Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana lakini niwie radhi leo sauti yangu sijui nani watani zangu wa Tanga wameniroga lakini nasikika. Nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie lakini kwanza nianze shukurani kwa Wizara hii ya Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Festo na Watendaji wote wa Wizara hii wamefanya kazi kubwa sana, mambo yameonekana Jimboni kwangu tumepata fedha za kujenga kituo cha afya lakini nimepata fedha za TARURA. Pia upande wa elimu kuna madarasa mengi yamejengwa hii ni juhudi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwaunge mkono wenzangu wanaosema Waziri huyu ni mtiifu, Waziri hana mabega ya juu, ni Waziri mzuri kijana mzuri na ataipeleka mbali sana Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze suala la Mfuko wa Jimbo. Mfuko huu umewekwa kwa ajili ya kuchangia au kuchochea maendeleo ya Jimbo na bahati nzuri sana, nimpongeze Waziri huyu pia ameongeza Mfuko huu kutoka shilingi bilioni 11 mpaka shilingi bilioni 15.9 karibu shilingi bilioni 6 ameongeza. Ameona umuhimu wa kuendeleza Majimbo na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuunga mkono suala hili na kuruhusu fedha zitoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la ugawaji wa Mfuko huu, Kitaifa Mfuko huu unagaiwa kutokana na mahitaji ya kuchochea maendeleo ya Jimbo, lakini kuna Majimbo tofauti. Majimbo mengine yana maji, yana umeme, yana barabara, yana kila kitu na Majimbo mengine hayana chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo ndiyo umejenga maboma ya zahanati, maboma ya vituo vya afya, lakini maeneo ambayo kuna maendeleo tayari fedha hizi ziangaliwe kwamba zigawiwe kwenye sehemu ambayo kuna mahitaji. Haina haja ya kugawa Mfuko wa Jimbo sawasawa kwa Majimbo yenye uwezo mkubwa na Majimbo ambayo ni masikini kabisa, ningependa sana Wizara ifikirie kuugawa Mfuko huu kwa mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia liko suala la Halmashauri zenye Majimbo zaidi ya moja lakini tofauti ya Majimbo hayo katika Jiografia. Kwa mfano Jimbo lina Kata 19 na Jimbo lina Kata 11, Kata 10 au Kata Tano lakini Mfuko unagawiwa nusu kwa nusu, sidhani kama ni sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni Jimbo langu la Tabora Kaskazini katika Halmashauri ya Uyui, Jimbo la Igalula lina Kata 11 na Jimbo la Tabora Kaskazini lina Kata 19, Mfuko unagawiwa sawa sawa. Kwa hiyo, maendeleo yanadumaa kwenye Jimbo kubwa imekuwa haraka namna hiyo? Ningeomba Mheshimiwa Waziri Bashungwa ufikirie upya vigezo vya kugawa Mfuko huu ili haki itendeke katika Majimbo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la elimu ya kufundishia na hili nalisema hapa kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu ni suala mtambuka kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara hii ya TAMISEMI. Kumefanyika tafiti nyingi sana kutambua kwamba je, Kiswahili kinafaa kufundishia masomo hapa Tanzania kwa elimu yetu darasa la kwanza mpaka darasa la saba na sekondari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nalisemea hapa kwa sababu ni muhimu ieleweke kwamba sera ya elimu ndio inayoamua lugha gani itumike. Lugha ya kufundishia duniani kote hakuna nchi iliyoendelea kwa kutumia lugha ya watu wengine. Hakuna kokote duniani ambako watu wameendelea kwa sababu wanatumia lugha ya watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uingereza wanatumia Kiingereza, Wafaransa Kifaransa, Wachina Kichina, Warusi Kirusi, Wajerumani Kijerumani, lakini Tanzania tunatumia lugha ya kufundishia Kiingereza watoto wanasoma Kiswahili Darasa la Kwanza mpaka Darasa la Saba, halafu wanabadilisha mawimbi wanaanza kutumia Kiingereza. Nusu ya elimu yao wanajifunza lugha badala ya kujifunza elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye tena utafiti ziko tafiti zaidi ya 40 kwa miaka 46 imefanyika na zote zinasema lugha inayofaa kufundishia Tanzania ni Kiswahili. Sasa naomba Serikali ifanye utafiti mahsusi kwa ajili ya lugha ya kufundishia iwe lugha gani Tanzania. Mimi nina imani nilileta katika Bunge hili Muswada wa kutaka Serikali ilete mabadiliko ya sera ili Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia. Katibu wa Bunge alinirudishia Muswada huo akaniambia kwamba Serikali inafanya mchakato na katika mchakato wa kuchambua sera lugha itafikiriwa pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina habari kwamba tumerudia pale pale kwamba lugha ziwe mbili Kiswahili na Kiingereza. Kwa hiyo, nina nia tena ya kuleta tena Muswada huo binafsi wa kuomba Serikali ilete Sheria ya Sera ya Elimu hapa kubadilisha lugha ya kufundishia iwe Kiswahili. Nitatumia Kanuni yetu ya kawaida Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka, 2020 Kanuni ya 94 na Kanuni ya 95. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)