Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii adhimu. Kwa sababu ya muda, naomba nijikite kwenye mambo manne kwa ufupi na ninaamini wenzangu watanielewa.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, tunayo hoja ya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri ameyazungumza ambayo tumekubaliana. Ameyataja katika hotuba yake. Naomba kushauri kwamba haya ambayo tumekubaliana, basi sasa mchakato wa kisheria uendelee ili mambo haya yaeleweke kisheria kwamba sasa ni mambo tuliyokubaliana na yanatambulika kisheria. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, tunayo hoja ya mazingira. Mimi natoka Jimbo moja linaitwa Mwera. Kwa lugha ya kawaida, Mwera ni mbali sana, lakini kiuhalisia Mwera ipo mjini, imezungukwa na majimbo mengi sana. Mwera ni chimbuko la maji, ni chimbuko la chakula, ni chimbuko la matunda na ni chimbuko la Zanzibar. Kwa sababu Mwera hii ndiyo ambayo imeleta Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwa sababu tumejaribu lakini bado tunayo changamoto. Mwera tunayo changamoto ya uharibifu wa mazingira, hasa kwa sababu maji yanatuathiri sana. Sasa kwa ufupi kabisa naomba Wizara yako na hili lichukuliwe kwa sababu tulishazungumza na hali halisi unaielewa, Mwera unaielewa na umeshakwenda siyo mara moja; siyo mara mbili na siyo mara tatu.
Mheshimiwa Spika, naomba sana Mwera itazamwe kwa jicho maalum ili kujua inasaidiwaje kutatua tatizo letu la mazingira. Mwera inaumia, Mwera inaangamia, Mwera inazama kwa sababu kila mvua inapokuja Mwera tunaingia kwenye matatizo ya mafuriko. Naomba sana iwe ni mradi maalum wa kusaidia Mwera ili kuiondolea tatizo la kuzama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine dogo kabisa, tunazungumza issue ya nafasi za ajira za Muungano. Hizi nafasi kwa mujibu wa sheria, tumekubaliana Zanzibar watapata ngapi, wenzetu watapata ngapi? Sasa sipo kwenye hoja hiyo; hoja yangu ipo kwenye hili; mara nyingi tunaangalia vijana wetu ambao wamepata nafasi ya kwenda kwenye Jeshi la Kujenga Taifa au Jeshi la Kujenga Uchumi. Sasa hiki kimekuwa kigezo kikubwa, kwa hiyo, vijana wetu wengi wanakosa nafasi hii kwa sababu hawakupata nafasi ya kwenda kwenye majeshi haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama Serikali hatuna uwezo wa ku-absorb vijana wote hawa wakaenda kwenye majeshi yetu, hatuna nafasi hiyo, kwa hiyo, hawawezi kwenda wote kwenye Jeshi la kujenga Taifa wala hawawezi kwenda wote kwenye Jeshi la kujenga Uchumi, nawaomba sana, kigezo hiki cha kwamba mtu amepitia kwenye JKU au JKT kisiwe kigezo pekee. Hiki kiwe ni nyongeza, lakini muhimu iwe elimu na vitu vingine ndiyo viwe vinazingatiwa. Siyo kwamba eti kwa sababu hakwenda JKT au JKU, ndiyo kigezo cha kumfelisha, naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha mwisho, amezungumza pale kaka yangu issue ya kuheshimiana. Naomba nirudie hapa, kwamba ili mradi sisi ni binadamu, hakuna nafasi kwamba tutakuwa wakamilifu mpaka tunayoingia kaburini. Kwa hiyo, nawaomba sana wenzetu, taaluma ya Muungano mwendelee kuitoa kwa sababu bila ya hivyo tutaendelea kulumbana kila siku; na bila hivyo kila siku tutaendelea kuona tuna matatizo. Matatizo ni sehemu yetu na yataendelea kutatuliwa taratibu, lakini kubwa tuendelee kutoa elimu kwa sababu bila elimu, kila siku tutazungumza hayo hayo.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)