Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Geita Vijijini kwa kuniamini kwa kura nyingi, hawanioni lakini mmo mtapeleka taarifa, kwa kuniamini na kunipa Jimbo la Geita Vijijini pamoja na mikwara mingi iliyOkuwepo kule maana helicopter ziliteremka zaidi ya mara nne. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kuzungumzia kidogo tu suala la Zanzibar. Ninyi ndugu zetu wa Upinzani acheni kuwachanganya watu, ngoma imetangazwa subirini mkashinde. Watu wanaojiamini hawaji hapa kutafuta sifa za kupiga kelele. Hata leo hii mkitengua uteuzi wangu tukarudia uchaguzi nawapiga bao kwa sababu ninapendwa. Kama mmeshinda kwa halali acheni kuja kuchukua sifa humu ndani za kuwadanganya watu mlishinda, mlishinda vipi, kama mlishinda mbona mko nje? Ujumbe umefika. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Mpango wa Maendeleo kama tunavyoendelea kujadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mambo mengi, hapa tunajadili Mpango na sisi Wabunge wapya tunasema Mpango huu ni mzuri isipokuwa tuusimamie. Hatutaki kuzungumzia Mipango iliyopita tunazungumzia Mpango tulionao. Huu Mpango ni mzuri na sisi wenyewe tutakabana kuukamilisha na kuusimamia. Wala tusianze kupotosha kwa kusema mambo ya miaka iliyopita sisi ni wapya tuzungumze haya tunayoanza nayo na kasi ya Mheshimiwa Rais aliyepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la reli. Upande wa reli naomba tuondoe hii sintofahamu. Sisi watu tunaotumia reli tunaomba kwanza kabla hatujajenga reli ya kwenda kuungana na Rwanda tuimarishe reli zetu ambazo zipo. Tusianze kuongeza mambo ya kutengeneza uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati kwetu huku kumeoza, tuimarishe kwanza ya kwetu, ya kwenda Mwanza, Mpanda, Kigoma baada ya hapo sasa ndiyo tufikirie kutafuta mahusiano na nchi zingine za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naona humu halizungumzwi kabisa, sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa, ukienda Mwanza leo barabara zinazokatisha airpot kwenda Igombe zilishafungwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa kiwanja cha ndege. Kwa kweli ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza umekuwa unasuasua kwa miaka mingi. Humu ndani sijaona kabisa wapi pamesema tutaujenga uwanja wa Mwanza uwe uwanja wa kimataifa na mkizingatia Mwanza ni mji mkubwa nadhani ukiondoa Dar es Salaam sasa Mwanza ndiyo inafuata. Pia Mwanza tuko kilomita 92 tu kwenda Serengeti lakini hatuna uwanja watalii wanatua Arusha wanatembezwa kilometa 300 mpaka 400 na zaidi, kwa nini tusiimarishe uwanja wetu wa Mwanza ili na Mwanza nayo ikawa na utalii, tukajaribu ku-balance na wenzetu wa Kanda ya Kaskazini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye Mpango huu tuzungumze kuhusu uwanja wa ndege wa Mwanza, ni tegemeo kubwa. Leo hii ukienda Mwanza watu wana hoteli hakuna wateja wa kulala. Sisi Wasukuma ni washamba tukiona ghorofa tunakimbia hatulali humo. Tulijenga ghorofa kwa ajili ya wageni, wageni wanaishia Arusha tu. Niombe sana Mpango huu tuachane na porojo tumalizie Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza. Eneo tunalo na nguvu kazi na kila kitu kiko Mwanza, naomba sana hilo tulizingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala la wachimbaji wadogo. Sikuona mahali kabisa linatajwa humu, sikuona! Kwa vile nilishazungumza na Profesa Muhongo nikamwambia Bunge lililopita ulipata figisu figisu ukaondoka, ukaingia kama mwanaume kwenda kugombea Jimbo, umerudi sasa na kasi ya Jimbo, porojo porojo tena hakuna. Kwa hiyo, sisi watu tunaotoka kwenye maeneo ya wachimbaji wadogowadogo tunahitaji kuwa na maeneo yetu ya kudumu, tena uwanyang‟anye Wazungu wala usihangaike kututafutia mapya. Kwa sababu sheria inasema kila baada ya miaka mitano unawanyang‟anya kiasi fulani unaturudishia, upeleke wataalam wako watafute maeneo yenye dhahabu za kina kifupi utukabidhi sisi wachimbaji wadogowadogo tuweze kuchimba na kupata dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la kilimo na viwanda. Ukianzia Musoma mpaka Bukoba sisi tunazungukwa na Ziwa, ni neema pekee ambayo tumepewa na Mungu. Watu wa Kanda ya Ziwa wala hatuhitaji elimu kubwa ya kutusaidia katika suala la ajira. Tulikuwa na viwanda vingi lakini vimekufa vyote. Sasa ni jinsi gani Serikali inakaa upya na watu wenye viwanda kule Kanda ya Ziwa waweze kuweka mpango mzuri ili viwanda vyote vile vinavyozunguka kwenye kanda ile viweze kufunguliwa na kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wana nia sana ya kuwekeza katika viwanda vya samaki na viwanda vingine. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu vijiji vya Kagu, Nyewilimilwa, Bugurula tunaweza kuweka viwanda hata vya unga wa muhogo lakini hakuna barabara, umeme na maji hatuwezi kuweka viwanda kama hivi viambatanishi havijafuatana pamoja. Kwa hiyo, niwaombe wahusika waweze kuzingatia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda kwa Kanda ya Ziwa tunalihitaji, hatuhitaji maelezo marefu. Nataka niwaambie watu wote wa Kanda ya Ziwa tutaungana kwa sababu tunataka kuwa na viwanda vyetu. Humu hakuna itikadi, watu wanahama vyama lakini tunachotaka ni viwanda, sitaki kusema ni nani mnaelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie suala la kilimo, sisi tunatoka sehemu za wakulima. Ukizunguka kule kwetu kote wimbo mkubwa ni kilimo cha pamba ambacho hakieleweki na hakuna mtu ataweza kukisimamia hata rafiki yangu Mwigulu hutaweza. Hii ni kwa sababu biashara ile imezungukwa na matapeli na Serikali inaona na tumeshindwa kabisa kuwadhibiti watu hawa.
Sasa mimi nilikuwa napendekeza na nikizungumza humu watu wananicheka, yako mazao ambayo hayahitaji kupigiwa debe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliuliza swali, niulize tena kwa sababu tuko kwenye Bunge la pamoja kwamba ni utafiti gani uliwahi kufanyika na waliofanya ni madaktari gani mpaka tukafika mahali tukapitisha mirungi kuwa dawa za kulevya? Nasema kila siku, ukienda Nairobi mirungi inasindikizwa na SMG za Jeshi la Kenya. Kuna ndege mbili Boeing zinateremka kwa wiki mara mbili kupeleka mirungi nchi za Ulaya. Sisi ukienda Tarime, Morogoro, Bunda kuna mirungi mingi, kwa nini tusirudie kufanya utafiti upya ili hii mirungi ikarudi kuwa zao la biashara ambalo halina utapeli, ni biashara inayoenda moja kwa moja? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia twende sambamba na bangi msinicheke, hata bangi mimi sina hakika kama inafaa kuzuiwa. Watafiti wetu waliofanya utafiti kuhusu madhara ya bangi hebu wafanye na utafiti wa madhara ya viroba. Tufanye utafiti kiroba na bangi ni kipi kinachowaumiza vijana wetu huko mitaani? Mimi naamini huko Usukamani mtu akila bangi analima heka mbili kwa siku. Sasa kwa nini tusiiboreshe tukaangalia madhara yake tukaiweka kuwa zao la biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani wako wengi tu wanaotumia bangi tunaweza kutoa mifano na wala hawana shida na ndiyo vigogo kwenye hili Bunge. Sasa kama ninyi wenyewe watunga sheria mnatumia, message imeenda. (Kicheko/Makofi)
WABUNGE FULANI: Aaaaah!
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la maji, tunatoka kwenye Ziwa lakini hatuna maji. Tunaamini hii kauli mbiu ya Mama Samia kwamba baada ya miaka mitano akinamama hawatahangaika na suala la maji itatekelezwa. Tuusimamie vizuri Mpango huu ili uweze kwenda sambamba na kauli ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie ndugu zangu wa Upinzani, tunapofika humu sisi wageni tunawashangaa. Tulipokuwa kule nje nilikuwa nikiwaona watu fulani sitaki kuwataja nahemkwa kusikiliza, lakini ukikaa humu ndani naona kama watu mnacheza maigizo. Mtu anasimama hapa anasema watu kondoo, wanaoitwa kondoo wenyewe wanashangilia, tunawafundisha nini watu wanaoangalia Bunge?
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, samahani Taarifa, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Kuhusu bangi au?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri unaoburudisha anaotoa mchangiaji Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, napenda kuumpa taarifa kwa sababu ameuliza kuhusu utafiti kwamba bangi ama mihadarati ya aina ya mirungi ina madhara gani kwa binadamu. Kitaalam napenda kumwambia bangi pamoja na mirungi inasababisha kitu kinaitwa alosto maana yake ni kwamba ukitumia kwa muda mrefu ile addiction ikazidi kwa muda mrefu unaweza ukaugua ugonjwa wa akili unaojulikana kama cannabis-Induced psychosis. Kwa maana hiyo, bangi ina madhara kwa afya ya binadamu na siyo vyema sisi kama viongozi tukatafuta namna yoyote ile ya kuchangia ili kuhalalisha kwa sababu za kiuchumi.
MBUNGE FULANI: Mwambie aache kuvuta bangi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma Taarifa hiyo unaipokea?
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea lakini nataka pia nimwambie afanye uchunguzi na viroba navyo pengine vina madhara zaidi ya mirungi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bangi, sigara na bia...
MWENYEKITI: Una dakika mbili zimebaki malizia.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hizo nazitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana unaona hata upande wa pili kuhusu huu mwongozo wa Mheshimiwa Kigwangalla hawauungi mkono. Naomba tuendelee kufanya uchunguzi wa kina. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia pia suala la elimu bure. Ndugu zangu wa Upinzani tumwogope Mungu, pengine ninyi hamtoki huko na wala hamjapokea taarifa kutoka kwenye shule zenu, hebu fanyeni ziara kwa kukashifu hili neno la elimu bure. Kaka yangu mmoja alikuwa anaomba Mwongozo hukumpa, hebu nenda kule Usukumani ukazungumze hayo mambo watakushangaa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure ndiyo sera yetu na hata Wabunge wengine wa CHADEMA na Madiwani wanaunga mkono, kwa nini tusibadilike, huu ni mwanzo. Kama ameahidi Mheshimiwa Rais elimu bure miezi mitatu au siku mia moja utamaliza matatizo yote? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ndugu zangu wa Upinzani wajazie nyama, zungumzia upungufu unaouona katika suala hili ili Serikali iyachukue ikafanye marekebisho tukirudi Bunge lijalo tunamsifu Rais kwa mpango wa elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushuru. (Makofi)