Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nai pia nikushukuru kwa nafasi hii. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya kututangazia ajira hizi ambazo zinajaribu kutupunguzia gape la watu walioko mtaani na hatimaye kutusaidia kwenye ujenzi wa uchumi na halikadhalika kuwapa fursa Watanzania ya kushiriki ujenzi wa Taifa lao.

Mheshimiwa Spika, nadhani nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye Hotuba, lakini vile vile taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari wiki hii iliyopita. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na msaidizi wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Vile vile niipongeze Serikali kwa ajira hizi mpya kwa sababu tumeona kwamba ajira hizi takribani 32,604 kwa mujibu wa taarifa zinaenda kuigharimu Serikali takribani milioni 26.297 na kwa mwaka ni bilioni 315. Hii ni hela nyingi sana ambayo sasa Serikali inaitoa irudi kwa wananchi na hatimaye isaidie mzunguko huko mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunachokiona ni kwamba itatusaidia kupunguza ukali wa maisha na hatimaye vijana wetu ambao wamekuwa stranded kwa muda mrefu wataweza kupata ahueni halikadhalika waweze kwenda mbele zaidi.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri hasa kwa tamko ambalo amelitoa kuhusu mpango mzuri wa kufanya usaili katika Mwaka huu wa Fedha ambao unakuja hasa suala lile la kuweza kufanya usaili kutokea kwenye maeneo yale yale ambayo wananchi wapo kule. Nayasema haya Mheshimiwa Waziri kwa sababu vijana wetu wamekuwa wanapata shida sana sana kupita kiasi, maana ilikuwa inafikia hatua mtu unajiuliza ni mwakilishi wa wananchi na mbaya zaidi hata hizi interview zimekuwa zinafanyika mara nyingi kipindi Wabunge tuko majumbani hatuko hapa. Walau hata tungekuwa hapa tungeweza kui-feel ile pinch ya kwamba vijana wako hapa. Unaita vijana 3,000 kuja kuwafanyisha interview hapa Dodoma ya kutafuta watu 400 au watu 600. Vijana ambao wamekaa miaka mitano bila ajira, vijana wamekaa miaka minne bila ajira, ila anapoitwa anaona matumaini yanakuja anaingia kwenye mikopo ya pesa, wengine wanauza mali walizonazo wanasafiri kuja Dodoma. Anafika hapa kati ya 4,000 uliowaita ni 300 tu ndiyo watakaochukuliwa au ni 400 ndiyo watakaochukuliwa. Wale vijana wengine 4,600 wanarudi wapi?

Mheshimiwa Spika, wamekuwa wanarudi na masononeko makubwa na mioyo yao inauma kwa sababu wanajiona kwamba hawana bahati, kusoma kwao ni kwa bure. Kwa hiyo ile hali pamoja na kwamba tunao ukali wa maisha ambao tulikuwa tunaendelea nao, ila ile hali ilikuwa inaleta manung’uniko huko mitaani na kuzidi kuleta chuki hata kuzidi kuichukia Serikali. Kwa hiyo mfumo huu ambao tunasema tunauleta leo, vijana wafanyiwe usahili huko kwao itatusaidia kutupunguzia vurugu nyingine ambazo zilikuwa zinatuletea kero kwa vijana wetu. Kwa sababu kama usahili utafanyika na mtu yuko Biharamulo, akafanyiwa usahili pale pale kwake alipo, haingii gharama kubwa sana kwa sababu bado ataendelea na shughuli zake ambazo anahangaika nazo na majibu yakija amekosa atakuwa na matumaini ya kujaribu tena next time.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa najiuliza, kama tunaweza kupeleka mitihani ya darasa la saba, tukapeleka mitihani ya kidato cha nne, tukapeleka mitihani ya kidato cha sita, wakaisimamia kule hatimaye ikarudishwa huku ikasahihishwa. Unamsafirisha mtu hapa ambaye hana ajira muda mrefu, aje tu hapa kufanya written examination haikuwa sawa kabisa. Kwa hiyo tumpongeze Waziri kwa hatua hiyo nzuri ambayo sasa inaenda kutengeneza platform nzuri kwa vijana wetu ili sasa waweze kutoka kwenye maumivu yale ambayo walikuwa nayo, hatimaye waweze kusogea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote yanayotokea, tungeomba sasa watu wa Sekretarieti ya Ajira wajitahidi zaidi, pamoja na kwamba watakuwa wanafanya huu mchujo hebu haki itendeke. Haki itendeke kwa sababu nyie nyote ni Wabunge humu ndani. Tuko Wabunge zaidi ya 390, kila Mbunge anawapiga kura hapa. Hata kama hamsemi lakini lazima meseji za vijana wetu tunazo na vijana wanalalamika. Wengine wanakwambia Mheshimiwa jaribu kutusaidia, ukimwambia kuna mfumo sasa guvu hivi, anakwambia hamna mbona wenzetu wamepitia sehemu Fulani na wamepata. Kwa hiyo kama kuna Wabunge special humu wanao uwezo wa kupita huko tujulishane ili na sisi tuje, lakini kama kuna platform ya haki kwa Wabunge wote, tunaomba huu mchakato ufanyike kwa haki ili vijana wajue kwamba tuko kwa ajili ya kuwawakilisha lakini hatuingilii mchakato wa usaili huko. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba hilo jambo lijaribu kufanyika hivyo ili muweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile tumieni ya first in first out, FIFO itumike Mheshimiwa Waziri. Kwa sababu kuna mtu mwingine kamaliza miaka mitano iliyopita unakuja unaajiri mtu aliyemaliza mwaka jana, kozi ile ile, kwa kigezo gani unamwacha yule kule aliyekuwa amemaliza kipindi cha nyuma? Wakati yule aliyekuwa amemaliza nyuma, hakupenda kutoku-apply ajira ni kwamba Serikali haikuwa imetoa ajira, kwa hiyo alikuwa hana pakwenda. Kwa hiyo fursa inapopatikana leo tumpe aliyekuwa ametangulia nafasi tuendelee kujipanga kwa ajili ya wale ambao wanakuja leo. Kwa sababu umri wa kuajiriwa Serikalini nao unapita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumeona sasa hivi vigezo vingi sana, tumekuwa na vigezo vya miaka 18 mpaka 25 na hili jambo naomba tuliweke wazi hapa. Leo tuseme conditions nyingine ambazo zinawanyima fursa Watanzania tuziache. Katiba ya nchi hii inampa kila mtu haki ya kutokubaguliwa hasa anapotaka kushiriki shughuli za maendeleo za Taifa hili. Sasa unapokuja unatangaza nafasi ya kazi. Mimi nina document hapa, nina tangazo la kazi, hii ni Public Service Recruitment Secretariat tarehe 14 Aprili. Hizi wametangaza nafasi za Ngorongoro Conservation nyingi sana nafasi ziko hapa. Wametangaza madereva, wametangaza na wengine, huku chini sasa kwenye condition; general conditions all applicants must be citizens of Tanzania with age between 18 and 25 years old for certificate and diploma, age 18 and 30 years for bachelor degree holders.

Mheshimiwa Spika, hii sikatai wameweka condition hii, lakini nimerudi kwenye tangazo hapa, hii hapa Pasiansi Chuo cha Wanyamapori. Hiki Chuo ni cha Wizara ya Maliasili na Utalii, age waliyoweka hapa applications za mwaka jana ambao hawa wako shule leo wameweka mtu anayetakiwa aingie chuo miaka 18 mpaka 24. Sasa unajiuliza mtu aliyeingia chuo na miaka 24 labda na miezi 11 au miaka 24 na miezi 10 anamaliza chuo akiwa tayari na miaka 25. Halafu condition ya ajira, wewe huyo huyo unayemiliki Wizara unampa condition ya ajira kwamba huyu mtu asizidi miaka 25. Unajiuliza wewe mwenye chuo unayempa condition huyu umeongea na Wizara kwamba hili darasa lote mtaliajiri muda ule utakaokuwa umeisha? Huna hiyo condition, matokeo yake unaweka condition ambayo inazidi kuongeza maumivu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kitu kibaya zaidi hii hapa wazazi wanalipa, ada milioni tatu, ada milioni nne, mzazi amejihimu kapeleka mtoto pale Chuo cha Wanyamapori. Mtoto anamaliza unamwambia kazidi umri. Chuo kina conditions zake, anayeajiri ana conditions zake. Hili jambo naomba tuliache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni lazima tuwatendee haki Watanzania na tuwape fursa ya kuajiriwa. Kwa sababu hapa wangelikuwa wanafanya vizuri kama wanataka haya masharti ya miaka na nini, wawachukue fresh from school, wawasomeshe wenyewe kwenye kile chuo, wawapeleke tayari, hiyo hawatakuwa na kigezo kingine, lakini wasiache mzazi anapeleka mtoto wake pale, mtoto hujampa condition hiyo, anamaliza chuo, yuko mtaani unaanza kumwambia miaka 25. Miaka 25 anaitoa wapi? Miaka minne hujaajiri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ezra kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe Mheshimiwa Engineer Ezra anachokizungumza ni kweli, siyo tu kwenye maliasili, ajira zote ambazo Serikali inatangaza inaweka vigezo ambavyo vinaengu Watanzania wengi wasiweze kuajiriwa bila kuangalia uhalisia wa umri na lini anamaliza chuo. Siyo kwenye maliasili tu, ni sekta zote ambazo wanatangaza hata kwenye majeshi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mhandisi Ezra Chiwelesa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, labda sasa kwa kumalizia kwenye hili eneo ningeomba kama Bunge, sisi ndiyo tuna nafasi ya kuwasemea vijana hawa wa Kitanzania na wazazi hawa ambao wamepeleka watoto wao. Hii condition naomba tuiangalie upya, ifutike kama ni kusaili waite hata watu 10,000, watafute wawili lakini hawa wawili wanaowataka wawape fursa, kila mtu ajue kwamba nili-apply sikuzuiliwa kuliko hiki kinachofanyika leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na hali nyingine pia tumeiona. Recently, kazi nyingi ambazo zimekuwa zinatangazwa Magereza, Polisi, Uhamiaji, condition mtu awe amepita JKT. Ni lini Taifa hili liliweka kigezo cha kupita JKT? Au ililetwa humu tukakubaliana kwamba sasa JKT kama JKT ndiyo condition turuhusu vijana wetu walioko mtaani waanze kwenda JKT na Serikali itupe nafasi ya kwamba vijana wote walioko mtaani, wataweza kuwabeba kweli? Tukiruhusu vijana wote waliomaliza form four waje wajiunge na JKT tutaweza kuwabeba? Hatutaweza. Kwa hiyo hizi conditions nyingine tujaribu kuzitoa ili tutengeneze fursa sawa kwa vijana ambao wako huko kila mmoja aone na aweze kuitumia nafasi yake kushiriki kwenye kuleta maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)