Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimesimama mbele ya Bunge lako kwa heshima kubwa. Awali ya yote nianze kuwapongeza sana Ofisi Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri hongera sana Manaibu wako wote wawili ni watu ambao wanatupa ushirikiano wa kutosha tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika, pia nisisahau kumpongeza mshauri Mtendaji Mkuu wa Wizara Profesa Shemdoe pamoja na timu yake yote, nisiwasahau Ndugu Seif pamoja na DID Ndugu Moga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwanza nimeanza kwa kuwapongeza kwa sababu ninakiri kwamba kazi iliyofanyika na TAMISEMI ni kazi kubwa sana, kazi hii imefanyika kwenye Majimbo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. Mfano, kwangu Kaliua wamenisaidia mpaka sasa tunapoongea tumemaliza hospitali ya Wilaya karibu Bilioni 2.2, tunaendelea na ujenzi wa vituo vya afya viwili Shilingi Bilioni Moja, lakini tunaendelea na zahanati nane za ujenzi, ndiyo maana nasimama na kusema siyo hiyo tu hata barabara kazi iliyofanyika ni kubwa sana na nilikuwa najiuliza hawa mabwana hii teamwork wanaitoa wapi. Nikagundua inawezekana hawa ni mashabiki wa ile timu ya nguvu moja ile, ndiyo maana mambo yanazidi kuwa mazuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wenzangu kuweka msimamo mkubwa sana kwa Waheshimiwa Madiwani. Waheshimiwa Madiwani wanaishi mazingira magumu sana, wapo Madiwani kutoka Kijiji mpaka Kijiji ni kilomita 60. Kwa mfano, kwangu kuna Kata inaitwa Ukumbisiganga kutoka Ukumbisiganga mpaka Usinga kilomita 48, Diwani anatakiwa ahudumie wananchi kule. Anahudumia vipi hana pikipiki, posho 350,000 kwa kweli mfumuko wa bei upo, hii hali kwa nini tuiangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawiwa kuishauri Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nawaomba kwa heshima zote tuhakikishe Madiwani tunawapandishia posho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina ushauri mkubwa sana sehemu ya Kamati zile za kwetu kule Halmashauri, Kamati ya Elimu, Afya na Maji na Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira. Kamati hizi hazikagui miradi kwa sasa, kwa nini Kamati ya elimu, afya na maji haikagui miradi yake ya elimu, miradi yake ya elimu na miradi yake afya. Kwa nini Kamati za uchumi hazikagui miradi ya kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo mliyoutoa TAMISEMI hapo nataka niwashauri mlielekeza Kamati ya fedha ndiyo ikague, hizi Kamati zingine wanapokutana kwenye vikao tumewanyima ownership, wanatakiwa wafahamu nini kinaendelea kwenye maeneo mengine. Kwa hiyo, nashauri mtoe mwongozo angalau mara mbili kila mwaka hizi Kamati za Elimu, Afya na Maji na Kamati za Uchumi, Ujenzi na Mazingira zikague mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri jambo lingine kwenye upande wa TARURA, bararaba mtandao wa barabara kwangu ulikuwa kilomita 1,370 sasa vijiji 26 Mheshimiwa Rais kaviachia, sasa mtandao umeongezeka tuna kilomita 2,370 naomba tuangalie zile bajeti zetu za maintenance pamoja na mambo mengine ili kuhakikisha tunaisaidia TARURA vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizugumzie suala la Watumishi, nimeongea mazuri yaliyofanyika lakini haya mapya yote yaliyofanyika zikiwemo shule shikizi zinahitaji watumishi, zinahitaji walimu, zinahitaji watumishi wa Idara ya Afya, zinahitaji Maendeleo ya Jamii. Naomba kwa hekima zote, niwaombe Serikali yangu Sikivu ya CCM tuhakikishe tunawapata watumishi hawa ili kuhakikisha tunakuwa na kauli moja ya kusaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nimalizie kwa kuomba jambo moja, TARURA hawana vifaa vya maabara hebu TAMISEMI wazungumze na watu wa ujenzi. Miradi inapokamilika yale majengo yaachwe kwenye Halmashauri husika, kinyume cha kuyaacha hayafanyi chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwangu Mkurugenzi alishaomba TARURA wakitumia yale kama Ofisi na vile vifaa vya maabara Mratibu wa Mkoa wa TARURA hana vile vifaa. Barabara zetu tunazipimaje? Ni kwa nini tusiweke uratibu mzuri wa vifaa ili barabara zetu zipimwe vizuri na tuweze kujua na kuzijenga kwa ubora unaotakiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nakushuru, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)