Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijali afya kuweza kuzungumza leo ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wote ambao wamezungumzia maslahi ya Madiwani, tukiamini na Wabunge ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu. Tunatambua changamoto ambazo wanapitia Madiwani wetu, na kwa sababu ya muda hiyo hoja naamini imepokelewa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye Ibara ya 145 ya Katiba ya nchi yetu ambayo inazungumzia kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa. Mwaka 2008 tulipata Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere, mwaka 2014 tukiwa tumeanzia kwenye vikao vya DCC, RCC aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Stella Manyanya akaandika barua kumuandikia Waziri wa TAMISEMI kipindi hicho na 2014 hiyohiyo ikaonekana katika Halmashauri ambazo zinatakiwa kupewa Halmashauri ya Mji ikaonekana Wilaya ya Nkasi tumekidhi vigezo 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza ni mwaka 2022 na hili suala siyo utashi wa mtu ni takwa la Kisheria. Kwenye Ibara 145 Kifungu Kidogo cha Pili Bunge wamepewa Mamlaka ya kutunga Sheria ya kuelekeza namna ya kutengeneza hivyo vyombo vya Serikali za Mitaa.

Mheshimiaw Mwenyekiti, Bunge lilishatunga Sheria, kama tumeshakidhi vigezo bado mkatunga Kanuni mkaleta na vigezo vyenu, kigezo cha kwanza ni kwamba hiyo Halmashauri ya Mji inatakiwa iwe na mitaa 60, tunayo mitaa 90. Mmezungumzia kwamba kuwe na kilomita za mraba kuanzia 300 tuna 1,688, mmezungumzia Kata tumeshafika mpaka Kata 12. Kwa hiyo ukiangalia kwenye asilimia imekuja Tume kutoka TAMISEMI ikaja pale ikaangalia wakasema tumekidhi vigezo asilimia 97.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa umekuwa Mkoa toka mwaka 1974 lakini ndiyo Mkoa wenye Halmashauri Nne tu. Kama sheria zipo, kanuni zimetungwa, vigezo vimeletwa ikaonekana tumekidhi vigezo, nini kinapelekea mpaka leo hatujapata Halmashauri ya Mji? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa!

MWENYEKITI: Utaratibu kuhusu taarifa nafikiri umeshatolewa, kwa hiyo utasimama mahali pako jicho la Kiti likikuona atakunyanyua. Endelea Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu dhana ya kuanzisha Serikali za Mitaa ilikuwa ni kupeleka huduma kwa wananchi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Manyanya Kanuni gani? Umesimama kwa Kanuni gani Mheshimiwa Manyanya?

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 76 jambo ambalo linaendelea.

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru nilikuwa najaribisha utaratibu ambao Mheshimiwa Spika ametuelekeza lakini ni ngumu sana kuonekana. Pili, niseme tu kwamba najaribu kusema kwa hili suala ambalo limezungumzwa inaonekana kwamba kuna changamoto kubwa sana katika baadhi ya Halmashauri ambazo zipo pembezoni kwa muda mrefu zikiomba.

MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa Manyanya umesema Kanuni namba?

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, 76 jambo ambalo limepita linazungumzwa. (Kicheko)

MWENYEKITI: Anaendelea kuzungumza, Mheshimiwa Khenani endelea.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana pamoja na kwamba Mheshimiwa Stella Manyanya hajapewa nafasi nilitegemea angezungumza kitu ambacho alikifanya mwenyewe akiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiyo njema, tunapokuwa tunazungumzia keki ya Taifa lazima tuangalie mgawanyo wake, kama Mkoa wa Rukwa umepata Mamlaka ya kuwa Mkoa toka mwaka 1974. Ukiangalia kwenye miradi ya kimkakati bado Mkoa wa Rukwa kama jina lenyewe. Mnaruka Mkoa kama ambavyo uko kwenye jina hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo inapokuwa ni keki ya Taifa basi iangaliwe kwenye mazingira hayo. Mradi wa kimkakati kwenye Mkoa mzima ni stendi ya Sumbawanga Mjini. Kwa mazingira hayo tunategemea leo unawezaje kulinganisha ile ya Halmashauri ya Nkansi na Halmashauri zingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, kwa kuwa document ipo mezani kwenu, kuondoka Waziri mmoja kuja mwingine haimaanishi kwamba ofisi imehama. Nimeshaona utendaji wenu wote mnafanya kazi nzuri, naomba na hili mkaonekane kwa vitendo kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu TARURA. Nami niungane na Wabunge wengine, kuompongeza Chifu Seif kwa kazi anayoifanya. Jambo la kwanza la sifa yake ni kuheshimu viongozi kusikiliza mawazo yao. Hata kama fedha haipo unapomsikiliza mtu anasema nini unaweza ukamshauri na akaelewa. Hiyo ni pongezi ambayo tunampa pamoja na Waziri na timu yako yote mmekuwa mkifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hilo jambo ninaushauri. Kwa kuwa Wizara ya TAMISEMI ni pana sana na ina vitu vingi, ukiangalia hapa kuna Naibu Waziri anahusika sijui na mambo ya afya, mwingine anahusika na barabara, sijui Serikali za Mitaa, mambo ya elimu. Kwa kuwa Waziri Mkuu yupo hapa, lengo siyo kuongeza wigo wa Mawaziri ni vizuri, kwa sababu yupo Chief wa TARURA tukapata Naibu Waziri ambaye atahusika na barabara peke yake na jambo hili litakuwa ufanisi upande wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia changamoto ya barabara kwenye nchi hii bado ni kubwa sana, ni kubwa mno. Nitampiga leo Mheshimiwa Naibu Waziri, nitakupigia wewe Waziri, huku unapigiwa mambo ya elimu, huku sijui unaambiwa mambo ya Local Government, lakini akiwepo mtu ambaye atashughulika moja kwa moja na barabara italeta ufanisi kwenye Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nimeshazungumza bajeti iliyopita nikasema Wilaya ya Nkansi kuna shule ambazo mpaka sasa wanafunzi wanapotaka kufanya mtihani wa darasa la saba hawawezi kufanya kwenye shule yao mpaka wapande boti waende wakafanye mtihani kwenye shule nyingine, siku ya mtihani. Mnaweza mkanona mna wa disturb watoto kiasi gani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunategemea watoto wa Nkansi wafanye vizuri? Hayo maboti yenyewe tunayasema Serikali hamjapeleka hayo maboti inabidi wategemee ya wafanyabiashara, kwa hiyo kama siku hiyo hayapo mnawafanya wasifanye mitihani. Kama maboti yapo kwa nini Askari wasiandaliwe wapeleke kule hiyo mitihani na wakaisimamia, badala ya kuwa disturb wanafunzi?