Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuichangia hotuba hii ya Waziri wetu wa TAMISEMI. Kabla sijaanza kuchangia hotuba hii naomba kwanza nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Waziri wanafanya kazi nzuri kwelikweli. Waziri huyu siku zote mabega yako chini na mimi niseme tu Mawaziri wengine mchukue mfano huu. Kijana huyu unampigia simu anapokea, kama akiwa kwenye kikao nipo kwenye kikao halafu anakupigia, lakini sijawahi kumuona hata siku moja akikasirika, yeye anakasirika akiwa field kule akiwa anazungumza na Wakurugenzi pamoja na Watendaji wa Halmashauri. Mheshimiwa Waziri piga kazi na Naibu Mawaziri safi sana hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa na mazuri ambayo ametufanyia sisi watu wa Jimbo la Kibiti. Mheshimiwa Rais alitafuta fedha takriban shilingi trilioni1.3, katika fedha hizo najua ziligawiwa Tanzania nzima katika sekta nzima ya elimu shilingi bilioni 662.32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kibiti vilevile humo tumo, tumepewa fedha Shilingi Milioni 470 tunajenga shule ya Sekondari pale. Kama hivyo haitoshi tumepewa fedha shilingi 1,480,000,000 tumejenga madarasa takriban 74, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika eneo hilo. lakini kama hivyo haitoshi Mheshimiwa Rais vilevile ametupa fedha shilingi milioni 100, tumejenga bweni kwa vijana ambao wana mahitaji maalum. Safi sana Mheshimiwa Rais nami sina budi kusema nani kama Mama Samia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika sekta nzima ya afya mimi najua kuna fedha zilizokuwa zimeanza kutolewa takribani shilingi bilioni 241.41 katika fedha hizo nasi Kibiti vilevile tumo. Tumepewa fedha takribani shilingi milioni 500, tumejenga pale kituo cha afya kizuri katika Kata ya Mjawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo haitoshi tumekwenda vilevile kujenga nyumba za Watumishi kule katika Kata ya Ngw’aluke pale Nyamatanga, kwa Diwani Bingwa kabisa Ndugu yangu Mkenya kazi nzuri sana inakwenda kufanyika na Mheshimiwa Rais. Nani kama Mama Samia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, tunafahamu vilevile katika fedha hizo kuna fedha ambazo Mheshimiwa Rais ameweza kututafutia sisi watu wa Jimbo la Kibiti. Tumepewa fedha katika kujenga zahanati, tumejenga zahanati kule kwetu Mbuchi, Mtawanya, tumekwenda kujenga zahanati katika Kata vilevile ya Mjao. Tumepewa vilevile fedha Shilingi Milioni 50, tumejenga zahanati katika Kata ya Kibiti, nani kama Mama Samia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee mbele. Katika fedha hizi vilevile kuna fedha za TARURAambazo zimetolewa Bilioni 597, katika fedha hizo nasi Kibiti vilevile tumo. Tumepewa fedha takribani Shilingi Bilioni 200 lakini kubwa kuliko yote Mheshimiwa Rais ameweza kutupa fedha takribani shilingi bilioni 6.2. tumejenga daraja pale Mbuchi, daraja zuri kabisa leo hii wananchi wa Mbwera wanaweza wakaja Kibiti na kuja Dar es Salaam na wakalala Mbwera bila shida yoyote. Nani kama Mama Samia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, nilikuwa naomba nitoe changamoto zilizopo ndani ya Jimbo langu. Nikianza katika sekta ya afya. Katika Jimbo langu nina shida pale kidogo kuna Kituo cha Afya kilichopo katika Kata ya Mwambao, kuna Kituo cha Afya kilichokuwa katika Katika ya pale Mbuchi. Vituo vya Afya hivi vimeshakamilika; lakini mpaka hivi leo ninavyozungumza hatuna vifaa tiba, tuna uhaba wa watumishi vilevile, kama hivyo haitoshi tuna zahanati kule Kiongoloni, Mbwera mpaka Maparoni hatuna Watumishi. Mheshimiwa Waziri hili naomba uliangalie kwa karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo lingine ambalo vilevile naomba nilichangie. Sasa naomba nitoe ushauri pale TAMISEMI. TAMISEMI pale kuna shinda, shida iliyopo kubwa zaidi ipo kwenye suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Tuna mfumo unaoitwa mfumo wa POS; mimi nipo katika Kamati ya LAAC, katika taarifa ya CAG ya mwaka jana fedha ambazo zilikuwa zimefanyiwa adjustment ni takribani Bilioni 4.5, fedha hizi zimefanyiwa adjustment na huu ni wizi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayekusanya mapato kule chini, amekusanya labda Shilingi Milioni Moja, halafu anakuja kufanya adjustment inaandika Shilingi 10,000 huu ni wizi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba liangalie hili kwa karibu sana kwa sababu tusipofanya hivyo tunakwenda kupoteza fedha nyingi sana kule katika eneo zima la ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo naomba nitoe ushauri wa hali ya juu TAMISEMI ni kuweza kuangalia ni jinsi gani ya kuweza kudhibiti mapato ndani ya Halmashauri zetu. Kuna shida kubwa tena kuna shida kubwa ya msingi kwa sababu kinachokuwa kinafanyika mapato yanapigwa, kuna Watendaji ambao siyo waadilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mtengeneze mfumo ulio halisia ili sasa kuweza kuhakikisha mnakwenda kudhibiti mapato ndani ya Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba kulizungumza hapa kidogo nitakwenda tofauti na Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Kuna baadhi ya Wabunge wenzangu wameweza kuchangia kwa heshima kubwa kwamba posho za Halmashauri ziende equal kwa kila Majimbo. Hapa kuna shida!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu nina Kata zipo kule Visiwani kabisa, kuna Kata ya Kiongoloni, Maparoni, Msala na Salale, ili Diwani kutoka kule kuja katika Makao Makuu ya Halmashauri kuja kufanya shughuli za Halmashauri maana yake ni kwamba lazima atumie siku mbili.
Mheshimiwa Waziri kila mtu ale na umbali wa Kamba yake kwa tukifanya hivyo tutakuwa tunawatendea haki hao Madiwani. Tena mimi ikiwezekana katika Halmashauri yangu suggest tu Taifa zima, tuweze kuweka utaratibu Madiwani hawa wapatiwe mpaka vyombo vya usafiri wanafanya kazi kubwa kweli, tukifanya hivyo tunakwenda kutetea maslahi mapana ya Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo haitoshi tunakwenda vilevile kutetea maslahi mapana ya kuweza kusuma maendeleo. Sisi Wabunge tupo huku, muda mwingi sana tunakuwa tupo katika Vikao vya Bunge, wao wapo kule ndiyo wanasimamia shughuli za kimaendeleo, kwa hiyo, tusipowawezesha hawa inakuwa shida tena ni shida ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)