Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Ofisi ya Rais TAMISEMI muda huu wa asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya uchumi jumuishi kwa maana ya inclusive economy ambapo kila Mtanzania atanufaika na ukuaji wa uchumi wa Taifa letu ni pale ambapo kila Mtanzania atakuwa amefikiwa na huduma muhimu na za lazima kama vile maji, umeme, barabara, afya na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu hii ya Sita kwa sehemu kubwa imefaulu sana kwenye maeneo makubwa mawili au matatu. Kwa sehemu kubwa tumefaulu suala la umeme vijijini lakini changamoto bado zipo, linalohusiana na sehemu hii ya TAMISEMI tumefaulu sana kwenye eneo la elimu na afya hasa kwenye shule zetu za msingi na sekondari kwa bajeti kubwa ambazo zimetengwa kwenda kuboresha maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upande wa afya kwa kiwango kikubwa, fedha zimekuwa zinakwenda kwenye zahanati, fedha zimekuwa zinakwenda kwenye vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa tumeendelea kuzijenga. Kwenye eneo hili naomba niipongeze sana Serikali ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri Mheshimiwa Innocent Bashungwa pamoja na Manaibu Waziri wake wote wanafanya kazi nzuri sana. Nitumie pia fursa hii kumpongeza Katibu Mkuu Profesa Shemdoe haya ni majembe kwelikweli na wamefanya kazi nzuri katika maeneo hayo niliyoyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia nzuri na kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na jitiahada kubwa ambazo Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuzifanya bado tuna changamoto kubwa kwenye barabara za vijijini. Nimesema ili Watanzania wanufaike na dhana ya inclusive economy ni lazima barabara za vijijini ziboreshwe na zijengwe kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo imekuwa inatolewa bado haitoshi, Madaba Halmashauri yetu kwa miaka mitano mfululizo imekuwa ikipokea asilimia tano tu ya mahitaji yake yote ya barabara za vijijini. Madhara yake tumeendelea kuwa na barabara mbovu kwa muda mrefu. Hata hivyo, nitambue kazi kubwa ambayo Serikali imeifanya kwenye bajeti iliyopita ambapo alitoa zaidi ya Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano ambayo kwa mahitaji ya Madaba ni asilimia 15 ya mahitaji ya barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kupiga hatua kwenye eneo hilo, nampongeza sana CEO wa TARURA na timu yake nzima na Serikali katika ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Serikali itambue kwamba pamoja na kutoa fedha kiwango hicho, kwa Madaba yetu sisi hiyo ni asilimia 15 tu ya mahitaji halisi ya barabara Halmashauri ya Wilaya ya Madaba. Ndani ya Mji wa Madaba tuna kilomita 66 zimeanza kufunguliwa kwa maeneo ya Lituta na Madaba Mjini na bado hatujakidhi mahitaji ya Watanzania wanaoishi Madaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Halmashauri ya Madaba tuna zaidi ya kilomita 642 ambazo zinahitajika kujengwa na kuboreshwa. Tuna madaraja yanayokwenda maeneo muhimu ya uzalishaji, ikiwemo Yerusalemu, Kwangoko, maeneo mengine ya Mtengimbole, Litepatile na maeneo yote ya Madaba tunayo changamoto kubwa ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri azingatie kwanza kuhakikisha kwamba bajeti iliyokusudiwa itolewe lakini fedha zaidi za ujenzi wa barabara vijijini ziongezwe, bila hivyo tutakuwa hatujakidhi matakwa ya kujenga uchumi inclusive ambao utawanufaisha Watanzania wengi hasa walioko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Madaba ni Halmashauri changa, mapato yake kwa asilimia kubwa yanawategemea wakulima wadogo wadogo na kwa sehemu nyingine tunategemea kilimo cha miti, ukiachana na hizo hatuna vyanzo vingine. Tunaomba Serikali itusaidie tujenge stendi ya Madaba ambayo itachangia asilimia 20 ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maslahi ya muda, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)