala ya mazingira ya udhibiti wa mifuko ya plastiki na vifungashio ambayo kifungu cha 32 kinasema kwamba; “Iwapo mtu aliyeingiza vifungashio na vikakamatwa basi mtu huyo atakuwa na haki ya kukata rufaa ndani ya siku thelathini kwa Waziri mwenye dhamana.” Lakini kanuni hiyo haisemi Waziri mwenye dhamana itamchukua muda gani kutoa haki au kumaliza shauri hilo na kwa vyovyote vile jambo hili linaweza likafika mahala likapoteza haki ya muhusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 64(5) inasema; “Katiba itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba basi Katiba itakuwa na nguvu na sheria hiyo nyingine kwa kiasi inachoathiri Katiba itakuawa ni batili.”
Kwa hiyo, sisi katika kuchambua sheria ndogo tuliona kabisa kwamba sheria ndogo hizi nyingine zinatungwa na zinakinzana na Katiba na kwa mamlaka haya ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 64(5) basi sheria hizi au kanuni hizi zinazotungwa zinakuwa zimekufa zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa mchango wangu huo, basi naomba kuendelea kuunga mkono hoja na nawapongeza sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili, ahsante sana. (Makofi)