Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuungana na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya kuendelea kutuletea maendeleo Watanzania. Lakini kubwa zaidi nimpongeze kwa jambo hili kubwa la Royal Tour kule Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya nchi duniani zilikuwa zikiamini Mlima Kilimanjaro upo Kenya, lakini kupitia hii Royal Tour anayofanya Mheshimiwa Rais leo hii dunia inatambua kwamba Mlima Kilimanjaro upo Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaipongeza Wizara. Nianze na Waziri mwenye dhamana na Manaibu wake, Katibu Mkuu, Watendaji na Watumishi wote wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Mlimba wameniagiza niwasilishe hoja ya maombi yao ya kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kuwa Wilaya kamili. Kwa sababu mwananchi wa Mlimba inamgharimu kutembea umbali wa takribani kilometa 80 kufuata huduma kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Kwa hiyo, wameniagiza hilo nami nawasilisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu Kituo cha Afya cha Kata ya Chita. Wananchi wa Mlimba tumeanzisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Chita. Katika kituo kile tumeshakamilisha ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), maombi yetu ni Wizara kutusaidia kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali, Mheshimiwa Waziri Ummy akiwa TAMISEMI alitoa ahadi za vituo vya afya kwenye Halmashauri zetu. Na sisi tulipendekeza vituo vya afya viwili, Kata ya Idete na Kata ya Utengule, na hili nakumbusha tu nalo kimsingi kwenye bajeti hii ni muhimu likazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niendelee kwenye suala ambalo limezungumzwa humu ndani, suala la kupanda kwa bei za bidhaa. Limeelezwa humu ndani, nimefuatilia mijadala yote ndani na nje ya Bunge letu lakini pia na majibu ya Serikali. Naomba niseme tu kwa dhati kabisa, haya maswali ya Watanzania ni magumu na majibu yao yanapaswa kuwa yanakwenda kutatua kero zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nimefanya research ndogo tu, unga wa mahindi pale soko la Majengo, kilo 25 hapo awali zilikuwa zinauzwa shilingi 18,000, sasa hivi ni 28,000. Imezidi takribani 10,000. Labda nishauri mambo ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Serikali ingetoa ruzuku kwa bidhaa muhimu, hasa za chakula. Jambo la pili, Serikali ingeangalia namna ya kupunguza kodi hasa kwa bidhaa muhimu na kupeleka kodi kwenye bidhaa ambazo siyo za muhimu kwa mfano bidhaa za vileo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufanya tathmini, bei hizi zina uhalisia? Wasije wakawa wafanyabiashara wengine wana-take advantage kwenye suala la UVIKO na vita ya Ukraine wakapandisha bei maksudi tu. Kwa hiyo, niiombe Wizara ifanye tathmini kutumia Wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya ili kuona kama bei hizi zinaendana na uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu suala la machinga. Machinga ni wachuuzi, ni wafanyabiashara wadogowadogo wachuuzi; machinga hafuatwi, machinga anafuata mteja. Nimeona hapa, ukurasa wa 45 kuna Bilioni Tano za UVIKO zimetumika kwenye kujengea maeneo ya machinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, machinga hawajengewi masoko, tunakosea. Machinga ni mfanyabiashara mchuuzi, ni biashara ambayo ni informal, siyo formal. Sasa ukisema ujenge majengo, mfano Machinga Complex pale Dar es Salaam, nani anakaa pale? Hapa Dodoma mmejaribu tena kujenga, mtakuja kuniambia. Hatuwezi kupunguza watu watakaokaa barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nishauri machinga watengenezewe maeneo rafiki palepale walipo kwa kuboresha. Ukienda Guangzhou, China tutaona wenzetu wanafanyaje. Ukienda pale Dubai ukitoka tu hotelini unakutana na machinga. Duniani kote, miji yote machinga wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kupeleka fedha nyingi kujenga masoko ya machinga, machinga yeye ni mchuuzi anatafuta mteja, hafuatwi na mteja. Ukimlazimisha mteja amfuate machinga tunatwanga maji kwenye kinu. Kwa hiyo, niombe kwa dhati kabisa tuachane na mfumo wa kuwajengea masoko machinga, tuwaboreshee mazingira yao rafiki palepale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijaribu kidogo hapa Dodoma wakati ule kwenye zile barabara. Unatengeneza miundombinu. Kwa mfano kuna watu wa benki, kuna watu wa makampuni ya simu, watengeneze vibanda rafiki ambavyo ni vya muda machinga wakae pale. Lakini pia tuwafuatilie, tuwafanyie tathmini za mara kwa mara. Machinga anatakiwa a-graduate, yaani asiwe machinga miaka yote.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema Lugangira, taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninapenda kumpa mzungumzaji taarifa kwamba tulipata fursa ya kwenda kwenye soko hili la machinga hapa Dodoma na tayari machinga 6,000 wameshajiandikisha, wameridhia kwenda pale kwa sababu wamechoka kukaa juani, wamechoka kunyeshewa mvua. Kwa hiyo, huo ni utaratibu mzuri sana wa Serikali ambao imekuja nao. Kama ilivyo kwenye nchi nyingine nasi tutajifunza jinsi ya kuwafuata pale walipo. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Unaipokea taarifa hiyo Mheshimiwa Kunambi?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sipokei taarifa. Nataka kusema ninathibisha maneno yangu, mtakuja kuwa mashahidi. Tumefanya Dodoma si ndiyo? Tufuatilie kama tutatoa machinga barabarani. Wataendelea kuwepo barabarani, wataendelea kuwepo maeneo yote, watakuwepo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi nikuombe, kwamba machinga hawa waboreshewe mazingira yao maeneo husika. Mheshimiwa Rais amesema wapangwe, sasa sisi tunakwenda kujenga.

Nawaambia, miaka ijayo tutashuhudia machinga hawa wataendelea kuwepo barabarani, maeneo yote ya wananchi. Ahsante. (Makofi)