Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona nami niweze kuchangia baadhi ya masuala ya Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ameweza kunisimamisha mimi hapa pamoja na Wabunge wenzangu tukiwa salama.
Pia napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wangu, Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na hata sasa naamini kabisa huko aliko anatufanyia kazi na anatutendea haki kabisa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Temeke kwa madarasa tuliyopata, ni madarasa mengi sana na ukizingatia kwamba Temeke tunazaliana sana lakini ameweza kutupa madarasa mengi ambayo sasa mabinti pamoja na wavulana hakuna second selection; wote wamekwenda Form One kwa pamoja. Hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata zahanati kila Kata na tumebakiza Kata mbili ambazo ninaamini Kata hizi kwa bajeti inayokuja tutapata. Vifaa ambavyo vimekwenda katika hospitali zetu, kweli ni vya maana sana na sasa tunaringa sana Temeke kwa jinsi ambavyo tunapata tiba za uhakika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amewapa uwezo Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora, mdogo wangu Mheshimiwa Jenista pamoja na mdogo wangu Mheshimiwa Deogratius, kwa kweli kazi mnaifanya na tunashukuru sana, hakika hata sisi tunajivunia ninyi kuwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenda tu moja kwa moja kwenye Jimbo langu la Temeke, hasa wafanyakazi wa Bandari. Wafanyakazi wetu wa Bandari kipindi kile wengi mliweza kuwasimamisha kwa sababu walikuwa na elimu ya Darasa la Saba, wengine walikuwa wamegushi vitu vingine. Hata hivyo mliwapa namna ya kuweza kujifunza au kujiendeleza ili waweze kuajiriwa tena. Wako baadhi ambao tayari kwa kweli nawashukuru sana waliweza kujiendeleza na wakaweza kuajiriwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo moja la wengine ambao hawakuweza kwenda kujiendeleza na sababu kubwa tunapoongea nao wanasema kwamba pesa ambazo walitamani mngekuwa mmewalipa kipindi kile walipoachishwa kazi wangeweza labda kuzitumia kujiendeleza, lakini mpaka sasa fedha zao hazijalipwa, wala hawajui lini watalipwa fedha hizo kwa sababu wametumikia Bandari muda mrefu sana. Pia walitamani wao wenyewe kwamba kama kweli, basi walikosea na hawakuweza kujiendeleza, lakini wanaomba sana wapate hata mafao yao waweze kuondoka ndani ya mji waliokaa hasa kule Temeke. Wakati mwingine wanaomba hata kuajiriwa mahali pengine, lakini umri umewatupa mkono, hawawezi kuajiriwa tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wizara hii iwaangalie hawa watumishi wa Bandari ambao wako kama 196 hivi kama sikosei, muwaangalie upya waweze kupewa fedha zao ili waondoke ndani ya miji hii na kurudi vijijini kwao kuendelea na maisha mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hawa wameshatufata mara nyingi, hata mdogo wangu Mheshimiwa Jenista ameweza kuongea na baadhi na kuliangalia hili jambo, naamini sasa kwa kusema kwangu, nao watasikia, kwa kweli mtawatendea haki ili waweze kurudi makwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko Bandari; wako madereva ambao wanaendesha magari yale makubwa. Siyo madereva tu wa yale magari makubwa, lakini naamini hata madereva hawa ambao wanaotuendesha, labda wanaweza wakawa wanawaendesha hata nyie viongozi wangu mlioko hapo; mishahara yao wanalalamika sana kwamba ni midogo sana, kiasi kwamba hata leo unapompa Dereva gari lile V8 kwa thamani yake na kumwendesha labda Waziri Jenista aweze kufika salama mahali anapokwenda kufanya kazi, hakika anakuwa amebeba mzigo mzito sana. Kwanza gari lilivyo na thamani, lakini pia utu wa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, naomba sana mwangalie upya mishahara yao. Tuone kwamba kazi wanayoifanya inalingana kidogo na mshahara wanaoupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa siyo mkaaji sana kwenye vijiwe lakini nimependa sana wakati wote kuwa ndani ya vijiwe vya wale madereva wa malori kule Bandari. Madereva wetu wa malori, inawezekana ni malori ya Serikali lakini pia ni malori ya wanafanyabiashara binafsi lakini. Mara nyingi nakuwa napita katika vijiwe vile, nakaa, naongea nao na wale Madereva kwa kweli wanalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wanasema unampa gari ambalo labda ni Scania la thamani kubwa sana, ameweka mzigo wa thamani kubwa sana, anaondoka nao hapa Tanzania kwenda nao labda Rwanda, Burundi, lakini mshahaara wanaopokea ni mshahara mdogo sana ambao utaona mara nyingi malori yetu yanakaa njiani, yanapaki njiani kwa sababu fedha uliyompa aweze kuacha nyumbani, lakini pia hiyo hiyo fedha aweze kujikimu yeye mwenyewe. Kwa hiyo, unaona wengi wanalala ndani ya magari yao katika baadhi ya vituo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia muwaangalie. Labda mtengeneze namna ya kuweza kuwafikia wale wenye magari makubwa, wafanyabiashara wakubwa wenye magari yao hayo ili mwone mtawasaidiajie hawa, kwa sababu huu ndiyo utawala bora ambao mama anataka. Hawa madereva nao ni wafanyakazi, ndiyo utawala bora unaohitajika uwaone nao wako katika utawala bora unaoelekezwa katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, ninaamini mnasikia na mtakaa na waajiri wao muone wanafanyiwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kuhusiana na Walimu. Walimu wetu pia ni waajiriwa, nao wanatamani kuwa katika utawala bora. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ameweza kujenga madarasa mengi sana nchi nzima, lakini Walimu wetu wanapotoka madarasani kufundisha wanakosa ofisi za kukaa. Ofisi zao wanaweza kutumia labda darasa ndiyo wakafanya ofisi na mahitaji yao ni madawati yale ya shule ndiyo wanafanya meza zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hili linakwenda kwa Waziri wa Elimu, lakini nilikuwa naanzia hapo kwa sababu ya utawala bora, kwamba sasa Walimu hawa wapate namna ya kukaa vizuri ili wanapotoka madarasani, basi wanavyokuja kusahihisha madaftari yale, wakae mahali salama ili wanafunzi wetu ambao tumewawekea madarasa nao wahudumiwe vizuri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Ni kengele ya pili.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)