Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani jioni hii. Awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na upendeleo aliotupatia sisi wanadamu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru sana Viongozi wa Kamati yetu lakini pia Mawaziri ambao wanaiongoza Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Mimi nikiri kwanza ni Mjumbe wa kamati ya USEMI. Mawaziri hawa Dada yangu Mheshimiwa Jenista, Kaka yangu Mheshimiwa Deo Ndejembi na Watumishi wote walio chini ya Wizara hii, wanafanya kazi vizuri na wanatupa ushirikiano wa kutosha. Kwa sababu ya muda naomba niende haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kuishukuru Serikali kwa mambo yote inayoyafanya juu ya watumishi wetu wa umma. Tumeona jitihada nyingi sana zimefanyika ili kuhakikisha hawa Watumishi wa Umma wanafanya kazi katika mazingira very conducive.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wafanyakazi sasa hivi baadhi wamebadilishiwa madaraja, wamelipwa madeni yao ya arrears, madeni ya likizo, matibabu na vitu vingi pia wamefanyiwa re-categorization. Hivyo ningependa sana kuishukuru Serikali kwa kuwa sikivu juu ya hawa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, panapokuwa na mazuri pia mabaya yanaweza yakawepo, nitajikita zaidi kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina raia ambao walikuwa wananchi wa Burundi. Wananchi hawa baadhi yao wamezaliwa Tanzania, wamesomea Tanzania na wanafanya kazi Tanzania. Raia hawa tuliwapa uraia, baada ya kuwapa uraia bado wanaendelea kufanya kazi kwa kibali. Tangu waanze kufanya kazi wengine wameanza mwaka 2003 mpaka leo hii hawa raia wanafanya kazi kwa mkataba. Walisainishwa barua ya mkataba mara moja tu lakini tangu hapo hawajapewa tena barua ya mkataba. Sasa sijajua wanafanya kazi kwa utaratibu upi?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa, ama watumishi hawa wanateseka sana. Hivi ninavyokwambia haki yao kama watumishi ni ile Check Number tu inayowapa mshahara. Hawana haki ya likizo, hawana haki ya pensheni na wakati huo huo kila mwezi wanakatwa pesa za PSSSF. Hawa wananchi hawana haki ya kushiriki kwenye Vyama vya Wafanyakazi lakini hawana haki ya kupata likizo ya uzazi, likizo maalum, lakini hawana haki hata ya kuweza kushiriki kwenye baadhi ya shughuli mbalimbali za Kitaifa kama sensa, sijui uchaguzi, hawana hiyo haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba hawa watu tayari wameshakuwa ni raia wetu, hivyo nikuombe sana Dada yangu, najua Wizara hii ni sikivu na ninyi ni wasikivu, kilio cha hawa wananchi, hawa watumishi wetu kwa sababu tumewakuza wenyewe, wamesoma kwenye vyuo vyetu, wanayo mahitaji yao ya msingi sana, ninaomba Wizara na Serikali iyasikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo wanaomba hawa watumishi. Kwanza wapatiwe ajira ya kudumu, hii ajira waliyonayo haina sustainability. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuna watu ambao walistaafu lakini mpaka leo kwa sababu walikuwa wanafanya kazi kwa mkataba hawajui hata pensheni zao watapa lini, ilihali kila mwezi walikuwa wanakatwa PSSSF inapofika wamestaafu hawana wanachoondoka nacho kama Mtumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo wanahitaji hawa watu ni kupata stahiki kwa wale ambao wameshafariki, wale warithi wao, wajane, wagane, watoto basi waweze kupata stahiki zao ambazo alikuwa anazifanyia kazi huyo Mtumishi wa Umma. Ninakuomba sana najua Serikali yetu ni sikivu sana, kilio cha hawa watu naomba tukisikie kwa mikono miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hili suala nimeshaliongelea sana, najua Mheshimiwa Waziri na tangu akiwa Mheshimiwa Mchengerwa nilishalifikisha sana na Mheshimiwa Jenista nimeshakufikishia na hata Katibu Mkuu Dkt. Ndumbaro nimeshamfikishia. Kwa sababu leo mpo cabinet yote najua kilio cha hawa wananchi kimefika tamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine ni suala la uhaba wa watumishi hasa wa Kada ya Afya. Ni ukweli uliowazi kabisa watumishi wa Kada ya Afya hususani kwenye Majimbo ya Vijijini unasikitisha mno. Kituo cha Afya au Zahanati unakuta ina Mtumishi mmoja tu. Mimi Kata ninayotoka Kata ya Ichemba kuna Zahanati pale Mtumishi mmoja tu ndiyo anafanya kazi pale. Sasa anapokuwa Mtumishi mmoja au wawili kiukweli utendaji wa kazi unakuwa ni mgumu. Mtu huyo huyo ahudumie familia yake lakini mtu huyo huyo anatakiwa ahudumie hawa wananchi. Sasa anapokuwa peke yake kuna mambo yanajitokeza mengi sana ambayo yanaweza kwa namna moja au nyingine yakamsababishia hata akafukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokuambia Mheshimiwa Waziri huko kijijini kwetu kuna utaratibu watumishi wa zahanati wanafanya kazi kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa tena kuanzia saa mbili mpaka saa kumi, kwa hiyo mgonjwa anapopatikana baada muda huo hana msaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia bado kuna unyanyasaji mkubwa sana unaofanywa na hawa watumishi kwa sababu ya uchache wao. Unakuta Mama Mjamzito anapofika pale anaambiwa kwamba hii ni mimba ya ngapi, akisema ya kwanza anaambiwa aende Hospitali nyingine. Lakini anaambiwa hayo ni kwa sababu Mtaalam wa kuzalisha pale hiyo mimba ya kwanza anakuwa pale hayupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hawa wataalam mnaowapeleka huko, utaalam ni ukoje? Haiwezekani huyo mtaalam aliyosomea eti atuwekee masharti kwamba mimba ya kwanza kituo cha Afya, mimba ya pili mpaka ya tatu ndiyo zahanati pale. Hivi haya mafunzo ndiyo wanafanya hivyo kweli? Tunaomba sana hawa watumishi kwenye Kada ya Afya tuwapeleke huko vijijini. Kwenye ajira hizi niombe sana watu wa vijijni tuongezewe watumishi wa Kada ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine ni kuhusu Mishahara na mabadiliko ya mishahara kwa watumishi. Kiukweli watumishi, hata mimi nilikuwa Mtumishi wana manung’uniko makubwa sana. Watumishi wa Serikali takribani miaka mitano iliyopita hawajawahi kupata nyongeza ya mshahara, maisha yao yamekuwa ni magumu sana, gharama za maisha zimepanda, lakini mshahara wao haupandi. Imefikia sasa hivi hata tamaa ya kufanya kazi imekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nimeshuhudia huko kwangu Mfanyakazi ana-bet, ukiuliza wanakuambia hali ngumu ya maisha. Wafanyakazi wanakopa mpaka songesha, wanakopa vikoba hebu ifikie mahali hawa wafanyakazi tuwaonee huruma jamani wana maisha magumu, mfumuko wa bei unawahusu, kodi, nyumba kila kitu matibabu jamani tuwaonee huruma hawa wafanyakazi, this time tuwaongezee mshahara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni matumizi mabaya hasa ya ubadhirifu wa fedha. Sifa mojawapo ya mtumishi wa umma ni kuwa muadilifu katika kazi anayoifanya lakini wafanyakazi walio wengi tunaona wana ubadhirifu mkubwa sana wa madaraka yao. Hapa juzi kuna crip ime- trend sana hapa ya temporary offices, hivi kweli mtu anatumia milioni 100 kwa kujenga temporary office kiasi kwamba mpaka Waziri Mbarawa anawaambia TAKUKURU fanyeni kazi. Ina maana huyu mtu mpaka Mbarawa anasema TAKUKURU wafanye kazi hakuna means nyingine zilizomwangalia mpaka amefikia kufanya ubadhirifu wa kiasi hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ninachoshangaa hawa wanaofanya ubadhirifu hivyo, hatuoni hatua za makusudi zikichukuliwa dhidi yao. Tunaona wengi akishagundulika na tatizo anaweza akahamishwa kituo, anatolewa kituo A anakwenda kituo B. Hivi huyu ameshakuwa ni mwizi kwanza ukimtoa kituo A ukimpeleka kituo B ndiyo ataacha wizi? Huo wizi ataendeleza. Kwa hiyo, kuwahamisha sioni kama ni solution ya hawa wanaofanya ubadhirifu wa mali za wananchi. Wananchi wanalipa kodi kwa shida, maisha ni magumu halafu wao tu wanapiga, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri kwa hao wanaofanya hivi, nafikiri hatua kali zichukuliwe dhidi yao. Isiishie tu kumsimamisha kazi au kumfukuza kazi; iendelee aidha, wafungwe jela au hata wafilisiwe mali zao. Hivi mimi Rehema hapa nimekaa najua kabisa nina mchongo wa maana ambao najua mwisho wa siku nitasimamishwa tu kazi au nitafukuzwa kazi, si nitaiba? Nitaiba, halafu najua kabisa mwisho wa siku nitafukuzwa kazi lakini tayari nimeshatengeneza mchongo wa maana fedha ya maana. Kwa hiyo, akifikiria fedha yake ya kustaafu ni ndogo kuliko huo mchongo, nafikiria tuongeze adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.