Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikusukuru sana wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hoja hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais ambaye kwa logic hasa na yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia ni Waziri wa hii ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujikita hasa kuongea kwa Habari ya dhana ya utawala bora. Mwaka jana siku kama hii wakati hoja ya ofisi hii imeletwa mezani niliomba Serikali kupitia aliyekuwa Waziri, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, kwa Habari ya Masheikh wa Uamsho waliokuwa wamekaa miaka minane jela bila kupelekwa Mahakamani. Na nilipoiomba Serikali, naishukuru Serikali kwamba, ilifanyia kazi vizuri na Masheikh hawa waliachiwa. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiri, pia niliomba tena Serikali kwa ajili ya kutekeleza dhana ya utawala bora wakati ule, kushughulika na suala la Mashekhe waliokuwa Arusha. Masheikh zaidi ya 18 ambao nao waliwekwa ndani miaka mingi bila kesi yao kusikilizwa, nashukuru Serikali imeyatimiza hayo na Mashekhe hao waliachiwa ahsante sana nakushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo liko jambo moja tu ambalo nataka kulizungumzia leo ambalo ni dhana ya utawala bora. Mara nyingi Viongozi Wakuu kama Rais, wanapotoa matamko yenye lengo la kuijenga nchi, viongozi walio chini ambao ni wajibu wao kutekeleza matamko hayo, wanatakiwa wawe makini sana na mahiri sana katika kuyatekeleza matamko ambayo yametolewa na Viongozi Wakuu kama Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano nimnukuu Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan katika mkutano wake mmoja alisema: “ninaomba muwapange wamachinga” hayo ndiyo maneno aliyosema, hakusema naomba muwafukuze wamachinga, hakusema naomba muwapige wamachinga, hakusema naomba muwavuruge wamachinga. Mheshimiwa Rais alisema naomba muwapange wamachinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili lilileta mambo ya ajabu, dhana ya Mheshimiwa Rais iwapange wamachinga ilikuwa njema, nzuri yenye maana na tija kwa wamachinga wenyewe. Lakini watekelezaji walipoanza kutekeleza dhana hii, wakaanza kuwakimbiza wamachinga kuwapiga, kuwanyang’anya mali zao, bomoa mabanda yao, haikuwa dhana ya Mheshimiwa Rais na hii inaharibu dhana ya ujumla ya utawala bora kwa wale watekelezaji walio chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano, Mheshimiwa Rais aliposema wapangeni wamachinga hakumaanisha wafukuzwe. Kupanga wamachinga siyo lazima uwaburuze ukawaweke kwenye kibanda, dhana ya machinga anamfata mteja, machinga hafuatwi na mteja hiyo ndiyo dhana ya machinga. Ukimchukua machinga ukamuweka kwenye kona siyo machinga tena, ukamuweka kwenye duka siyo machinga tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano tena, sehemu kama Uingereza kwa mfano ukienda Tottenham au East London kuna nyakati ambazo wanafunga mitaa kuwaruhusu wale vendors wauze vitu vyao, hata wakati fulani hapa wakati wa utawala wa Mzee Kikwete ile barabara yetu ya karibu na Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi Jumamosi walikuwa wanafunga ili hawa watu wauze vitu vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Watendaji wenye akili yenye kupanga vizuri, wangewaza badala ya kuwafukuza wamachinga wawe angalau na machinga’s day, waseme wamachinga fanyeni kazi yenu Jumatatu au fanyeni kazi yenu Jumanne au Jumatano kuwe na siku moja wapo ambayo wamachinga wanaruhusiwa kufanyakazi zao ili kuruhusu utaratibu mwingine uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifanya kama ulivyofanya kwa wamachinga leo, nakuhakikishia wamachinga watarudi tena mitaani kama kawaida. Huwezi kuwaweka kwenye banda wamachinga na ukafikiri watakaa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hawa machingas ni fans wetu wakubwa wa uchaguzi na ndiyo wapiga kura wetu wakubwa sana tunapowavuruga leo watatuvuruga siku chache zijazo, tutavurugika kweli kweli na tusijifanye hatuoni. Kuna msomi mmoja aliwahi kusema ni afadhali kisu cha Daktari kinachopasua ngozi kwa lengo la kuponya, kuliko dawa ya kuondoa maumivu inayomponya mtu kwa muda halafu ikampeleka kwenye maumivu ya kifo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme ukweli, kwenye suala la machinga we are on the wrong destination, tumeenda vibaya na wamachinga hawa watatuhukumu siku chache zijazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa kwenye Kata ya Kawe, Mikocheni, Bunju na maeneo mengine ya Jimbo la Kawe nina wamachinga wa kutosha, ninaomba nijitoe kabisa kwenye hili suala la kuwakimbiza wamachinga na kuwapeleka kona moja baada ya nyingine kwa mambo ambayo wangeweza kutengenezewa na wakakaa vizuri na wakaenda vizuri. Kwa hiyo, hapa hatujaenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nisema kuna baadhi ya watu wanamharibia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais alikuwa na maana njema kabisa, wapangwe wamachinga! Kupangwa angesema wamachinga fanyeni shughuli zenu za machinga Alhamis peke yake, siku zingine mtulie nyumbani, hiyo ndiyo maana ya kupanga wamachinga. Huwezi kusema wamachinga wajipange wakati ni watu wenye njaa wanahitaji chakula, after all kusema ukweli hatuwezi kufikia mpangilio kwa viwango vya Ulaya, hii vurugu mechi yetu ya wamachinga ndiyo utalii wenyewe ule kwetu huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mismatch ya machinga ndiyo yenyewe. Kwa hiyo, nataka kusema hapa hatujaenda sawa na lazima tujue lile soko la Ilala Machinga litengenezwe halina machinga mle sasa hivi, tunatengeneza masoko mengine ya machinga hayatakuwa na matching guys wataendelea kuzurura mitaani, kwa hiyo lazima tuwe na namna nzuri ya kuwa handle hawa mabwana kwa sababu nao ni Watanzania wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho...
MWENYEKITI: Naomba utumie dakika moja kuhitimisha Mheshimiwa Gwajima.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu zimekimbia haraka. Naomba sasa nihitimishe kwa kusema ni vizuri viongozi wetu wakubwa wanapotoa maelekezo, watekelezaji walio chini waangalie modality nzuri ya kutekeleza hayo yaliyosemwa na kiongozi ili kuondoa kumfanya kiongozi aonekane ameharibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)