Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima. Pia nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanyia Taifa hili. Tumeshuhudia miradi kemkemu imeingia ndani ya Wilaya ya Hai na nchi nzima. Kubwa ni hili la filamu ya Royal Tour ambayo imefanyika. Uzinduzi huu kule kwetu Hai tayari tumeshaanza kuona matunda. Watalii wameongezeka kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na Katibu Mkuu, Dkt. Ndumbaro na watumishi wote kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri, kule Hai wanakuita wewe ni mtu bingwa sana. Wanakuita mtu bingwa kwa sababu pale Hai Rundugai tulikuwa na chuo cha ufundi, kilijengwa miaka 11 kikatelekezwa pale. Nilipokuja kwako nikakuomba, umetuletea fedha na kile Chuo cha Rundugai kinajengwa sasa hivi. (Makofi)
Vilevile wewe ni mtu bingwa kwa sababu Kata ya Bondeni kulikuwa hakuna kituo cha afya, wala zahanati. Kupitia TASAF umetuletea fedha pale, tunaenda kujenga zahanati pamoja na vifaa tiba. Nakushukuru sana. Hizi ni sambamba na kumshukuru Mkurugenzi wetu wa TASAF kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya USEMI, tumetembelea Zanzibar, tumetembelea Tanzania Bara huku, tumeona ufanisi (value for money) kwenye miradi. Nazungumza kwenye eneo la miradi, sijazungumza kwenye ile ruzuku wanayotoa kwa wananchi. Kwenye eneo la miradi kwa kweli wanafanya vizuri sana. Kama kuna eneo la kwenda kujifunza, TAMISEMI wanatakiwa waende wajifunze hapa kuona namna ambavyo miradi hii imekuwa sahihi. Hayo makofi unayoyasikia ni ya Wajumbe wenzangu wa USEMI tumeona miradi inavyotekelezwa vizuri na TASAF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, naomba niende moja kwa moja kwenye kuchangia hoja yetu. Nianze kwa kazi kubwa ambayo Mei Mosi watumishi wa Umma nchini wanategemea kusikia jambo moja tu, ongezeko la mishahara. Naomba sana, ninafahamu hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais mwenyewe, lakini nawe Waziri mfanye mfanyavyo, Mei Mosi hii watumishi waongezewe mishahara pamoja na kupandisha kima cha chini. Sababu za kuwaongezea mishahara, wanafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, naomba sana hilo kwa kweli mwaka huu tujitahidi ili kazi iweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kushauri kuhusu Muundo wa Utumishi wa Umma wa Mwaka 2002. Nadhani kuna haja ya kufanya marekebisho kwenye maeneo kadhaa. Moja ya eneo hili ni zile sifa zinazomtaka mtumishi kupandishwa cheo. Wako watumishi ambao kwenye kada tofauti wanatakiwa waende shuleni, wakasome na wafaulu ndipo wapandishwe cheo. Wakati kuna kada nyingine hicho kitu hakipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano kwenye kada ya Maafisa Tarafa na Maafisa Tawala, nafahamu zipo na kada nyingine. Ukienda kwenye ule Muundo wa Utumishi wa Mwaka 2002, sifa za kumpandisha Afisa Tawala kutoka Daraja la Kwanza kuwa Mwandamizi, moja ya sifa inayotakiwa, anatakiwa akafanye mtihani unaitwa Qualified Examination Test. Ukisoma kwenye kanuni hii inasema, siyo tu kufanya mtihani, anafanya mtihani halafu afaulu ndiyo apandishwe daraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili kwanza linaleta tofauti kwenye Utumishi wa Umma. Kuna kada nyingine hazifanyi, kuna kada nyingine zinafanya. Pia hebu tupime umuhimu wa mitihani hii. Mimi nimefanya huu wa Maafisa Tawala, unaenda pale umetoka kazini; hili linawasumbua sana watumishi wa kada zile. Kwanza Serikali yenyewe haiwalipii kupata hicho kibali cha kwenda kufanya mitihani hii. Ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, mtu anaacha kupanda daraja tu kwa sababu hakuruhusiwa kwenda. Pia hana hela ya kwenda kulipia mitihani ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kulipia na kujitahidi kufanya hivyo, akienda darasani, mtu huyo anaenda kusoma vitu vingine tofauti. Mtu amesoma degree ya kwanza, degree ya pili, halafu unampeleka katikati ya utumishi wake, ameshakaa zaidi ya miaka mitano huko mtaani, aende akafanye mitihani ambayo ni administrative law, anatakiwa kwenda kumeza madude pale, ajibu kwenye mtihani na afaulu, lakini lina-embarrass sana watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtumishi anaomba ruhusa kwa Mkuu wake wa Mkoa, anaaga kwamba anaenda kusoma, anafika kule bahati mbaya anafeli, akirudi huku mtaani hapakaliki. Wewe fikiria Afisa Tarafa anaenda kwenye mtihani huo, anaaga Kata zote zinajua bosi kaenda kwenye mtihani. Anaenda kule anakwama, anarudije kufanya kazi? Naomba, kama ni muhimu sana, basi kile kipengele cha kufaulu kifutwe. Waende wafanye kama refreshers course, lakini kusiwe na kigezo kwamba lazima afaulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye eneo lingine kuhusu madeni ya watumishi. Ni kweli Serikali inalipa, lakini bado watumishi wanadai. Mheshimiwa Naibu Waziri, wewe ulikuja kule Hai, uliona wale wamama wanatulilia na kila siku wanatuma jumbe, wanapiga simu. Wamelipwa kiwango kidogo sana. Naomba ifike mahali madeni ya watumishi hawa myamalize. Fanyeni kazi hii mhakikishe tunamaliza, siyo jambo zuri, mtu ameshatutumikia vizuri, amemaliza utumishi wake wa Umma, bado tunaendelea kumsumbua na madeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na pesa yao ya kustaafu, wanazungushwa mno wanapodai. Bahati nzuri na Spika naye amekuwa akilipigia kelele hili. Mtu anakuwa kwenye Utumishi wa Umma, Serikali imetumia fedha nyingi kufanya data cleaning, kwa hiyo tunaamini taarifa za watumishi ziko safi. Sasa anapostaafu unaenda kumdai taarifa, zipi tena wakati unazo wewe? Tayari tuna mifumo ambayo inachukua taarifa zao? Naomba hili na lenyewe tulishughulikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mafunzo elekezi; kwenye Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinazungumza mtumishi kabla hajaingia kazini apewe mafunzo elekezi. Naomba Serikali itenge fedha ya kutosha kwenye eneo hili na kazi hii wapewe Chuo cha Utumishi wa Umma. Tunaenda kuwalaumu watumishi kwa sababu hatukuwafundisha vizuri na ni kinyume na sheria ili mtumishi aajiriwe, tuhakikishe lazima aende apate mafunzo ili aingie kazini akijua ni jambo gani anaenda kulifanya. Hili ni pamoja na viongozi wote, hata viongozi wa kuteuliwa ni muhimu sana wakapata haya ili kuepuka mambo ambayo hayafai ya kinidhamu yanaoendelea kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze pia kuhusu e-GA. Nawapongeza sana e-GA. Tulienda kutembelea pale tukaona vijana wa Kitanzania wamechukuliwa kutoka nchi mbalimbali walikokuwa wanasoma, wamekusanywa pale; na wale ambao bado wako mashuleni wanakuja kufanya mafunzo kwa vitendo pale. Kwa kweli hili jambo la kizalendo tunawapongeza sana. Bado naendelea kuwasisitiza, mifumo hii iunganishwe iseme, izungumze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda hapa Dodoma Jiji kulipia kiwanja chako, utakaa hapo masaa mawili au matatu; na wakati mwingine unaambiwa mtandao umeshuka, mtandao sijui umefanya vitu gani. Hii siyo sawa, watafute backup ya kudumu. Tumesema kwenye Kamati lakini narudia humu tena kwamba hii mifumo tunayoitengeneza tuwe na backup ya hakika. Serikali inapoteza pesa nyingi, lakini tunawasumbua wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe ukienda hapo Dodoma Jiji sasa hivi utakuta foleni ya kutosha pale. Jambo hili halifai, Serikali inakosa pesa kwa sababu ya kukosa backup. Kwa kukosa backup inatoa mianya ya watu kuweza kucheza na hii mifumo na kutumia fedha za Serikali. Mfano, mfumo wa GoT-HoMIS ukienda kule umeme ukizimika hawana backup ya kuweza... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)