Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia kwenye hotuba hii ya Utumishi. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha promotion kwa wafanyakazi wote nchini kwa bajeti tatu mfululizo kwa maana ya 2018/2019, 2020/2021 na 2019/ 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia leo habari ya watumishi, sitapenda kuacha kutoa pongezi nyingi sana kwa Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na harakati zake za kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ya kwamba anawasemea watumishi na kutetea maslahi ya watumishi nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na kaka yangu Mheshimiwa Ndejembi, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia mambo machache sana kwa siku ya leo. Wamezungumza hapa suala zima la mafao, sitataka kulirudia, lakini nataka nikazie tu kwamba, hata kwenye Jimbo langu la Msalala, suala zima la mafao kwa wastaafu limekuwa ni changamoto kubwa sana, hasa kwenye familia ambazo wamepoteza watu wao ambao wanastahili kupewa hayo mafao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatolea mfano leo kwenye Kata ya Burige kuna mama mmoja alifiwa na mume wake Mtendaji wa Kijiji, leo hii tunazungumza ni zaidi ya miaka kadhaa sasa, bado hajapatiwa mafao ya mume wake ili yaweze kumsaidia katika harakati za kusomesha watoto wake na kulea familia yake. Kwa hiyo, naendelea kuomba na kusisitiza Wizara waone namna gani wanaweza kuboresha mfumo huu wa mafao ili wastaafu waweze kupatiwa mafao yao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua hapo zamani tulipokuwa na Mfuko wa LAPF na PSSF tunaona changamoto hizi zilikuwa ni chache sana, lakini sasa baada ya kuundwa mfumo huu changamoto zimekuwa ni kubwa sana. Kwa hiyo, naendelea kumwomba dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kuhakikisha ya kwamba wanalitilia suala zima la mafao ya wastaafu waweze kupata kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuzungumzia suala zima la upungufu wa watumishi. Katika Jimbo langu la Msalala tuna upungufu wa watumishi takribani 500. Kama alivyochangia Mheshimiwa Mbunge mwenzangu hapo, kwamba sisi tunaotoka katika Majimbo ya vijijini, hali ya mazingira katika maeneo yale ni ngumu sana. Watumishi hawa wanaishi katika mazingira magumu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao upungufu mkubwa wa watumishi, wengi wao wanahama katika maeneo yale kutokana na mazingira magumu ya pale. Siungani na Mheshimiwa Tabasam kwa hoja aliyoisema hapa kwamba wanatakiwa wahame kwa sababu wanatakiwa waolewe. Nasema mazingira magumu na mikopo ndiyo inayowafanya watumishi katika maeneo yetu hasa katika kada ya Ualimu, Afya na maeneo mengine waondoke katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ije na mfumo, ikiwezekana waweze kutafuta hata taasisi moja, ambayo itaweza kuwatafutia mikopo isiyokuwa na riba. Watumishi hawa hasa walimu katika maeneo yetu wanakopa sana VICOBA kutokana na hali ngumu ya maisha iliyoko kule. Leo hii utaniambia kwamba mwalimu anakwenda kufundisha darasani, lakini kila wakati anapigiwa simu za madeni na riba kubwa ambazo yeye mwenyewe katika mshahara hawezi kupokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama uangalie namna gani ya kutafuta, ikiwezekana uongee na Taasisi za kibenki, ambazo zitaweza kuweka mfumo mzuri kuwasaidia hawa watumishi wetu huko waweze kupata mikopo yenye riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba upungufu wa watumishi katika Jimbo la Msalala ni mkubwa sana, na nizungumzie katika Idara ya TAKUKURU. Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu, lakini nimefanya utafiti, Wilaya nzima, tunao watumishi 10 tu wa TAKUKURU. Katika watumishi 10 hao, ni wanne tu ambao wanafanya kazi za kwenda kufanya investigation huko katika Halmashauri hizi. (Makofi)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Cherehani.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchangiaji anachangia katika Wilaya ya Kahama na katika Jimbo la Ushetu pia Mheshimiwa Rais anapeleka fedha nyingi sana, lakini hatuna watumishi wa TAKUKURU wala Ofisi ya TAKUKURU; pia, anavyoongea mchangiaji nataka nimpe taarifa kuwa katika Jimbo la Ushetu tumemaliza Zahanati sita na Kituo cha Afya kimoja, lakini hatuna watumishi hata mmoja kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unapokea taarifa?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hii ya Mbunge mwenzangu kwa sababu ndio Mbunge ambaye tunatoka kwenye Wilaya moja. Wilaya ya Kahama ina Majimbo matatu kwa maana ya Ushetu, Msalala na Kahama Mjini. Kama ninavyosema, tuna watumishi 10 tu wa TAKUKURU na watumishi hao 10 wa TAKUKURU ni wanne tu ambao wanafanya shughuli hizo za tafiti na katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Msalala, Mama Samia Suluhu Hassan ameweza kutupatia kwenye bajeti ya 2021 zaidi ya takribani shilingi bilioni 24 kwenye miradi ya afya, kwenye miradi ya umeme na kwenye miradi ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Cherehani Ushetu nako fedha zimekwenda nyingi. Ni saa ngapi sasa hao wafanyakazi wanne tu wa TAKUKURU wataweza kusimamia miradi ile? Nimemwona Mkurugenzi wa TAKUKURU hapa ndugu yangu Salum yuko hapa, Mheshimiwa Waziri tuongezeeni na ikiwezekana mtuletee Ofisi kwenye Halmashauri zetu. Idadi hii ya watu 10 ambayo imetajwa hapa ndiyo idadi sahihi ya kwenye kila Halmashauri, lakini sisi tutaangalia Halmashauri tatu, zote tuna wafanyakazi 10 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, atuongezee na ikiwezekana atuwekee ofisi za TAKUKURU kwenye kila Halmashauri; kwa maana ya Halmashauri yangu ya Msalala, Halmashauri ya Ushetu na waliopo wabaki Halmashauri ya Kahama Mji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi kwa mchango wako. Nilimwita Mheshimiwa Nicodemas…

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Nilimwita Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga wakati huo wafuatao wanajiandaa: Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu tena kwa siku ya leo kuweza kusimama mahali hapa kuwawakilisha wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja kulingana na muda. Wilaya yangu ya Mbogwe ina upungufu wa watumishi 467 kwenye nyanja mbalimbali; walimu pamoja na kitengo cha afya. Namwomba Waziri wa Utumishi na Utawala Bora aangalie Wilaya yangu ili kusudi iweze kupata watumishi 467 ili wananchi wangu wa Mbogwe waweze kuhudumiwa kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo zipo changamoto zinazowakabili watumishi hasa kwenye upande wa afya. Unakuta mgonjwa amekuja huyu mtumishi anakwenda kumhudumia lakini hakuna vifaa tiba. Daktari anakutana na mgonjwa ambaye ameumia kwa ajali mfano ya bodaboda, hana vitendea kazi. Kwa kuwa, Wizara hii inahusika na watumishi, ni vyema Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri mtenge muda wa kuwaona kwanza watumishi hawa matatizo yao. Ni shida gani zinazowakabili katika upande wa utumishi wao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto nyingi kwa watumishi. Mimi nimekaa nao, nimekuwa mwanachama sana wa kupiga nao story watumishi ili kujua shida gani inayoweza kuwakabili kwenye kazi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uhamisho, Mheshimiwa Tabasam pale amezungumza japokuwa watu wameshindwa kumwelewa vizuri. Naomba nifafanue hiyo hoja. Suala la ndoa ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba kila mtu atakuwa na mwenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na tabia, mtu anapata uhamisho kwenda Mtwara kutoka kwa mfano, Bukoba; ina maana ndoa hiyo inakuwa ya ku-scratch scratch, hakuna ndoa pale tena. Maana katika taratibu za ajira jinsi zinavyotolewa hizi ruhusa ya kwenda kusalimia watu wako nyumbani ni kwa mwaka sijui siku 14 na vile vile akitaka mtu aende sasa kwenye familia yake, Serikali inatoa nauli tu bila kuangalia kwamba huyu mtu anaishi Mtwara, anatakiwa alale Dar es Salaam kesho yake ili aamkie kwenda kwenye familia yake, kunakuwa hakuna bajeti kama hiyo. Kwa hiyo, hilo Serikali iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala moja la hawa madereva. Mwaka jana wakati naingia humu nilizungumzia habari ya madereva. Katika sekta hii ya utumishi, madereva wanapata taabu sana. Ajali hazitaisha bila kuwasemea hawa watu. Kuna baadhi hata ya Waheshimiwa, wanakaa na madereva hawasemeshani ndani ya gari. Lililopo, dereva hapo anakuwa anafikiria tu jinsi gani ampige chini bosi wake ili kusudi maisha haya yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta dereva halipwi mshahara, hana mkataba wa kufanya kazi, anavyopelekwa dereva, yaani bora hata kuku au ng’ombe, yaani anaburuzwa tu. Unakuta Mbunge ametoka hata Bungeni bila kujua dereva huyu amekula, wala nini; kana kwamba yeye sio binadamu, ni kama anatumia remote. Inaniuma sana kwa kuwa maisha haya ya udereva na mimi nilishayaishi. Kwa hiyo, hii sekta sasa ione sababu, na Mheshimiwa Waziri…(Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa, unao mfano wa Mbunge ambaye anafanya hivi? Maana umetaja Wabunge hapa.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana, siyo vizuri kumtaja mtu. Watajijua tu wale wenye roho mbaya, wataweza kuacha.

MWENYEKITI: Basi ifute hiyo; kwa upande wa Wabunge, ifute hiyo.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, naifuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee tu kwa kuwatetea hawa madereva. Kuna dada yangu pale aliongelea suala la madereva wale wanaosafiri na magari makubwa (transit), wanapata taabu sana kwenye nchi hii, lakini hawa madereva wana chama na wana uongozi wao wa Kitaifa, nimekaa nao. Ukiwasikiliza madai yao ni ya msingi. Wanapopewa malori siku ya kuachishwa kazi hawaandaliwi kwamba lini mkataba wa ajira utasitishwa. Hawa madereva wana familia zao, wanalisha kupitia haya magari, lakini pale anapomdai tajiri mshahara wake, tajiri anamsingizia lose pamoja na mambo mengine ili kuweza kumfukuza huyu dereva. Kwa hiyo, kwenye sekta hii haijakaa vizuri, naomba Wizara hii kwa vile inahusika, iweze kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kwenye Halmashauri yangu nina wasomi wengi sana, hawajapata ajira. Mheshimiwa Lusinde amezungumza. Naomba sasa kama kuna uwezekano tufumue huu mfumo wa kuajiri kwa computer, maana computer hazichukui watu wa kijijini. Kuna walimu wengi vyeti vinaoza majumbani, hawapati ajira. Kuna madaktari wengi wamesoma, wako vijijini, wengine walishakata hata tamaa kabisa kuingia kwenye online hizi, maana hata kama uki-apply haupati kazi unakuta imefyatua tu watu wengine wa Dar es Salaam, Arusha lakini Mbogwe haionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa ushauri wangu, hizi ajira ziwe zinatolewa kila Halmashauri ili wasomi hawa tuliowasomesha kama Serikali waweze kuajiriwa. Kama kuna ugumu sana, Serikali muwe wawazi tu, kama nafasi zilishajaa kabisa hakuna haja hata ya kuwalazimisha watu kusoma sasa. Maana unamlazimisha mtoto anapomaliza Darasa la Saba akasome, atafute ajira, halafu kazi zinakuwa hazipatikani. Watu hawa wanakuwa hawajui kusoma, hawajui kulima na kufanya kazi zile nyingine ngumu. Wamefanya kazi yao ya kusoma na wamehitimu vizuri, lakini ajira hazipatikani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie suala hili la kuajiri watu upya. Wapo watu wanajitolea miaka na miaka, wengine wana miaka hadi 15 wanajitolea kwenye mashule kufundisha pamoja na kufanya mambo mengine, lakini hawapati ajira kabisa. Kwa hiyo, namwomba Waziri ajaribu kuliangalia hili suala ili kwenye Halmashauri zetu katika hizi ajira ulizozitangaza 3,200…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: …ziweze kupatiwa ufumbuzi, kila Halmashauri at least watoke watu mia mbili mia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)