Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya TAMISEMI, nami kama walivyotangulia wenzangu ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwenye Taifa hili. Pia naipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri inazofanya, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia mambo mawili lakini nitaanza na hili la mikopo ya asilimia 10. Kwanza ninaipongeza Serikali kwa kusamehe madeni ya vikundi vya mwanzo kabisa ambavyo walikuwa wamenufaika na mikopo hii kwa kushindwa kurejesha yale marejesho. Ni kweli na ni wazi kabisa kwamba mwanzo wa mikopo hii kulikuwa na mapungufu mengi sana vikundi vingi vilikuwa vinapewa mikopo lakini hawakuwa na elimu ya kutosha, walijikuta akinamama, vijana na watu wenye ulemavu wakishapata mikopo hiyo wanagawana mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kulikuwa kuna wanaoweza kufanya vizuri na kurejesha na wengine walikuwa wanashindwa kurejesha mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine iliyopo kwenye suala hili ni kwamba kuna kundi la akina Mama ambao wanashindwa kukopesheka sasa hivi kwa kigezo kwamba wanaambiwa mlishakopa awali, kuna wengine wamerudisha lakini wenzetu hawakurudisha, mkawatafute warudishe fedha zile ili muweze kukopesheka tena. Sasa kama Serikali ilishasamehe basi niziombe Halmashauri zichukulie vikundi hivi kama vipya viweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana hawa watu sasa wamekaa pembeni hawakopesheki tena tunawasaidiaje ni akinamama wengi sana na vijana wanashindwa kukopesheka, lakini pia niiombe Wizara kupitia Halmashauri zetu ziangalie tatizo kubwa linalofanya fedha hizi hazirudi.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Janeth kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mwandabila.

T A A R I F A

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumpa taarifa dada yangu Mheshimiwa Janeth.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumwambia kwamba hoja anayoongelea ya masuala ya mikopo ya wanawake ni hoja ya msingi na nilitaka kumpa taarifa kwamba kwenye taarifa ya Waziri TAMISEMI hakuna sehemu inayotuonesha impact ya assessment ya hiyo mikopo tunayoitoa kwamba iliwavusha watu kutoka eneo gani kwenda eneo gani. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Mahawanga unapokea taarifa.

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaipokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara kupitia Halmashauri zetu iangalie vikundi hivi sababu kubwa inayofanya fedha hazirudi na mpaka impact ya mikopo hii haionekani. Tuangalie zaidi kwenye kuwasaidia hawa wanaopata hii mikopo wengi wao ni wale ambao wanaanza kujiunga kwenye vikundi, wanakosa fursa ya kupata elimu ya mambo ya fursa, ubunifu, utunzaji wa fedha na nidhamu ya fedha sambamba na kufanya biashara kidigitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia sasa hivi imebadilika, kuna vikundi ambavyo havitegemei mikopo ya Halmashauri hivi vimekuwa vikifanya vizuri sana sababu vina uwezo wa kugharamia mafunzo tuna taasisi, mashirika, watu binafsi mengi sana wanaotoa mafunzo kwenye vikundi vya akina mama, tumeona vinafanya vizuri sana, na mpaka wanatoka kwenye vikundi wanakwenda kufungua microfinance na wengine wanafungua kampuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie hawa wajasiriamali wadogo akinamama na vijana ambao ndio wanufaika wakubwa wa mikopo ya asilimia 10, wanashindwa kukidhi haja ya kuingia kwenye mafunzo haya sababu ya kukosa fedha ya kulipia mafunzo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu haya mafunzo yanatolewa kwa kulipia ada siyo bure, kwa hiyo Halmashauri zetu ziangalie namna ya kuweza kulipia mafunzo haya kuviwezesha vile vikundi viweze kupata mafunzo ili vikundi viweze kudumu fedha hii iweze kuzunguka irudi iwafikie wengi zaidi lakini fedha hii ionekane, isiendelee kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto nyingine ambayo inawakuta akina mama na vijana waliokwishapata mikopo, hawa waliweza kufungua viwanda na kampuni zao walipata kazi kwenye Halmashauri zetu na taasisi za Serikali lakini kwenye kulipwa imekuwa ni issue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana na akinamama wamefanya kazi kupitia Halmashauri wanatakiwa malipo yao wanazunguka kila siku kwenda kuomba walipwe, hawalipwi! Kwa hiyo kazi zimesimama vikundi havizalishi tena, fedha ile hairudi matokeo yake vikundi vinakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahamasisha vikundi, tunawakopesha, tunawapa kazi tunashindwa kuwalipa fedha inapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nilikuwa ninataka kuongelea kuhusu mashine za POS ambazo zinatumika na Mamlaka zetu kukusanya mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashine hizi zimekuwa na changamoto na zinasababisha upotevu mkubwa sana wa fedha za Serikali. Changamoto ya kwanza ni watumiaji wa mashine hizi wanapokusanya zile fedha, fedha hizi zinatumika zikiwa mbichi kabla hazijawa banked kwa hiyo hapa ni mwanya mkubwa sana wa upotevu wa hivi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niziombe Halmashauri na Wizara ya TAMISEMI iliangalie hili hasa kwenye kipengele hiki cha kutumika fedha mbichi kabla hazijaenda benki. Hii inasababisha upotevu mkubwa wa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili kumekuwa na adjustment ambazo zinafanyika bila utaratibu, hili nalo ni kipengele kingine kinachosababisha fedha hizi kupotea, mapato ya shilingi 1,000,000 yanafanyiwa adjustment yanaonekana kama yalikusanywa kama shilingi 100,000, shilingi 100,000 inaonekana shilingi 10,000; shilingi 50,000 inaonekana shilingi 5,000 hapa pana upotevu wa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu mashine nyingi za POS zinakuwa offline kwa muda mrefu, sasa tunajiuliza fedha hizi zinakusanywaje au zinakwenda wapi? Halmashauri zetu ziangalie hawa wakusanyaji.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga.

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.