Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wabunge wanne ambao wameingia safari hii baadaye, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mheshimiwa Lucy Owenya na Mheshimiwa Ritta Kabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali. Hakuna kitu ambacho kinanikera kama kuendelea kufanya vibaya kwa timu zetu za Taifa, juzi niliuliza swali Mheshimiwa alijibu, lakini nataka kumshauri leo. Bahati nzuri nimekuwa mchezaji kwa ngazi ya juu kabisa, nimekuwa kwenye Baraza la Michezo, Mjumbe kwenye TFF, nimekuwa Kapteni wa timu wa Bunge lililopita, na sasa hivi ndiye kocha wa timu ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nashauri, kwa kuwa nilipokuwa kwenye Baraza na nina hakika kuwa Baraza letu linajiendesha katika mazingira magumu sana. Hakuna fedha ya kutosha ambayo inapelekwa pale, lipo pale kwa sababu lipo kisheria na sidhani kama linafanya kazi yake kama inavyotakikana. Nimekuwa TFF mzigo ni mzito nitatoa ushauri baadaye kwamba iweje kwa timu ya Taifa. Kwa kuwa Baraza la Michezo lina vitu vingi, michezo yote iko mle pamoja na wasanii wapo mle ndani. Ninapendekeza tuunde Shirika la Michezo. Ukienda Uingereza baada ya kugundua kwamba baadhi ya michezo haifanyi vizuri walianzisha Shirika la Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuanzisha shirika la michezo badala ya baraza ni kwamba itakuwa rahisi kujitengemea, litakuwa linakaguliwa kama kawaida na Serikali/CAG, lakini litafanya kazi vizuri kuliko sasa kwa sababu sasa hivi halina fedha lakini tutakapounda shirika itakuwa rahisi wao kufanya mambo mengi. Kwa mfano, wanaweza wakatafuta kwenye harambee, wanaweza kuwa na vyanzo vingine vya mapato na hivyo itakuwa ni rahisi sana kuzihudumia hizi timu za Taifa. Leo kuna kuna mashindano ya olympiki, wakimbiaji wako Arusha, sijui wako camp, hawana fedha wanapata shida. Timu ya Taifa inaachiwa na TFF, TFF wanapata wapi pesa? Kwa sababu kiingilio kile nilitegemea makato ya ile kodi ingerudi baadaye ikasaidia kwenye timu ya Taifa. Lakini tunataka tu tuone timu ya Taifa inafanya vizuri bila kuipa support, hii ni pamoja na michezo mingine. Mheshimiwa Waziri ninashauri tuanzishe Shirika la Michezo, hapa ndipo utakapoona tofauti. Leo ni miaka mingapi hatujafanya vizuri?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri pia kuhusu timu ya Taifa. Ili timu ya Taifa ifanye vizuri ninashauri TFF najua wapo, idadi ya wachezaji ambao wanatoka nje, wanaoruhusiwa kuchezea vilabu vyetu vya ndani ni wengi mno kiasi kwamba leo ukienda timu ya Yanga wanaoongoza kufunga magoli ni wachezaji wa kutoka nje, ukienda timu ya Simba wanaoongoza kufunga magoli ni wachezaji wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lake ni nini, ukiangalia ligi ya Uingereza ndiyo ligi bora ninaamini kuliko ligi nyingine na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa nje. Lakini timu ya Taifa ni mbovu sana kwa sababu wanaocheza ligi ile ni wageni, kwa hiyo na sisi tunanufaisha tu timu za Simba na Yanga lakini uwezo wa kunufaisha Taifa kwa kutumia wachezaji wengi wa nje itakuwa ni kizungumkuti, hatutafanya vizuri hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri wa Kazi Mheshimiwa Mavunde yupo, hebu kapitie mikataba ya wachezaji wetu kwenye vilabu vyao, kwa sababu tofauti ya mshahara ya wachezaji wa nje na wachezaji wetu inakatisha tamaa. Ukienda pale wale watu unaweza ukafikiri labda wanafanya mgomo lakini wameshakata tamaa kiasi kwamba wanaona afadhali basi hawa wanaolipwa fedha nyingi ndiyo wacheze wenyewe. Sasa nafikiri Mheshimiwa Waziri pita pale kagua ile mikataba yao utaona kinachoendelea pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nigependa nishauri ni kwamba vilabu vyetu vinachukua muda mrefu sana kufanya uchaguzi na hii ni pamoja na mikoa. Mimi natoka mkoa wa Iringa, tunapokea malalamiko mengi sana kutoka kwenye klabu za Lipuli na klabu ya mkoa wa Iringa kwamba chaguzi hazijafanyika. Kwa hiyo, ningeomba taratibu zifuatwe kama ni Baraza la Michezo la Taifa au ni Mabaraza ya Mikoa yasimamiwe yahakikishe chaguzi zinafanyika kwa sababu hapo ndipo ambapo vurugu inaanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kushauri ni jinsi ya kutenga siku maalum. Mheshimiwa Rais ametenga siku maalum ya usafi, sasa Mheshimiwa Waziri wa Michezo, kuna haja kabisa ya kuangalia kama nchi zingine, mfano ukienda Burundi, Congo na sehemu zingine wana siku maalum ya michezo na hii tungeanza Wabunge kwa sababu michezo ni afya, michezo ni dawa na michezo ni tiba. Tukifanya hivyo tutawafanya na watu wengine wakaona umuhimu wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni academy, lazima tuwe na academy. Sisi wakati tunacheza wakati huo tulikuwa tunatumia zaidi michezo ya shule za sekondari, vyuo na mashirika. Lakini ukiangalia hii michezo sasa hivi imekufa kabisa, zile ndizo zilikuwa academy. Leo ukianzisha academy unapata wapi vifaa, uwanja ule wa bandia ambao kodi yake na ununuzi huwezi ku-afford, vifaa vya michezo bei ziko juu, sasa bila kufanya hivyo matatizo yake yatakuwa ni makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wasanii ni vema kama nilivyosema tukiwa na shirika la michezo na wasanii waatakuwa ndani, itakuwa rahisi kuwasimamia haki zao. Wanadhulimika sana, wanafanya kazi kubwa lakini haki zao hazitambuliwi. Tumeshuhudia wacheza filamu, filamu zao zipo mitaani, wanachopata wao hakuna, ni shida tupu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba kabisa hebu kaa na watu wako muweze kuona mnawasaidiaje wasanii na wanamichezo wa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kwa sababu muda bado ninao mimi nilikuwa Rais wa wacheza mpira Tanzania, chama kinaitwa Spurtanza (Chama cha Wachezaji Mpira). Mimi nigekushauri jaribu kuwatumia wale wachezaji tungeweza kuwatawanya kwenye shule za msingi hata kwa posho kidogo wangeweza kusaidia kufundisha michezo na ingekuwa ni academy tayari. Wapo wengi, anapomaliza kucheza mpira mchezaji wa Tanzania wengi maisha yao ni shida, lakini tayari wanakuwa wameshafikia level ya Taifa, kwa hiyo automatically wanakuwa kwenye level ya coaching ya mwanzo, ni kiasi cha kuwaendeleza tu. Kwa hiyo wangetumika kwenye shule zetu za misingi wangesaidia kubadili michezo kwenye nchi yetu kwa baadhi ya michezo kama mpira wa miguu, riadha,ngumi na kadhalika, badala ya kusubiri academy ambayo kwa kweli ni gharama kuziendesha na Serikali bado haijatia nguvu labda wakiamua kuweka ruzuku kwenye michezo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba Mheshimiwa Waziri, pesa hizi ulizoomba ni ndogo hazitasaidia kitu chochote. Hizi ni za semina na mambo mengine, lakini kwenye mambo ya michezo sahau kama kutakuwana mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.