Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kupata nafasi ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ambayo mimi nasema ni wizara nyeti sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumeanza kuchangia jana mpaka leo imetolewa michango mingi yenye umahiri na weledi mkubwa sana hasa kwa upande wa masuala ya utumishi. Na katika michango hiyo pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumebaini jinsi ambavyo kazi kubwa imefanyika katika kurekebisha suala zima la utumishi wa umma na kuwajengea watumishi mazingira mazuri ya kazi na matumaini ya kuendelea kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika hili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, kazi waliofanya ni kubwa na Watanzania wameiona. Lakini kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu wizara hii iko chini ya ofisi yake, kwa hiyo haya yote yaliyofanyika yana m-reflect yeye mwenyewe, jinsi ambavyo amekuwa mtu wa kujali na jinsi ambavyo amekuwa mtu mwenye nia ya kuifikisha nchi yetu mahali pazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nichangie upande wa utawala bora kwa sababu ni jambo ambalo ni cross cutting, linakwenda kila Wizara. Hawa watumishi tunaowazungumzia popote pale walipo wana wajibu wa kutumika kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na hakuna taasisi wala idara yeyote ambayo inaweza ikafanya kazi nje ya mfumo wa utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili kwanza nitambue jinsi ambavyo tumefanya vizuri, na si kwa viwango vyetu sisi, tumesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba tumepanda ngazi katika kiwango cha Corruption Perception Index na hata kwenye Rule of Law Index tumepanda. Sasa tathmini hizi ambazo zinafanywa na mashirika ya kimataifa yaani hakuna namna ya kusema kuna mtu amejipendelea hapo, zimefanyika kwa viwango vya kitaaluma na kitaalam, kwa hiyo tunastahili kuipongeza Serikali kwa hilo na pia sisi wenyewe kujivunia kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora katika nchi ambayo ina katiba iliyoandikwa (written constitution) unaanzia na kuishia kwenye utawala wa sheria; yaani utawala ambao kila mtu, ikiwa ni pamoja na dola yenyewe, inapaswa kutenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na kwa kutii sheria, hakuna aliye juu ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia sheria si kila sheria ni sheria, kwamba hata zile za wakati wa Idi Amin anaamka kule kwake anasema leo weka watu hawa kwenye karandinga tukawatupe baharini nayo ni sheria hapana. Sheria inayozungumziwa katika utawala wa sheria ni ile sheria ambayo imetungwa na chombo halali kama sheria zetu ambazo zinatungwa na Bunge hili, na imetungwa kwa mfumo wa uwazi ambao inashirikisha hata wadau kupata maoni ya wadau na kadhalika kwa mfumo ambao ni shirikishi, na ni sheria ambayo inaweza kutumika kwa ajili na dhidi ya mtu yeyote yule hata dola yenyewe kama ambavyo nimekuwa nikizungumza; na pia ni sheria ambazo zinaendana na misingi ya haki za binadamu, ile misingi ya kimataifa; na katika hili bado tumefanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili bado tumefanya vizuri kwa nini nasema tumefanya vizuri. Mwaka 1984 Bill of Rights ule mkataba wa Haki za Binadamu uliingizwa katika Katiba yetu, baada ya hapo ikatokea kipindi karibu cha miaka 10 ambapo Idara mbalimbali zilianza kurekebisha Sheria zao ili ziendane na Bill of Rights na pale ambapo hawakufanya hivyo wananchi binafsi waliweza kufanya hivyo kupitia Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka kesi kama ya Daudi Pete ambayo ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Dhamana, mtakumbuka Sheria ile ya Government Proceedings Act ambayo ilikuwa inakataza wananchi kuishitaki Serikali mpaka wapate kibali cha Waziri wa Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 kuna mtu mmoja ni Mwalimu anaitwa Peter Ng’omango alikwenda Mahakamani wakaifuta ile Sheria. Ilipofika mwaka 1994, Bunge hili likaona sasa tuwarahisishie zaidi wananchi kazi kwamba wanapotaka kurekebisha sheria siyo lazima waende wakaishambulie ile Sheria Mahakamani kwamba inakiuka Katiba, ikatungwa ile Sheria ya Basic Rights and Duties Enforcement Act, ambayo kwa mujibu ya Sheria ile ya Mwaka 1984 nafikiri ni Sheria Na. 33, mtu yeyote ambaye haki yake imenyimwa au anaona kwamba haki yake itanyimwa ana haki ya kwenda Mahakamani na akaipinga ile Sheria na ile Sheria ikafutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sheria hii imetumika kurekebisha Sheria nyingi sana ambazo watu walikuwa wanaona zinawanyima haki na hata juzi juzi kesi ambayo bado nadhani iko kwenye mawazo ya watu ni kesi ya Ndugu Rebecca ambapo alikwenda Mahakamani kupinga vile vifungu vya Sheria ya Ndoa ambayo ilikuwa inaruhusu watoto wa kike kuolewa chini ya umri na ile sheria Mahakama ikaitamka kwamba inakiuka Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba Katiba yetu, Sheria zetu na mifumo yetu iko ambayo inatuwezesha kupata haki zetu kwa mujibu wa Katiba, lakini tatizo linakuwa wapi? Tatizo ninakuwa uelewa tu ndiyo tatizo. Kwa hiyo, tunapopanga bajeti zetu na kuleta hapa Bungeni ni vizuri sana tukazingatia suala la training na kujenga uelewa kwa upande wa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya zile bajeti zinazopita kwenye Kamati yetu ya Katiba na Sheria kwa kweli tuling’ang’ana sana na walioleta bajeti kwamba jamani bajeti ya training ni ndogo, bajeti ya mafunzo ni ndogo mambo ya kujenga uelewa, wakati ule tunaambiwa ni ukomo wa bajeti, nafikiri sasa ukakomoe maeneo mengine tusikomoe suala la training ambalo kwa kweli ni muhimu sana. Unaweza ukawa na sheria nzuri, unaweza ukawa na Katiba nzuri lakini kama watu hawaifahamu na hawaifahamu jinsi ya kuitumia kufikia haki zao inakuwa unafanya kazi bure, unakuwa na karatasi za bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Waheshimiwa Wabunge ni vizuri tukajengewa uwezo kwenye maeneo ya kimkakati ili tunapokwenda kwenye mikutano ya hadhara tuweze kuwaelimisha watu wetu ili waweze kujua jinsi ya kufikia haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo madogo mdogo ambayo yanawakerakera wananchi ambayo kama tu mafunzo yangekuwa yanafanyika kwa wananchi wenyewe na kwa wale Watendaji tusingekuwa na tatizo. Kwa mfano, mtu anakwenda anataka dhamana ana kitambulisho cha Taifa cha NIDA ambacho kimepatikana kwa mifumo ya hali ya juu lakini anaambiwa kalete barua ya Mtendaji. Sasa anakwenda kufuata barua ya Mtendaji anakuta Mtendaji siku hiyo kafiwa kaenda mazikoni, anarudi anakuta OCS ameshaondoka, mtu analala ndani bila sababu wakati kitambulisho cha Taifa kimejitosheleza kufanya hiyo kazi. Wengine wanaofanya hivyo ni kuelewa awaelewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dhamana unaambiwa kalete barua ya mtu ambaye ameajiriwa Serikalini. Sasa upo pale umekamatwa, uende ukatafute mfanyakazi wa Serikali, by the time unarudi muda umeisha mtu anakosa dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu pale kuna jambo moja lilitokea hapo ni la kuchekesha tu ambalo ni lakusikitisha kwa kweli, kwenye Kata ambazo zilishambuliwa na Tembo, Kata ambazo zina matatizo ya Tembo Kata ya Kwakoa, Kigoligoli na Toloa walikwenda watu kulipwa kifuta jasho, sasa anakuja mtu anakitambulisho kimeandikwa kwa mfano Zaituni Athumani Mbarouk, sasa lile jina lilivyochapwa huko Wizarani kuletwa kwake limeandikwa Zaituni Athumani Mbaraka anaambiwa sasa nenda kaape Mahakamni kubadilisha hii Mbarouk na Mbaraka ili upate hela yako, wanakwenda kuapa Mahakamani anarudi tayari watu wameshaondoka na mpaka leo hawajarudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mengine ni uelewa tu wa hawa tu ambao kwa kweli kama wangepewa mafunzo, wakajengewa uwezo, nadhani kwamba tusingefika hapa, haya matatizo madogo madogo tungeyaondoa, tunaweza tukawekeza kwenye haya makubwa tuka-shine tukapata na sifa, lakini haya madogo ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)